Halmashauri hiyo mpya, inaundwa na kata 17 na vijiji 87. Ilianza kufanya kazi rasmi Julai, mwaka jana, ilipopatiwa baadhi ya vitendea kazi na watendaji ambao walikuwa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Miongoni mwa watumishi wao ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, ambaye sasa amekuwa Mkurugenzi katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.
Akizungumza katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Desemba mwaka jana, Ng’itu anataja baadhi ya vitendea kazi alivyopatiwa ni magari sita ambayo hata hivyo ni mabovu.
Ng’itu anasema hilo linawafanya wanatumie fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo ya magari hayo, wakiwa hawana vyanzo vya uhakika vya mapato.
Anakiri kuwa safari ndefu ya kuhakikisha halmashauri inajitegemea kutokana na changamoto nyingi inazokabiliana nazo, zinazohitaji msaada kutoka ngazi za juu serikalini.
Ng’itu alitoa ufafanuzi huo katika kikao cha kumchagua Mwenyekiti wa Halmshauri. Alitaja baadhi kuwa ni kukosa jengo rasmi na wanalazimika kutumia ofisi za kata.
“Halmashauri ya mji wa Nanyamba, kwa sasa ofisi zake kwa maana ya makao makuu, inatumia ofisi za Kata ya Nanyamba. Majengo ambayo awali yalikuwa yanatumika kama ofisi za kata ndio yanayotumiwa sasa na Mkurugenzi na Watendaji wote waliopo katika mji huo kwa maana ya makao makuu,” anasema Ng’itu.
Anaongeza: “Pia kuna ofisi ambazo zipo nje ya hili jengo ambalo tunazungumza, tumepata vyumba vitano kutoka kwa Shirika la Ukombozi. Hivi vyumba vitano vinatumiwa na Idara ya Afya.”
Katika azma ya kujenga ofisi na nyumba za watumishi, halmashauri hiyo imelipa fidia katika eneo lenye ukubwa wa hekta 40, ambalo litaiwezesha ofisi kupima na kupanga mji, kwa ajili ya ujenzi wa mji ambako pia kutakuwa makao makuu ya halmashauri hiyo.
MADENI
Anasema kutokana na utaratibu wa kupokea watumishi na wakuu wa idara kutoka halmashauri zingine nchini, wamejikuta wanakabiliwa na madeni yanayofikia Sh. milioni 242.5, deni lililogawanyika katika maeneo matatu.
Ng’itu anataja la eneo la kwanza ni ukarabati wa ofisi ya Kata ya Nanyamba, ili itumike kama ofisi ya kuanzia ya halmashauri hiyo na wameingia mkataba na mkandarasi wa Sh. milioni 49.3 na hadi Desemba mwaka jana, alikuwa hajalipwa .
Eneo lingine ni utengenezaji samani za ofisi na magari, ambayo anasema kuna uwezekano magari hayo yasitumike tena muda mfupi ujao.
“Pia tuna madeni ya watumishi. Mtumishi anavyohama kutoka kituo kimoja kwenda kingine, ana stahili zake za kisheria, ambazo kimsingi kwa watumishi wanaotoka Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na watumishi waliohamia kutoka halmashauri mbalimbali. Jumla imetengeneza deni la Sh. milioni 160,” anasema Mkurugenzi huyo.
“Hizi pesa ndizo ambazo zingewawezesha watumishi wakija huku kuona wanawezaje kuanza kazi, kujitafutia vitanda, mazingira ya kuishi na vitu vingine, lakini hadi sasa hivi hawajalipwa hata shilingi moja,” anafafanua.
MFUMO DUNI WA MISHAHARA
Pia, anasema halmashauri haina mfumo sahihi wa kulipa mishahara kwa watumishi wake, jambo linaliowafanya waendelee kutumia mfumo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, hali inayowanyima Namba ya Utambulisho kutoka mfumo wa malipo, itakayoiwezesha kupata ruzuku kutoka serikalini.
Kwa mujibu wa Ng’itu, halmashauri ina watumishi pungufu wakiwamo wanasheria na wakaguzi wa ndani.
Wakati kuna jumla ya idara 15, huku wakuu wa idara waliopo ni wanane pekee, hali inayosababisha pengo la watendaji saba.
