Hifadhi ya Ngorongoro ilivyoihamisha Karatu kijijini hadi mji mkuu

20May 2016
John Ngunge
KARATU
Nipashe
Hifadhi ya Ngorongoro ilivyoihamisha Karatu kijijini hadi mji mkuu

KATI ya mwaka 1974 na 1975, Karatu ilikuwa moja ya vijiji kati ya vijiji vingi vya Ujamaa na Kujitegemea vilivyoasisiwa na sera ya wakati huo, chini uongozi wa Rais wa Kwanza, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

karatu mjini

Wakati huo alitangaza Azimio la Vijiji vya Ujamaa, katika Kijiji cha Endabashi kilichoko umbali wa kilomita 40 kutoka mjini Karatu.

Mji wa Karatu ulikuwa wilaya ndogo kwa muda wa miaka 50, wakati Mbulu ambayo ipo umbali wa kilomita 76 kutoka Karatu, ndiyo iliyokuwa wilaya kubwa katika zama hizo, ikiwa moja ya wilaya ya Mkoa wa Arusha.

Karatu ilipandishwa hadhi na kuwa mji mdogo mwaka 1979 yakiingizwa maeneo yake kama vile Ayabele na Tloma. Hivi sasa ina tarafa nne za Karatu, Mbulumbulu, Endabashi na Eyasi na kata 14 zenye vijiji 49.

Wilaya hiyo ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu. Awali ngano ilikuwa ikilimwa kwa wingi mahali hapo, lakini sasa wakulima wengi wamejikita kwenye shayiri, mbaazi, mahindi na maharage.

KARATU NA UTALII

Pia ni wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo. Makisio ya mapato
ya jumla ya wilaya kwa mwaka, ni wastani wa Sh. bilioni.

Ni vigumu kutenganisha ukuaji na ustawi wa mji wa Karatu kiuchumi na kimaendeleo, bila kuhusianisha na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Tofauti na wilaya nyingi, Karatu ni mlango wa kituo (hub) cha kuingia NCAA na kwa maana hiyo, wananchi wametumia na wanaendelea kutumia fursa ya uwepo wa utalii kuendeleza mji wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Moses Mabula, anasema, wilaya hiyo ipo kwenye kiini cha utalii na ina sura hiyo kwa muda mrefu.

“Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikifa, hakuna Karatu yenye maendeleo, hilo tunalitambua.

Wananchi wamejengwa kutambua utalii kwa sababu unawanufaisha, hata kwa wale ambao hawajasoma, wanaelewa umuhimu wa utalii katika maisha yao ya kila siku,” anasema.

Mkurugenzi huyo anakiri kuwa mafanikio ya wilaya hiyo, hayawezi kuelezwa bila ya mchango wa NCAA.

Anasema kumekuwapo mahusiano mazuri, kati ya halmashauri yake na NCAA na Mamlaka hiyo imechangia kufanikisha miradi mingi.

Hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule za msingi na sekondari, maji, afya, hifadhi ya mazingira na ulinzi shirikishi wa kuzuia wanyama kuingia maeneo ya
makazi.

Utalii ni moja ya sekta zinazoongoza kukua uchumi wa Karatu na Mkoa wa Arusha kwa ujumla.

Ikiwa na wakazi 250,000, mji wa Karatu una jumla ya hoteli kubwa na kisasa 54 na nyumba 89 safi za kulala wageni.

Ujenzi wa hoteli kubwa zenye hadhi, umeshamiri na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaokwenda kuangalia maeneo ya kihistoria ya binadamu wa kale zaidi duniani.

Aidha, mahali hapo kuna Bonde la Olduvai kunakoshuhdiwa na wanyama wa aina mbalimbali kama vile tembo, simba, twiga na nyumbu, yote hayo yakipatikana ndani ya NCAA.

Mabula anasema wametumia fursa hiyo kujenga hoteli kubwa, za kati na nyumba za kulala wageni ambazo usafi zina usafi wa hali ya juu, kutokana na changamoto ya kupokea wageni kutoka nje ya nchi.

Mmiliki mmoja wa hoteli, anasema ushindani ndiyo umefanya nyumba nyingi za kulala wageni hapa kuwa safi na nzuri.

