Mwanasheria kutoka katika Shirika hilo linalojikita zaidi katika kutoa elimu ya kisheria na kusaidia katika upatikanaji haki katika maeneo mbalimbali, Zakia Msangi anasema ipo tabia ambayo imejengeka katika jamii kwamba umiliki wa vitu vyenye thamani ikiwamo ardhi, nyumba na magari ni kwa wanaume pekee.
Zakia anasema kasumba hiyo ipo pia hata kwenye ndoa hususani katika eneo la umiliki wa mali na ardhi, kwamba mali nyingi huandikwa jina la mume na si mke tofauti na sheria inavyoelekeza.
“Kwa wanandoa nako tumekuwa tukipokea kesi nyingi zinazolalamikiwa mali nyingi kumilikishwa mume na hivyo baadae inapokuja kwenye suala la mgawanyo endapo wanandoa hao wakiachana au mmoja wao akifariki huleta shida au kuzua migogoro,”anasema Zakia.”
“Lakini sheria inaeleza kwamba mke na mume wanaweza kumiliki ardhi pamoja, yaani hati ya nyumba ikaandikwa majina mawili la mume na mke, na hata inapokuja kwenye mgawanyo inakuwa rahisi zaidi kuliko kuandika jina la mtu mmoja.Kisheria, mali zilizopatikana kwenye ndoa ni za wanandoa wote.Kwa Tanzania ndoa zinazotambulika ni za kidini, kiserikali, kimila na kuna zile za watu walioishi pamoja zaidi ya miaka miwili kama mke na mume, hawa nao wakiachana huwa mgawanyo wa mali lazima uwe sawa.”
“Ni mapenzi watu au familia kupendelea kuandika jina la baba kama kichwa cha familia katika umiliki wa ardhi au mali, lakini shida kubwa huwa inatokea linapokuja suala la mgawanyo wa mali hizo baadae.
Zakia anasema inapotokea mtu alirithishwa au kumiliki mali kabla ya kuingia kwenye ndoa, hiyo ni mali yake na si ya wanandoa.
“Isipokuwa kama alipewa au alimiliki kabla namna hiyo lakini alipoingia rasmi kwenye ndoa wakaamua waiendeleze kwa pamoja, hapo ndio inakuja kuingizwa kwenye mali ya wana ndoa,”anasema Zakia.
“Haijalishi mwanamume ndio alichangia pakubwa kwenye mali au ni mwanamke, inapokuja kwenye suala la kugawanya ilimradi walikuwa ni wanandoa, mgawanyo unagawiwa sawa.”
Pia, anasema miongoni mwa kesi wanazopokea, wanawake wengi hususani wale ambao huwa ni watafutaji au wachangiaji wakubwa wa mali kwenye ndoa, huwa hawapendi usumbufu wa mgawanyo wa mali kwenye ndoa zao pale wanapoachana au kutokea mgogoro na wenza wao ali hupenda kufuata utaratibu na kuhakikisha kila kitu kimemalizika salama na kuendelea na maisha mengine.
“Lakini kama mwanaume ndiye alikuwa akichangia pakubwa kwenye upatikanaji wa mali, huwa hawapendi sana kufuata utaratibu, inapotokea wanaachana na wenzi wao, wao hukumbilia kuwafukuza wanawake bila kutaka wapate chochote hata kama walichangia upatikanaji wa mali za ndoa na hapo tunasema kufanya hivyo ni ukatili wa kijinsia,”anasema Zakia.
Anasema miongoni mwa maeneo ambayo bado kuna shida kubwa inayohitaji kutumia vizuri sheria katika kulishughulikia ikiwamo kutoa elimu kwa jamii kubadili mtizamo ni katika eneo la umiliki wa ardhi kwa wanawake.
“Mfano tumekuwa tukipokea kesi nyingi za wanawake kunyimwa kumiliki ardhi hata inapotokea kwenye mgawanyo wa mali hasa upande wa mirathi, yaani mwanamke yeye ni wa kumpatia kuku, bata, vyombo vya ndani halafu mali kubwa kama ardhi, magari na nyumba humilikishwa mwanaume.
“Kwenye mgawanyo huo wa mirathi, sisi kama wanasheria ndipo tunaingia hapo kwa ajili ya kusaidia kwa kusimamia sheria inavyoelekeza. Inabidi katika hili tuendelee kutoa elimu jamii ibadilike, ibadili mtizamo wake. Sheria iko wazi, kwamba umiliki wa ardhi au mali ni haki ya kila mtu bila kujali ni mwanamke au mwanaume.”
Mwanasheria huyo wa WiLDAF anafafanua pia katika eneo la umiliki wa mali kwa waliofunga ndoa kupitia dini.
Anasema kwa wanandoa waliofunga katika dini ya Kikristo, anayetambulika ni mke na mume mmoja lakini kwa Wailsamu inatambua mume mmoja na wake wanne.
Anasema inapokuwa ni mke na mume mmoja ni rahisi zaidi kwenye mgawanyo wa mali kwa sababu katika hillo, kinachoangaliwa ni kuanzia tangu wameoana kama ni mwaka huu wakaachana mwaka kesho, wanaangalia kile kilichopatikana wakati huo na siyo vilivyopatikana kabla.
“Wanaangalia kila mmoja katika kipindi hicho alichangia nini, kama ni matofali, mchanga au hata hakuchangia vitu vya namna hiyo lakini alikuwa anakupatia support yako kwa namna nyingine au alifanya hata kazi za kumwagilia hayo matofali au kipindi cha ujenzi huo nao ni mchango unaotambulika.”
“Kwa hiyo inapotokea mgawanyo wa mali kama wameamua kuachana, mahakama ndio chombo pekee chenye mamlaka ya kugawa mali.Na ugawaji wa mali unaangalia mchango wa kila mwanandoa katika upatikanaji wa mali husika.”
Kuhusu wenza ambao waliamua kuishi kama mke na mume kwa kipindi cha miaka miwli au zaidi bila kufunga ndoa, Zakia anafafanua kwamba nao hao sheria inatambua kwenye mgawanyo wa mali endapo wakaamua kuachana baada ya hapo au mmoja akifariki.
“Mfano sheria inatambua pia kwamba hata kama mmeishi kama mke na mume kwa kipindi cha miaka miwili na hawakubahatika kufunga ndoa na ikatokea mkaachana, kama kuna mali ambazo mlipata kwa kipindi hicho mnagawana na itaangaliwa kila mmoja ameshirikije kwenye kuipata hiyo mali.”
Zakia anasema wenza hao ambao waliishi pamoja kama mume na mke bila kufunga ndoa kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi halafu baadae wakaamua kufunga rasmi au kuihalalisha kwa kwenda kuifunga kanisani, serikalini au msikitini mambo hubadilika kidogo kuhusu umiliki wa mali.
“Lakini pindi mtaamua kuhalalisha kwa kwenda kanisani au msikitini, kuanzia hapo ndipo tunahesabu kwamba ni ndoa, huko nyuma kila aliyekuwa akimiliki chake ndipo kitaitwa chake.










