Msuguano unachukua sura katika kiwango kwamba wananchi wananyooshea vidole uongozi wa halmashauri na hasa katika ngazi za chini kwamba wanauza ardhi yao ya kitalii, uwindaji na kilimo kinyemela.
Ni hali iliyojitokeza hivi karibuni katika mkutano wakati wakazi wa Kijiji cha Idodi walipocharuka kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iringa Vijijini amuondoe Ofisa Mtendaji wa Kijiji chao.
Idodi pia ina sifa nyingine kuwa ni hifadhi na eneo la uwindaji kimataifa.
Malalamiko hayo yanabeba tuhuma kwamba, Ofisa Mtendaji amekuwa akishirikiana na baadhi ya viongozi, wakiwamo madiwani.
Ni mkutano uliowakutanisha wanakijiji zaidi ya 150 na uongozi wa Halmashauri, kidole cha lawama kikinyoshwa zaidi kwa uongozi wa kijiji.
Ilikuwa hoja yenye msukosuko mkubwa iliyomfanya Mwenyekiti wa kikao, Daniel Chiza, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri aonekane kuelemewa na kuamua kutamka:
Ni mkutano uliowaeta viongozi wa halamashauri hiyo na uongozi wa kijiji kukusanyika kuwasikiliza wananchi hao waliorodhesha malalamiko na tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi wa kijiji na diwani wa kata yao.
Malalamiko yao ni kuuzwa ardhi ya kijiji kwa waliowataja kuwa wawekezaji.
Wanakijiji wanalalamika kwamba, m,bali na kuuza ardhi yao kinyemela, viongozi wanashindwa kutoa taarifa muhimu za mapato na matumizi ya kijiji.
SAUTI YA WAKAZI
Derick Edson ambaye ni mkazi wa Idodi, anasema migogoro ni mingi kuhusu ardhi ya kijiji na wamekuwa wakiwahitaji wawekezaji wanaodaiwa kutwaaardhi yao, waje wajieleze kwenye mikutano ya hadhara, lakini hawajitokezi.
Edson analakamika katika baadhi ya matukio, walishawahi kuchanga pesa kuwatuma viongozi wao kijijini kuwasafirisha hadi Dar es Salaam, kuwaleta kijijini kuzungumza, lakini hakuna kilichofanikishwa.
Mwanakijiji Idrisa Msekwa anasema:“April 15 Mwaka huu baada ya kusomwa ajenda ya kuomba ardhi ekari 500, tunavyohoji ‘tumpe au tusimpe, faida gani ipo ama tufanyaje’ Mheshimwa Diwani alikuwa analazimisha sana kugawa hiyo ardhi.
“Baada ya kukataa tena kwa ‘mbinde’ huku tukiyumbishwa kama mahindi, tukashinda. Hivyo hivyo, ili ardhi isiuzwe, ameanza kampeni ya kuzunguka kitongoji kwa kitongoji akisema anaenda kutoa elimu kwa wananchi.”
Mkutano huo ulionekana mgumu kwa meza kuu, kutokana na kutawaliwa na kelele za wananchi, baadhi wakiwazomea na kuwakatisha baadhi ya viongozi wanapoongea kijiji pamoja na diwani wa kata ya Idodi Onesmo Mtatifikolo.
Viongozi hao waliomwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, wamekubaliana kuunda tume itakayofanya kazi kwa wiki mbili kuchunguza madai yaliyoorodheshwa na wanakijiji, ikiwamo ugawaji ardhi kinyemela.
Mwanakijiji Yona Olemesye, anasema kuwa katika awamu ya kwanza kuna mwekezaji aliomba ekari 50 kwa ajili ya kujenga hoteli, lakini baada ya kujenga aligeuza sehemu ya uwindaji.
Anaongeza katika awamu ya pili, mwekezaji aliomba kupewa ekari 100 kwa ajili ya kujenga uwanja wa ndege, lakini uongozi wa kijiji ulimuongezea ekari 400, jambo linalozua maswali mapya.
MWELEKEO WA UAMUZI
Mwenyekiti wa kikao - Chiza, anasema suala la kupitia muhtasari wa maamuzi na vitu vingine, vitafanyika na katika tume itakayoundwa itakuwa na wajumbe wanakijiji.
“Mtanitafutia watu wanne au watano watakuja hapa na Mkaguzi wa Ndani na Ofisa Utumishi tupitie, ili na sisi tuwe tunajiridhisha,” anasema na kuongeza;
“Kwa sababu naona serikali yenu (ya kijiji) imefika mahali hamuiamini kama inapitia muhtasari.”
Mwanasheria wa Halmashauri, Mohammed Mgimwa, anaahidi kuomba kuipitia sheria ndogo ya kijiji kukagua utaratibu wa ugawaji ardhi kama ulizingatia vigezo.
ORODHA YA MALALAMIKO
Miongoni mwa malalamiko yanayotajwa na wanakijiji ni ardhi yao kugaiwa bila ya ushirikishwaji wa wananchi
Jingine wanalodai ni kukaribisha wawekezaji kuanzisha miradi katika ardhi ya kijiji, bila ya wananchi kufahamu maudhui ya mikataba.
Wananchi wanalalakmika kuwa, haweafahamu wala hawapewi fursa ya kufahamu mapato na matumizi yatokanayo na uwekezaji kijijini kwao.
Katika suala la mikutano, uongozi wa kijiji unatuhumiwa kutoitisha mikutano mikuu kwa wakati na kusoma taarifa za mapato na matumizi na katika fursa chache, ripoti zimekuwa zikisomwa kwa ubabaishaji zaidi.
Sehemu kubwa ya kilio cha wanakijiji ni dai la hekta 20 za ardhi yao iliyouzwa na uongozi wao na fedha hizo hazionekani kwenye mfuko wa kijiji na hadi sasa hawajui kiasi kilichopo kwenye mfuko wa kijiji.
Waliendelea kusema kuwa hadi sasa hawajui kijiji kina fedha kiasi gani ambazo zimetokana na vyanzo vya mapato ya kijiji chao.
Katika madai yao wananchi wanasema walishaandika barua kwa mamlaka mbalimbali za kiutawala mkoani
Wananchi waliandika barua walizotuma nakala kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye ni mbunge wa Jimbo hilo, Mkuu wa Mkoa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa,Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Iringa,Ofisa Tarafa pamoja na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Idodi.
HALI SI SHWARI
Wakati Ofisa Mtendaji wa Kijiji akijibu malalamiko ya wananchi, kulitokea malumbano yaliyoendana na kuibuliwa mabango yenye ujumbe mbalimbali mkutanoni.
Akihitimisha mkutano, Mwenyekiti Chiza alitamka:“Nikisema tunamhamisha Ofisa Mtendaji, nitakuwa nimekosea.
“Katika hili nitaunda tume itakayojumuisha wawakilishi wenu wanne,viongozi wa serikali ya kijiji na wataalamu kutoka halmashauri.
“Hawa watafanya kazi kwa muda wa wiki mbili (kuanzia wiki iliyopita) na watatuletea majibu ili tuweze kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayethibitika katika hilo.”
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Idodi anaorodesha wawekezaji wa Idodi, kwamba wakubwa ni wanane na wadogo 46.
“Mimi sitaki kuegemea upande wowote. Kinachotakiwa hapa mwekezaji amepewa eneo na ameshindwa kuliendeleza na kulipatia mapato kwa wakati basi kuanzia leo ardhi hiyo ni mali yetu na asitufuatilie,” anasema Vedasto Rweyemamu mkazi wa kijiji