“Kwa sababu ya ushindani, nyumba nyingi za wageni hapa, usafi wake ni wa hali ya juu kuliko sehemu zingine nchini, hoteli nyingi na nyumba za wageni ni za wazawa,” anasema.

Kujengwa kwa barabara ya lami kutoka Arusha hadi lango la kuingilia NCAA iliyokamilika mwaka 2005, kumeufanya mji huo uchangamke zaidi, kwa kupokea wageni kutoka nje ya nchi.

Ni wageni wanaoenda kuangalia vivutio adimu vinavyopatikana katika hifadhi hiyo, ambayo ni moja ya maajabu saba ya urithi wa dunia. Anatoa mfano wa watu 8,000 wamepata ajira katika sekta ya utalii

MAAJABU YA HIFADHINI

Mambo yanayoingiza hifadhi hiyo katika maajabu ya dunia, ni kama vile tabia ya jamii ya Wamasaai ambao ni wafugaji kuishi maisha ya kirafiki na wanyama ndani ya hifadhi hiyo.

Mengine ni kuwapo kwa ‘Kreta’ kubwa yenye wanyama wa kila aina kuanzia wala nyama kama simba, chui, fisi, mbwa mwitu na wanaokula nyasi kama faru, nyati, paa, swala, twiga, pundamilia na nyumbu, japo kwa uchache.

Upande wa Kaskazini wa wilaya hiyo, kuna msitu wa hifadhi, lakini wakati mji ukikua kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za tofali za udongo, uharibifu mkubwa wa mazao ya misitu ulikuwa ukifanyika.

Ni hali inayoufanya uongozi wa hifadhi kununua mashine ya kutengeneza tofali (Hydraform) kutoka Afrika Kusini yenye thamani ya Sh. milioni 35.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mtendaji wa Hifadhi Mazingira Karatu, Aloyce Songay, imesaidia kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira katika msitu huo, tangu mashine hiyo ilipoanza kutumika miaka minne iliyopita.

Songay anasema mradi huo unajumuisha vijiji vinane vya Alayeme, Tloma,Orjieni, Bashai, Changarawe, Daah (Malera), Rotia na Kimatembo na kwamba kila mtu anayehitaji kununua matofali anatakiwa kwanza kupanda miti 50 kwenye eneo lake.

Anasema watu wengi walikuwa wakifyeka miti kwa ajili ya kuchoma matofali yanayotumika kujenmgea nyumba, lakini kupatikana kwa mashine hiyo inayotengeneza matofali, kumewafanya wawekezaji wengi kupenda kununua matofali hayo kwa ujenzi wa nyumba za kuishi na hoteli.

“Watu walikuwa wakikata miti kwenye Msitu wa Nyanda za Juu Kaskazini kwa ajili ya kuchoma matofali. Angalia mji unavyokua, ni miti mingapi ingekuwa imefyekwa kila siku,” anasema Songay na kuongeza:

“Hali hii ndiyo iliifanya NCAA kubuni mbadala na ikaamua kununua mashine itumike kwa ajili hiyo, ili kulinda mazingira dhidi ya ukataji ovyo wa misitu.”

HOTELI YENYE MIAKA 95

Hoteli ya kwanza kujengwa wilayani hapa ni Gibb’s Farm Tanzania, iliyopo kilomita saba kutoka katikati ya mji na ilijengwa mwaka 1920 ikiwa ndani ya shamba la kahawa linalomilikiwa na raia wa Kijerumani.

Jengo hilo lilibadilishwa na kufanywa kuwa hoteli mwaka 1973, wakati James Gibb na mkewe Margaret walipoamua kuigeuza kuwa nyumba ya kulala wageni, ili kuwawezesha kujiongezea kipato zaidi.

Lengo la msingi la shamba hilo lilikuwa kuzalisha na kuuza kahawa. Ikiwa bado na muonekano wa kizamani, hoteli hiyo ni kivutio kikubwa cha wageni, kutoka nchi za Ulaya na Marekani wanaomiminika kwenda kuona vivutio.

Yapo mategemeo makubwa kwamba, mji wa Karatu ukapanuka na kuwa mkubwa zaidi, kwani ujenzi wa nyumba za kisasa unaendelea kwa kasi sambamba na hoteli.

