‘Ma RC’ ondoeni migogoro ya ardhi, dhuluma,unyanyasaji

20Mar 2016
Dar
Nipashe Jumapili
‘Ma RC’ ondoeni migogoro ya ardhi, dhuluma,unyanyasaji

RAIS John Magufuli, ameteua wakuu wa mikoa kutoka taaluma mbalimbali kuanzia askari, makada wa kisiasa hadi wanasheria ili kumwakilishi kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara, wakuu hawa pia ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wa mikoa wanayoiongoza wakiwa na jukumu la kulinda amani na usalama.

Wakuu wa Mikoa wakila kiapo cha kuzingatia maadili ya viongozi wa umma.

Uteuzi huo umeleta sura mpya kwani wamo Makamanda wa Polisi, majenerali wastaafu, mawaziri wa awamu zilizotangulia kadhalika kuna wakuu wa wilaya na mikoa kwa nyakati tofauti hivyo kuwa na uzoefu wa kutosha katika nyanja ya uongozi.

Hongereni na karibuni katika kuwatumikia wananchi ambao matarajio yao makubwa ni kwa serikali ya awamu ya tano, ambayo imejinasibu kwa kubana matumizi, kupambana na ufisafi, watumishi wazembe na kuelekeza nguvu kuhakikisha kuwa Watanzania wa maskini wananufaika na raslimali zao.

Ma RC tunawategemea mkafanye kazi kwa kasi ya Rais Magufuli kuhakikisha kero za msingi za wananchi zinapata ufumbuzi wa kudumu, tena wawe watatuzi wa migogoro na siyo chanzo cha mitafaruku hiyo.

Kila mkoa unakabiliwa na changamoto zake na zipo zinazofanana kama za migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambazo utatuzi wake waweza kufanana au kuwa na tofauti ndogo ya mila na desturi za eneo husika, hivyo ni jukumu la wawakilishi wa Rais kujikita katika utatuzi wa kudumu na kutokubali kutumiwa.

Mamia ya wananchi wamepoteza maisha kwa migogoro hiyo ambayo ingeweza kumalizika mapema, lakini baadhi ya viongozi kwa kujua au kutokujua wamechochea moto kwa kupendelea upande mmoja na kukandamiza mwingine hivyo kulundika kinyongo na kisasi mioyoni mwa jamii za waathirika.

Mathalani, Mgogoro wa Kiteto uliohusisha mkoa wa Dodoma na Manyara baadhi ya viongozi walitajwa kuhusika katika kuchochea mgogoro huo, kwa kujikuta wanakuwa sehemu ya mgogoro kwa kuwa wanatoka katika moja ya jamii inayohusika na mapambano hayo na kusahau wajibu wao na kusababisha kupigana na kulikoleta vifo, kujeruhi na uharibifu wa mali.

Baadhi ya viongozi walitumia nafasi zao kujigawia ardhi katika wilaya mbalimbali na kuingia kwenye migogoro na wananchi waliokiwa wanamiliki maeneo hayo awali, lakini kwa nguvu ya fedha na mamlaka yao wanamiliki maeneo katikati ya miji ambayo ukifuatilia kwa kina kulikuwa na mchezo mchafu.

Hatutarajii RC wa Dk. Magufuli kushiriki kwenye uovu huo ambao ni dhuluma kwa wananchi wa kawaida, washiriki utatuzi wa migogoro na siyo kuingia kwenye mgogoro na kuchukua upande.

Changomoto nyingine uwepo wa viwanda vilivyobinafsishwa lakini havizalishi chochote, kwa mujibu wa ahadi za Dk. Magufuli wakati kampeni ni kuwawajibisha walioshindwa ili viendelezwe na kukuza uchumi , badala ya wamiliki wake kuvitumia kama dhamana ya mkopo benki, huku manufaa yaliyotariwa kupatikana kutoka kwenye miradi hiyo ikiyeyuka.

Ili nchi iendelee ni lazima kuwe na uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, vitavyozalisha bidhaa zitakazouzwa nje na ndani kuiwezesha Tanzania kuwa na fedha za ndani na za kugeni. Ni chanzo cha maendeleo mijini na majijini kwa upande wa ajira na uwekezaji.

Ni lazima kuwe na usimamizi wa viwanda husika, kumsaidia Rais kufuatilia kwa karibu uzalishaji au kushindwa kufanyakazi na vingine kubadilisha matumizi.

Jingine ni mashamba makubwa yanayoshikiliwa na wawekezaji na hayajaendelezwa tena baadhi yakigeuza matumizi .Mathalani, mkoani Kilimanjaro kuna mashamba makubwa mengi ambayo wawekezaji wanayashikilia kwa kuyatumia kama dhamana ya mkopo na wanaendesha kilimo cha maua au mazao ya muda mfupi kinyume na mkataba wa ununuzi.,

Mashamba mengi ya mkoa wa Kilimanjaro yalikabidhiwa wawekezaji na vyama vya ushirika kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kahawa, lakini wengj wameyatelekeza, wanalima maua, mbogamboga ambazo wanasafirisha nje huku baadhi wakiendesha utalii kwa kuwa na mashamba ya wanyama ‘zoo’ na nyumba za kulaza watalii ambao wakiwa chumbani wanauona mlima Kilimanjaro, hivyo kujikusanyia mapato yasiyotozwa kodi.

Wengine wanafuga farasi na wanapokea watalii wanaoona baadhi ya wanyama na ndege katika mashamba yao na baadaye kupanda mlima Kilimanjaro. Baya zaidi bodi ya shamba ambayo ndiyo inawajibu wa kusimamka kitega uchumi hicho hairuhusiwi kufika kwenye shamba hilo.

Baadhi wamewekwa mkononi mwa mwekezaji kwa kuridhika na vijisenti vidogo vidogo wanavyopewa na kusahau wajibu wao wa kuwawakilisha wanachama wa vyama vya ushirika ambao ndiyo wamiliki wa shamba.

Zipo nyingi ambazo zinaweza kujaza ukurasa lakini kwa uchache tunawaomba wakuu wa mikoa wakawe chache ya maendeleo kwenye maeneo yao, wananchi wafanyekazi kwa bidii, wasimamie huduma muhimu za kijamii kama maji, tiba, elimu na miundombinu ambako wananchi wengi ndiko wanakonung’unika.

Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki Afrika.
Mawasiliano::salome.kitomari@guardian.co.tz