JEAN BAPTISTE JOSEPH FOURIER

22Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JEAN BAPTISTE JOSEPH FOURIER
  • Gwiji wa hisabati aliyepewa uprofesa miaka 19; akokotoa uzito wa dunia

Siku ya Jumatatu kama ilivyo jana, lakini wiki iliyopita, magwiji wa somo la hisabati walikuwa na tukio la kitaifa kuadhimisha walichokiita ‘Siku ya Pai’ ambayo ni sehemu ya nadharia ya hisabati.

Jean baptiste joseph fourier.

Ni mkusanyiko uliofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Ni tukio lenye upekee katika ulingo wa taaluma, ikizingatiwa ni somo lililoko katika hali mbaya katika taaluma nchini, kiashiria kamili kikiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne, yakiongoza kufanya vibaya.

Licha ya hali ngumu kudhihirika kupitia matokeo ya mitihani ya Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), hata uongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, ulikiri uwanjani Mnazi Mmoja kuwa ‘hali ni ngumu.’ Kwa hiyo hali ni mbaya!

Kwa marejeo hayo hayo, wana – hisabati na wasio wana hisabati wanapotaka majina yenye mchango mkubwa wa kihistoria katika taaluma hiyo duniani, jina la Mfaransa Jean Baptiste Joseph Fourier, aliyeishi kati ya mwaka 1768 na 1830, lina upekee katika mchango mkubwa kwa maendeleo ya somo hilo.

Katika kukumbuka mchango huo, siku ya jana ina nafasi yake katika kuainisha kumbukumbu hiyo, kwani ndiyo tarehe aliyozaliwa mwana-hisabati Fourier.

Mbali na historia ya kwamba alikuwa ‘moto’ katika taaluma ya hisabati, mwaka 1820 alitoa michango ya nadharia tatu muhimu, mbili ikiangukia katika fani ya Fizikia na moja Hisabati.

Moja ya nadharia ya ki-mahesabu aliyotoa katika Fizikia, ilikuwa maboresho ya nadharia za mtaaluma Isaac Newton, kuhusiana na mwenendo wa joto.

Miongoni mwa nadharia za msingi katika hisabati aliianzisha na kufanyiwa maboresho na wasomi wa baadaye, bado ndio wanasimama leo wakimtambua kuwa muasisi wa nadharia iitwayo “Fourier Transform” aliyoiwakilisha kupitia kitabu chake.

Hata kanuni zinazotmumika leo katika hisabati za algebra, nadharia za mwana- hisabati Fourier zimo ndani yake.

Pia msomi huyo ana mengi makuu aliyoyavumbua katika mwaka 1820 kupitia nadharia zake kuhusu joto.

Alikokotoa uzito wa dunia na umbali wake hadi iliko jua na kiwango cha joto kinachofikia dunia na sababu zake.

Hata msingi wa nadharia zilizopo duniani kuhusu joto linaloipata dunia hivi sasa, kutokana na joto la mazingira ni matokeo ya nadharia zake za hisabati katika joto la dunia.

ALITOKEA WAPI

Huyu ni mtoto wa fundi cherehani wa Kifaransa, ambaye naye hakudumu na wazazi wake kwani alipokuwa na umri wa miaka minane tu, tayari alishapoteza wazazi wake.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wasamaria walimpeleka katika shule jirani na kwao ambayo ilikuwa inamilikiwa na jeshi la nchi hiyo.

Huko shule ndiko alipoanza kuonyesha cheche zake darasani, hususan katika somo la hisabati linalondelea kutetea jina lake hata miaka 286 tangu afariki

Hata hivyo, hakuweza kuingizwa katika mafunzo ya jeshi, kutokana na kukosa sifa ya vogezo vya wakati huo, ikiwemo umasikini na yatima.

Hata hivyo, alibaki katika mafunzo ya kawaida katika chuo kinachomilikiwa na jeshi akitikisa darasa katika hisabati.

Muda mfupi baadaye, mwaka 1787 akiwa mawanafunzi mwenye miaka 19 tu, alipandishwa hadhi na kuwa Profesa akiwa mwanafunzi katika chuo kingine alikohamishiwa.

Mbali na uanafunzi wake, pia alitumikia jukumu la kusaidia taaluma akiwa mwanafunzi wa kipekee mwenye kipaji.

Kutokana na upeo mkubwa wa kijana huyo, alialikwa kufundisha masomo mengine kama Falsafa na Historia ambazo uelewa wake nao ulikuwa umezazma mno.

Mwaka 1795 alirejea katika chuo chake cha zamani cha École Normale cha mjini Paris, ambako alipandishwa hadhi na kupewa nafasi ya kuwa mchambuzi wa taaluma.

Mwaka 1998 alipelekwa nchini Misri katika chuo kilichomilikiwa na nchi yake kuendeleza majukumu ya kisayansi, sambamba na majukumu mapya ya kisiasa, ambako nchi yake ilikuwa na maslahi.

Kuna wakati alipewa hadhi ya kuwa Gavana wa eneo kubwa la Misri na wakati huohuo mkuu wa chuo alichokitumikia. Mwaka 1801 alirudishwa nyumbani Ufaransa.

Aliporudi alipewea kazi ya kuandaa maandiko mengi ya kuhusiana na historia na suasa ya Misri.

Katika miaka 14 baada ya hapo, pia alizama mni katika utafiti wa kisayansi na hisabati na ndipo alipoibuka na nadharia nzito, ikiwemo inayohusu joto na inatikisa dunia hadi leo hii.

Kuna wakati aliandaa maandiko yanayohusiana na taifa la Ufaransa na siasa za taifa la Napoleone katika mwaka 1815, jambo lilomfanya aingie matatani.

Baada ya hapo alijikita katika ulingo wa kitaaluma, alikotumikia hadi kifo chake, siku ya Mei 16 ya mwaka 1830.