Tuachane na dini kwenye masuala ya msingi

20Mar 2016
Ibrahim Mkamba
Dar
Nipashe Jumapili
Tuachane na dini kwenye masuala ya msingi

KATIKA moja ya hotuba zake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuonya kuhusu udini kwa kubainisha kwamba mtu akikosa hoja kwenye kujadili suala fulani, huigeukia dini.

Mwalimu Julius Nyerere.

Huenda akili za wengi kwa sasa si nzuri kwenye kujenga hoja kiasi cha kukimbilia kwenye dini kila wanapojadili suala zito.

Hivi karibuni kumezuka mambo pengine ya ajabu ndani ya mijadala mitandaoni hasa ile ya kijamii kuonyesha upungufu wa mtu kiutendaji kwa kuangalia ameajiri Waislam wangapi ama Wakristo wangapi.

Mtu akikosolewa anatetewa kwa hoja kwamba kafanyiwa hivyo kwa sababu yeye ni wa dini fulani. Hata uteuzi wa watendaji unaangaliwa kwa jicho la huyu wa ana imani gani tene kwa uteuzi ameteua wangapi wa dini yake na wangapi si wa imani yake.

Pia huhesabiwa Waislam wako wangapi na idadi ya Wakristo pia huchunguzwa linapokuja suala la kuwawawajibisha kwa makosa.

Hili ni jambo ambalo kama Watanzania Bara wangekuwa hawahusiki na dini zote, hoja hizo zingeleta mpasuko.

Wapo ndugu wa damu wanaotofautiana kidini, kutokana na sababu mbalimbali za kijamii. Kuna waliooa au kuolewa na waamini wa dini nyingine waliowabadilisha dini wenza wao.

Je hawa wangeweza kubadilisha imani za jamaa wengine wote wanaowahusu wake au waume wao? Jibu ni hapana haiwezekani.

Lakini ni lazima watakuwa na ushirikiano na ndugu wa wenza wao waliobaki kwenye imani zisizo za waume au wake wao.

Kuna watoto wa baba na mama wa madhehebu tofauti wanafuata zaidi dini za baba zao au za upande walikokulia. Kuna wenye marafiki wakubwa na washirika wa hali ya juu wa kibiashara wa imani zisizo zao.

Kila siku wapo wanaohudumiwa na watu wa dini nyingine. Funga kazi ni marafiki wa kike na wa kiume (wapenzi), wapo wengi kwenye mahusiano hayo wakiwa na dini tofauti.

Kwa ufupi, dini zote, zinatuhusu, hivyo tunapojadili masuala tofauti ya ujenzi wa nchi, tujadili masuala hayo bila kuhusisha dini isipokuwa kama mjadala wenyewe unahusu dini.

Kama ni lazima dini kuhusishwa kwenye mjadala huo, ingefaa basi hilo lije kwenye hatua ya pili au ya tatu. Kwa mfano, inaposemwa taasisi fulani imejaa waamini wa madhehebu fulani, kilichopaswa kuanza taasisi hii imejaa watendaji wabovu na kazi hazifanywi inavyopaswa.

Pili, sababu ni kwamba watendaji hao hawana sifa za kushika nafasi zao hapo kazini. Tatu,wameajiriwa kwa upendeleo bila kufuata vigezo.

Nne, sababu ya jambo hilo ni kwamba watu ni wa dini fulani na wameajiriwa si kwa sababu nyingine wala si kwa kuzingatia vigezo bali kwa sababu kiongozi mkuu amewapenda kwani wote wanashiriki imani moja.

Tano, wafanyakazi wa dini nyingine wameajiriwa kwa sifa zao na hawafanyi kosa hilo linalofanywa na wenzao wa dini tofauti na sita, ajira ya hapo haifanywi na vyombo vilivyopo kikanuni bali kwa maamuzi ya mtu mmoja.

Mfano mwingine, huyu kawajibishwa.Hakufanya kosa la kufanya aondolewe kazini kisheria. Pili, kaondolewa kwa sababu ya nje ya kazi.

Tatu, sababu hiyo ni kwamba yeye ni wa dini fulani na mwenye dini tofauti na hiyo kafanya hayo hayo lakini hakuchukuliwa hatua .Bila mtiririko huo wa hoja kwenye mifano hiyo miwili hakuna mantiki ya kuhusisha dini kwenye mijadala kama hiyo.

Ni vizuri tuache dini ziendelee kuwa dini na shughuli zingine zisizozihusu ziendelee hivyo. Kampeni hii ya dini ni mbaya.Ukisema taasisi fulani ni ya dini fulani na hilo likizoeleka, ikitangazwa kazi hapo, watu wengi wa imani nyingine huacha kuomba wakijua hapo si kwao. Matokeo yake wanaomba zaidi wa dhehebu moja na kwa sababu wanazo sifa, wanaajiriwa wengi. Kwa nini isiwe hivyo wakati wale wa dini nyingine walikata tamaa?

Hata unaposema chama cha siasa ni cha dini au cha wana eneo fulani, unashangaa nini kinapovuna wanachama wengi wa imani hiyo na eneo hilo kwa kujiona kwamba hicho ndicho chama chao?

Nani alaumiwe hapa kati ya wanachama hao “wanaofuata maelekezo” na kiongozi wa umma “aliyetoa maelekezo” kwa watu wa dini hiyo au eneo hilo kuwaambia “chama chenu ni hicho”?

Ni wazi kiongozi huyo wa umma ndiye atastahili lawama kwa kutoa kauli iliyosababisha ubaguzi.
Ni jambo la kushukuru Mungu kwamba huku kulikokuwa kunaitwa Tanganyika, kila mmoja wetu anahusika na dini zote na hivyo kampeni zozote za kutufarakanisha haziwezekani.

Wenzetu visiwani hilo halipo kwani kimsingi kule ni kama kwa dini moja.

Hebu tujenge taifa moja imara lenye mshikamano kwa kuacha kujadili mambo kwa misingi ya udini. Tuna imani tofauti na hivyo kila atakayeshika nafasi fulani lazima awe wa madhehebu tofauti .Tusiangalie dini yake bali tutathmini sifa zake na uwezo wake kutimiza majukumu yake..

Mungu ibariki Tanzania.