Ujio wa wageni wengi wanaoenda kuangalia vivutio hifadhini na ongezeko la hoteli za kisasa kwa ajili ya kukidhi haja hiyo, umetoa changamoto kwa uongozi wa wilaya na halmashauri.
Ni jambo linalowahamasisha wananchi kuzalisha kama vile matunda kwa ajili ya kuhudumia soko hilo.

“Ukilima kwa mfano mapapai, utafanya biashara nzuri sana. Papai moja dogo, kwa mfano, hapa linauzwa Sh. 2000, lakini watu hawajishughulishi na kilimo cha matunda kama haya.

“Wenye hoteli wanalazimika kufuata mboga na matunda mjini Arusha,” anasema ofisa mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, kwa
sharti la kutotajwa jina, kwa sababu si msemaji rasmi.

Fursa nyingine itokanayo na kuwapo NCAA, ni kuibuka biashara ya magari ya kusafirisha watalii kwenda Ngorongoro kuangalia vivutio, usafiri wa haraka wa magari kutoka Arusha hadi Karatu na kurudi.

CHUO NA BENKI

Kasi ya ujenzi wa kasi wa hoteli za kitalii Karatu, umeibua changamoto kwa baadhi ya
wawekezaji wazalendo kuona umuhimu wa kuanzisha chuo cha mafunzo ya huduma ya utalii na kimoja tayari kimeshaanzishwa tangu mwaka 2006.

Lengo ni kukidhi mahitaji makubwa ya wataalamu wa kutoa huduma bora katika sekta hiyo wilayani Karatu na kwingineko nchini.

Maendeleo ya haraka ya mji wa Karatu, yametoa kipaumbele kusongezwa kwa huduma za kifedha na sasa zipo benki nne zinazotoa huduma hiyo kwa maelefu ya wakazi na wageni wanaotembelea au kupita mji huo kwa shughuli mbalimbali za kibiashara, utalii, starehe na mapumziko.

MSUKUMO WA MAGEUZI

Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk. Freddy Manongi anaelezea maendeleo yaliyofikiwa kwa mji wa Karatu, kuwa yameletwa kwa namna moja au nyingine na uwepo wa mamlaka hiyo.

“Karatu kama mji umefaidika sana na NCAA, watalii wanaolala ndani ya hifadhi, hawazidi wageni 300. Tunapata wageni zaidi ya 1000 kwa siku, wakati wa msimu wa utalii lakini asilimia 70 ya wageni hao wanalala Karatu.

“Karatu ina hoteli nyingi za kitalii kuliko mji mwingine wo wote nchini, hivyo fedha inayopatikana NCAA inasambaa kwa maendeleo ya watu wengine.

“Ujenzi wa hoteli za kisasa imewafanya watalii wengi wanaokuja hapa, watamani kuendelea kukaa au kurudi kwa mara nyingine kuja kuona vivutio vilivyopo katika Mamlaka yetu,” anasema Dk. Manongi.

Anasema kutokana na watalii hao, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inapata kipato kikubwa kutokana na makusanyo ya kodi na kinachotakiwa ni usimamizi bora zaidi wa makusanyo hayo.

Dk. Manongi anaishauri Halmashauri ya Wilaya Karatu, kuimarisha mifumo yake kukusanya kodi na anaeleza imani yake kwamba, wakijipanga vizuri kaika kukusanya kodi, zitapatikana fedha nyingi.

Anatoa mfano kwamba mamlaka yake imepata ekari 500 huko Karatu, ambako imejenga nyumba za kuishi wafanyakazi wake.

“Asilimia 70 ya wafanyakazi wetu wanaishi Karatu na hii ndiyo faida ya kukua kwa mji. Sasa ukijumlisha na wageni wa ndani na nje wanaokuja
NCAA lakini wanalala Karatu.

“Hao wanaingiza kipato kikubwa kwa
wafanyabishara mbalimbali wa vyakula, vinywaji, hoteli na huduma mbalimbali.

“Wageni hao wote wanahitaji chakula kila siku. Ukiondoa NCAA, mji wa Karatu utakuwa hoi kiuchumi,” anasema.

