Kabla ya maneno hayo kunakuwa na mlio kama kengele hivi, ndipo maneno hayo yanatamkwa.
Na kweli mnaangalia mnaona ndege iko hewani inatua taratibu kwa madaha hivi, kabla ya matairi yake kugusa ardhi.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha ya Watanzania kwenye miaka ya 1970, hadi katikati ya miaka ya 1990 hivi.
Nazungumzia kuzuru au kwenda Uwanja wa Ndege Dar es Salaam, wakati huo kabla haujaitwa wa Julius Nyerere.
Napoandika makala hii kuna watu wanaweza kuona kama ndoto, au aina uhalisia wowote hasa vijana wa kizazi cha sasa na ambao hawajawahi kusomuliwa aa kuliona hilo.
Kwenye miaka hiyo, watoto, vijana na watu wazima waliokuwa wakiishi jijini Dar es Salaam, au hata wale waliotoka mikoani kuja Dar kwa likizo, kusalimia ndugu au kikazi, walikuwa wakipata fursa ya kwenda kwenye Uwanja wa Ndege ili kuziangalia tu zilivyopaki pale uwanjani, zinavyotua na kupaa.
Nadhani asilimia 90 ya watoto wa zamani waliozaliwa au kukulia Dar es Salaam miaka hiyo watakuwa wameshazuru mara kadhaa Uwanja wa Ndege.
Kwanza kabisa ulikuwa ni kama mtoko wa familia. Ni kama baba au mama anavyowachukua watoto wake na kuwapeleka mbuga za wanyama, 'beach', au sehemu nyingine yoyote ya michezo ambayo watafurahi.
Moja ya sehemu hizo ilikuwa ni Uwanja wa Ndege Dar es Salaam. Hasa siku za wikiendi au sikukuu watu walijazana uwanjani kuangalia ndege zinavyotua na kupaa. Na hii ndiyo ilikuwa ndiyo raha yenyewe uwanjani hapo. Siku ambayo huoni ndege ikipaa au kutua watu hawafurahi, hasa watoto.
Siku ya bahati zikiwepo ndege kubwa zinapaa au kutua inakuwa ni ya furaha sana kwa watu wote na zikishaondoka watu pia wanaondoka.
Kuna watoto watundu nao waliokuwa wakiishi maeneo ambayo si mbali na uwanja, wakishatoka shule, wanakwenda.
Wakati wa likizo ndiyo kabisa, baadhi ya watoto wanashinda huko huko.
Pia ilikuwa huwezi kufika bila kukuta vijana na watu wazima. Kumbuka kuwa hapa nauzungumzia ule uwanja wa ndege wa mwanzo kabisa ambao kwa sasa umekuwa kama ni uwanja maalum kwa kushukia viongozi au kuna tukio maalum. Ni ule wenye jengo lenye rangi jekundu ambalo ukitoka mjini uwanja wa mwisho kabisa. Ule ndiyo ulikuwa uwanja mkuu zamani.
Kule juu kulikuwa na mabenchi mengi, maalum kwa watu au wananchi kwenda kuangalia. Na hakukua na matatizo yoyote, tena bure bila kiingilio.
Baada ya kukamilika uwanja mwingine ambao unajulikana kama terminal 1, kule juu nako walifanya kama ule mwingine na watu wakawa wanamiminika kwenda kuangalia ndege kama kawaida.
Dalili za marufuku zilianza katikati ya miaka ya 1990, hasa baada ya kushamiri kwa mambo ya ugaidi. Kwanza kabisa mambo yalianza kwenye ule uwanja ambao wakati huo uliitwa mpya, watu wakaanza kusachiwa kabla ya kupanda ngazi kwenda juu kuangalia.
Kila mtu mtoto na mkubwa alisachiwa kama vile inavyokuwa unapoingia kwenye sehemu zozote nyeti. Baadaye ikawa hakuna namna tena, wakazuia kabisa.
Terminal 2- na 3 zilijengwa miaka mingi baada ya zuio, na ndiyo maana kama utakuwa mdadisi utagundua utofauti wa ujengaji kati ya kile cha mwanzo kabisa ambacho kwa sasa ni maalum tu hakitumiki kwa ndege za raia, na kile kilichojengwa badala yake.
Aina ya ujenzi wake unaona kabisa hauruhusu watu wa kawaida kufika kwa urahisi, tofauti na hivi vya sasa vilivyojengwa baada ya ugaidi ambavyo mbali na kujengwa kisasa zaidi, lakini kuna ugumu wa kuufikia kama huhusiki kusindikiza mgeni, kupokea au kusafiri.
Tuma meseji 0716 350534.










