Tanzania nayo inapitia kwenye njia mbalimbali za ustawishaji michezo na hii imelazimu kutumbukia kwenye matumizi ya viwanja bandia.
Ingawa viwanja hivi vimeanza kutumika tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960, lakini kwa Tanzania matumizi yake hayajaanza muda mrefu.
Baadhi ya viwanja vya soka vya nyasi bandia nchini ni pamoja na Uhuru, Karume na Azam Complex, vyote vya Dar es Salaam na Gombani cha mjini Pemba.
Viwanja vingine ambavyo navyo vipo kwenye mpango wa kuweka nyasi bandia ni Kataba uliopo mkoani Kagera na Nyamagana uliopo mkoani Mwanza.
Kwa wenzetu, nchi kama Canada asilimia 95 ya viwanja vyote vya soka ni vile vya nyasi bandia kutokana na hali ya hewa inayowakabili.
Kwa mfano, fainali za soka za Kombe la Dunia Wanawake zilizofanyika mwaka jana nchini humo, mechi zote zilichezwa kwenye viwanja vya nyasi bandia.
Je, kuna madhara gani mchezaji anaweza kupata kwa kucheza kwenye viwanja vya aina hii? Mtafiti wa masuala ya michezo nchini, Dennis Manumbu anabainisha katika makala hii.
Anasema utafiti unaonyesha kuwa mchezaji hukumbana na msuguano wa ngozi kwenye vikanyagio vya miguu na viatu kutokana na nyasi hizo kutumia plastiki katika kutengenezaji wake.
Anabainisha kuwa kipindi cha jua, nyasi bandia hupokea na kuhifadhi joto kwa muda mrefu, hivyo kuvifanya viatu kuwa na joto kali linaloathiri miguu ya mchezaji.
“Hali hii imekuwa inasababisha ugonjwa wa malengelenge na kumfanya mchezaji ashindwe kucheza kwa kiwango kizuri,” utafiti umebaini.
Pia utafiti uliofanywa kwa wachezaji, unaonyesha kati ya wanasoka 20 waliowahi kuchezea mpira katika kiwanja cha nyasi bandia wamethibitisha viatu vyao vimekuwa vikipata joto kali kiasi kwamba hulazimika kuvimwagia maji ili kupunguza joto.
Pia utafiti umebaini madhara mengine kuwa ni misuli ya mchezaji hukakamaa kutokana na ugumu wa uwanja.
“Kwenye viatu kuna njumu, ambazo zinapokanyaga chini hukutana na ugumu hali inayoifanya misuli kukakamaa na wakati mwingine kusababisha maumivu kwenye maungio (joints) kama goti na kifundo cha mguu. Matatizo kama haya humpunguzia mchezaji uwezo wa kucheza uwanjani,” anasema.
Utafiti umebaini mpira unapochezwa kwenye viwanja hivyo hudunda kwa kasi sana tofauti na uwanja wenye nyasi za kawaida.
Mpira unapodunda kwa kasi, kunamalazimisha mchezaji kwenda na kasi hiyo, hivyo kujikuta akiuyumbisha mwili mara kwa mara, jambo ambalo anaweza kupata matatizo ya kukakamaa misuli au kupata maumivu ya nyonga.
“Katika kuendana na kasi hii baadhi ya wachezaji wamekuwa wanateguka magoti na maungio ya makanyagio ‘ankle’,” anasema.
Anaongeza: “Magonjwa haya kwa wachezaji yamekuwa yanashusha kiwango chake. Unaweza kuona jinsi timu ya Azam inayofanyia mazoezi yake kwenye uwanja wenye nyasi bandia inavyopata majeruhi wengi wakati wa mazoezi,” anafafanua.
Pia anasema mpira humpotezea mchezaji mwelekeo na kwamba tatizo hili ni kubwa wakati mvua ikinyesha.
Anasema utafiti umebaini wakati wa mvua, wachezaji hupata tabu kuumiliki mpira kwa sababu nyasi bandia zinapoloa huteleza na mpira huenda kwa kasi.
“Unaweza kuona mchezaji anausubiri mpira uliopigwa kwake, lakini ghafla unapodunda unapoteza mwelekeo na mchezaji kushindwa kuucheza (lack of ball control),” anasema.
Manumbu anasema utafiti unaonyesha viwanja vyenye nyasi bandia vinasababisha magonjwa (injuries) kwa wachezaji kwa kiwango cha asilimia 22 ukilinganisha na viwanja vya nyasi asilia.
Lakini pia utafiti umekwenda mbali zaidi na kubaini kuwa, wachezaji wanaweza kupata magonjwa ya maambukizi (infection).
Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya bakteria hukaa kwenye plastiki zinazotumika kutengeneza viwanja hivyo, hivyo mchezaji anapocheza anaweza kukutana na vijidudu hivyo na kunasa kwenye miguu yake.
Suala la kansa na viwanja hivyo nalo limetajwa kuwa moja ya athari wanazoweza kupata wachezaji.
FAIDA ZAKE
Manumbu anasema faida kubwa kwenye uchumi ni kwamba hupunguza gharama za utunzaji wa uwanja husika.
“Tunachonufaika nacho ni kupunguza gharama za utunzaji viwanja na mwonekano mzuri wa uwanja wa kuchezea ila wachezaji soka wanaathirika kiafya,” anasema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Wanamichezo Tanzania, Dk. Nassor Matuzya akieleza kitaalamu kuhusu athari zinazotokana na nyasi bandia anaanza kwa kusema: “Duniani hakuna kitu kisicho na madhara.”
Anasema katika kuangalia athari ya viwanja vyenye nyasi bandia, viwanja hivyo vina vipira vidogo vyeusi wanaangalia athari nyasi bandia (pastiki) na athari za pumba (vimpira vidogo vyeusi) zinazomwagwa kwenye nyasi hizo.
Dk. Matuzya anasema nyasi bandia ziko katika mfumo kama viwembe vidogo vidogo, hivyo zinapoachwa ndefu humsababishia mchezaji kuumia kwa kupata michubuko.
Akizungumzia kuhusu pumba (vipande vidogo vya plastiki), anasema vimetengenezwa katika hali ambayo inaleta athari kwa mwanadamu kwa sababu hutoa vumbi.
“Kuna madini jamii ya chuma kama zink, ambayo yana madhara kwa binadamu, ikiwemo kusababisha aleji na vumbi hilo kama litatua kwenye ngozi au vidonda ambavyo havijafungwa, kunaweza kusababisha kansa,” anasema.
Pia anasema mhusika anaweza kupata madhara kwenye mapafu, figo na ini kwa njia ya kuvuta fumbi la pumba hizo.










