Inapoangaliliwa katika elimu ya juu, suala linaigusa zaidi umma, kwani ndiko ambako wanapatikana wataalam wa kitaifa katika kila nyanja.
Katika elimu ya juu, wahusika ni kuanzia wahitimu wa elimu ya shahada, stashahada za juu, na vyeti vya juu zaidi kama vile stashahada ya uzamili, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu.
Kilio kikubwa kinasimama katika namna dhana ya ‘kusoma’ katika taasisi ya elimu ya juu inavyoendeshwa. Imebadilika na inaendelea kubadilika kadri muda unavyopita katika sura ya kudidimia.
Taasisi za elimu ya juu kila mahali duniani, zina majukumu makuu matatu ambayo ni kufundisha; kutoa ushauri wa kitalaam na kufanya utafiti.
Katika nadharia ya ufundishaji wa elimu ya juu, ambako kunatarajiwa mwanafunzi ameshaandaliwa katika kiwango cha kuwa na msingi unaojitosheleza, uko tofauti kidogo.
Ufundishaji unaopaswa kufanyika katika elimu ya juu ni wa mhadhara (lecturing), yaani mwalimu anatoa maelekezo zaidi na mwanafunzi anatakiwa kujitegemea kwa mengi, mojawapo ni kusoma vitabu.
Hilo lilifanyika nchini katika siku za mwanzo tangu vyuo hivyo kuanzishwa kati ya miaka 20 na 30 baada ya uhuru na kuweza kutoa matunda makubwa ya wahitimu wanaojiweza kitaaluma.
Mfano hai unapatikana katika vyuo kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Ardhi ambacho sasa ni Chuo Kikuu na Chuo cha Ardhi na kilichokuwa Chuo cha Maendeleo ya Uongozi (IDM) – Mzumbe (sasa Chuo Kikuu Mzumbe).
Lakini kadri muda ulivyopita, ubora wa wahitimu unazidi kuyumba. Hapo ndipo lawama zinapotokea, kila upande unaowajibika na elimu ukirusha mpira kwa mwenzake.
Wasomi wa elimu ya juu, mfano mmojawapo UDSM wakituhumu mzizi wa matatizo upo katika udhaifu kutoka elimu ya shuleni.
Kwa jumla, mabadiliko makubwa yaliyotokea ni kwamba utamaduni wa kusoma ukaanza kuteremka na inadaiwa hali ikaanza kuwa mbaya, baada ya uzao wa tuisheni kuanza kujiunga na vyuo vikuu mwishoni mwa miaka ya 1990.
Ikumbukwe tuisheni ni tunda la kuwepo mfumo huria katika elimu nchini, ambao mzizi wake umesimama katika mageuzi yaliyotokea mwaka 1985.
Nikiwanukuu maprofesa wawili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwanasosholojia marehemu Seithy Chachage na mwanasheria Chriss Peter – Maina, walikuwa na kilio kikuwa dhidi ya uzao wa tuisheni kujiunga na vyuo vikuu.
Ikumbukwe, ni katika zama hizo ambazo serikali nchini ilikuwa katika mipango ya kupanua elimu ya juu ili kuwezesha wahitimu wa shule wengi kujiunga na vyuo vikuu.
Profesa Maina alitoa ushuhuda katika kikao cha wahitimu wa UDSM mwaka 1998, namna mwanafuzi mpya wa mwaka wa kwanza kumfuata akiomba mwalimu huyo amfundishe tuisheni, kwani hakuelewa vizuri darasani.
Iilikuwa jambo lililomshangaza sana Profesa Maina, hata akalazimika kutoa ushuhuda wa mageuzi yalikofikia katika namna ya kusoma.
Profesa Chachage naye akatoa ushuhuda wa mshangao aliyoupata katika kikao hicho hicho, mwanafunzi wake alipomfuata ofisini akimuomba ‘material’ aliyofundishia darasani ili naye akatoe ‘photocopy.’