“Halmashauri ya mji Nanyamba, tangu imeanzishwa Julai Mosi 2015, haijapokea fedha yoyote kutoka serikali kuu. Kwa hiyo fedha zinazotumika ni vile vyanzo vidogo ambavyo tunakusanya wenyewe.
“Katika mipango ambayo tunayo hadi tarehe ya leo, hatujapokea fedha yoyote. Kuna mipango mingi ambayo haijaanza kutekelezwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
“Pia fedha ya uendeshaji wa ofisi ambayo kimsingi tunatakiwa kuipokea katika mgawanyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mpaka hivi sasa hatujaipokea. Hizo fedha zimeshakuja tumejaribu kufuatilia, lakini sasa hivi ni wiki ya tatu hatujapokea hata shilingi.” anasema Ng’itu.
CHANGAMOTO NA MIKAKATI
Anasema kuna mikakati ya halmashauri kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hizo, ikiwamo kuingiza mipango katika bajeti zake zijazo.
Wananchi wa halmashauri hiyo nao wanakiri changamoto, licha ya kupiga hatua ya kupata halmashauri mpya. , ikiwamo kulazimika kufuata baadhi ya huduma katika Halmashauri ya Mtwara.
Chikomele Jabiri, ni mzee anayesumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari. Analalamika kuhusu ukosefu wa dawa katika Zahanati ya Dinyecha, na analazaimika kuzifuata katika Kituo cha Afya Nanyamba, kwa gharama kubwa.
“Natakiwa kwenda kupima pale sukari kila wiki. Nikifiika kwanza naandika cheti kwa Sh. 2, 000,halafu nakwenda kupima damu kwa Sh. 2,000 halafu nikisharudi huko, naandikiwa dawa zinazoweza kufikia sh. 8,000. Sasa hiyo ukichanganya na 4,000 ni sh. 12,000 ndio nipate dawa za kutumia wiki moja,” anasema.
Mkazi mwingine, Hamisi Kamwendo, analalamikia shida ya maji ambayo ni kero ya kipindi kirefu na miradi mbalimbali ambayo waliitegemea kutatua kero hiyo, imekwama.
Anautaja mradi mmojawapo ni wa AMREF, ambao uliishia katika kusambaza matenki na mabomba ambayo hayajawahi kutoa maji.
Kamwendo anasema kuwa, chanzo cha maji kinachotumika katika halmashauri hiyo ni kimoja na hakina umeme, hali inayoigharimu fedha nyingi kununua mafuta ya kuendesha jenereta.
HUDUMA ZA JAMII
Kuhusu huduma za afya, Ng’itu anakiri changamoto ya wakazi wa sehemu tofauti kutegemea Kituo cha Afya Nanyamba na kingine cha Mkombozi kinachomilikiwa na shirika la dini.
Anasema wanaazimia kuingia ubia na shirika hilo la dini, ili kiwe kituo teule cha afya, huku wakiendelea na mpango wa kuwa na zahanati ya halmasahuri.
Kuhusu wazee, anasema alishaviagiza vituo vya afya na zahanati kutenga maeneo maalum ya kuwahudumia, jambo aliloahidi atafuatilia kuhakiki utekelezaji wa agizo lake.
Kuhusu kero ya maji, Ng’itu anasema tatizo lililopo ni la umeme na kwamba jenereta linalotumika sasa halina uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu, kwa sababu ya uhitaji wa mafuta.
Anasema halmashauri inalazimika kutumia lita 200 za mafuta kila siku kwa ajili ya jenereta, gharama zisizolingana na mapato kutoka miradi ya maji.
“Kuanzia mwaka juzi, Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini, waliweka utaratibu, ili umeme uweze kufika kwenye kile chanzo.
“Nilikutana na Meneja wa Tanesco mkoa, ameniambia mchakato umefikia hatua za mwisho na iliyobaki ni kwa mkandarasi kutia saini mkataba,” anasema.
Mhandisi wa Tanesco mkoa wa Mtwara, Daniel Kyando, anawaondoa hofu wakazi wa Nanyamba, akiwaambia kuwa ‘mambo yamekaa sawa’ kwa huduma kupatikana ndani ya kipindi kifupi.