Hapo ikatoa ujumbe fulani juu ya aina ya malezi ya kitaaluma walioandaliwa nayo vijana hao na mahali yalikofikia, wakifanya marejeo na maandalizi ya madarasa kama yao waliondaliwa wao.
Ubunifu katika taaluma na kusoma vitabu umetoweka na hali inaegemea katika utamaduni wa kudurufu maandiko ya mwalimu na kuvizia kurejesha maandiko hayo katika mitihani na kadhalika.
Ni utamaduni au mfumo ambao ulibatizwa na wanafunzi wenyewe kama ‘kudesa’ ikiwa ni lugha fulani ya kudhihaki mfumo huo wakiamini si wa kutumia akili, kama ilivyokuwa zamani wa kusoma vitabu.
Lakini kadri miaka inavyobadilika na hasa kuibuka matumizi ya nyenzo za kurahisisha kufikiri – kompyuta hali imebadilika na kuwa mbaya zaidi. ‘Kudesa ‘kumezoeleka’ na si jambo geni tena.
Utamaduni wa ‘kudesa’ umechukua hatua zaidi ya mabadiliko kwamba, wanafunzi hao uzao wa tuisheni waliojaa kila kona ya elimu, sasa wamehama kutoka ‘kudesa’ hadi kukariri kile wanachofunzwa, maarufu kama ‘kumeza.’
Unajengwa uzao wa kundi mahiri katika kukariri walichoelekezwa, huku wakiwa na asilimia ndogo ya kuelewa walichofafanuliwa na ama mhadhiri au profesa wa somo husika.
Wakati wanafanya hivyo, kundi hilohilo linaingia masomoni likiwa na uwezo mdogo sana katika kuelewa lugha ya Kiingereza inayotumika kufundisha.
Hali hiyo inaendana na udhaifu mkubwa wa vijana hao katika kumudu somo la hisabati ambalo ni ‘injini’ ya kila somo kwa maana inahitajika kila mahali katika taaluma, hali inayojidhihirisha katika elimu ya juu.
Mtazamo mpana uliopo kwenye udhaifu wa hisabati, ndiyo unaojitokeza katika masomo ya sayansi. Udhaifu huo wote unaanzia shuleni.
Kuna malalamiko kwamba, katika baadhi ya vyuo baadhi ya wahadhiri nao wameanza kuyumba kutoka katika dhana iliyopigwa vita na marehemu Profesa Chachage na Profesa Maina, kwamba mtazamo muhimu ni kuelewesha na badala yake wanahamia katika kukaririsha.
Hivyo, wanafunzi wamehama kabisa kutoka mfumo wa kusoma kwanza ili waelewe na kisha wajiandae na mtihani unatokana na alichojifunza na badala yake wamejikita katika kukariri.
Mfumo wanaoutumia wanafunzi sasa ni kusoma katika mtindo wa kukariri waliyoyajifunza ambao wameubatiza kama ‘kumeza’ na kuyarejesha siku ya mtihani maarufu kama ‘kutema,’
Kwa bahati mbaya, baadhi ya wahadhiri nao wamekuwa abiria wa mfumo huo, ikizingatiwa wapo wanaotokana na uzao wa mfumo huo wa usomaji.
Kwa lugha nyingine kuna wahadhiri wanaowapinga marehemu Profesa Chachage na Profesa Maina, kupitia matendo yao.
Kama alivyoeleza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kupitia utafiti wake alipogundua ‘madudu’ kuna mengi ya kurekebishwa katika elimu nchini.
Wataaluma katika ngazi ya juu wakiwa na nafasi yao ya kumsadia waziri katika vita dhidi ya usomaji wa ‘kudesa’ na ‘kumeza’ na wakahamia katika kusoma vitabu.
Katika dhana ya maboresho huwa kunaelezwa mabadiliko hufanywa katika idadi ya vitu, sambamba na ubora wake. Hicho ndicho kinachotakiwa kufanyika katika vyuo vikuu nchini ambavyo idadi yake inazidi 50 .