Kuhusu miundombinu, anasema imeanza kuboreka kutokana na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Makuyuni hadi lango la kuingilia NCAA, barabara
ambayo inayopita katikati ya mji huo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Salustine Hallu, anasema kazi ambayo Mamlaka imefanya ni kuchangia nguvu za wananchi, kwa miradi waiyoibuni wananchi hao, lakini usimamizi na uendeshaji ni suala linalobaki kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Hallu, NCAA imetumia zaidi ya Sh. milioni 500 katika kipindi cha miaka sita, kuanzia mwaka wa fedha 2010/11, hadi mwaka huu katika kufadhili mkradi hiyo.

Ni mtazamo wa kuchangia miradi mbalimbalai ya maendeleo wilayani Karatu, kama vile ujenzi wa darasa katika Shule ya Msingi Makhoromba, Hifadhi ya Mazingira Karatu (Himaka).

Pia kuna kiasi cha Sh. milioni 20.5 kwa ajili ya mradi wake wa kutengeneza matofali ya udongo saruji na upandaji miti,ujenzi wa msingi wa ukumbi wa Ofisi ya Tarafa Eyasi.

Jingine ni Sh. milioni tano zilizotumiwa kujenga nyumba za walimu wa Shule ya Sekondari Endashangwet na Mang’ola na Sh.milioni 10 za Mradi wa Mazingira wa Kambi ya Simba (MESSO) .

Mwenyekiti wa Kamati ya Kituo cha Afya cha Kijiji cha Kambi ya Simba, Augustine Watli, anasema walipata msaada wa fedha wa Sh.milioni 40 za kujengea Wodi ya Wanawake na Watoto, ambayo imekywa msaada mkubwa kwa wajawazito, ambao zamani walitembea kilomita 35 hadi Hospitali Teule ya mjini Karatu.

Hata hivyo, anasema kituo hicho kinakabiliwa na upungufu wa dawa, madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine.

HIFADHI YA MAZINGIRA

Mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa uliobuniwa na kuwezeshwa na NCAA, umenufaisha kaya 37 tangu
Ulipoanzishwa.

Mwenyekiti wa mradi huo kutoka Kijiji cha Ayalabe, Emmanuel Awati, anasema mwaka 2007, NCAA iliwapa ng’ombe wa maziwa 157 ili kuwafanya
Wanakijiji jirani na Msitu wa Nyanda za Juu Kaskazini uliopo ndani ya hifadhi hiyo, wasiingize ng’ombe kuwachunga ndani ya msitu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Salustine Hallu, anasema ufugaji ng’ombe wa kisasa wa maziwa ni rafiki wa mazingira na wameamua kuwashirikisha wakazi hao kuutunza msitu huo.

Mhifadhi huyo ambaye pia ni Mkuu wa NCAA wa Kanda ya Mbulumbulu, Mlungwana Mchomvu anasema wamebeba jukumu la kuwahamasisha wananchi jirani na msitu huo, kutokana na umuhimu wa uhifadhi na huduma ya maji katika mji wa Karatu, ambao asilimia 75 ya maji yake yanatoka katika msitu huo.

Katika kuwashirikisha wananachi kutunza mazingira ya chanzo hicho cha
maji, NCAA imetoa miche ya miti zaidi ya 1,683 kuwagawia bure wananchi wa maeneo jirani na
msitu huo wenye ukubwa wa kilomita za mraba 810.

Mhifadhi huyo anasema, wanatoa elimu shirikishi ya utunzaji mazingira ili wakazi wauone msitu ni mali yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Mji wa Karatu, Karatu (Kaviwasu), Selestine Lolo na Meneja wake, Stephen Siay, wanakiri Mto Endoro na
Mandera ambayo ni vyanzo vikuu vya maji.

“Maji haya yananufaisha zaidi ya nusu ya wakazi katika mji wa Karatu,tunatafuta vyanzo vingine kama vya visima virefu ili kukidhi
mahitaji,” anasema Lolo.

ELIMU

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Welwel ya mjini Karatu, Geofrey Nanyaro, anasema shule hiyo imenufaika na misaada mbalimbali kutoka
NCAA, ikiwa Sh. milioni saba zilizotumika kukamilisha ujenzi wa maabara ya kemia.

Pia anasema NCAA ilitoa Sh. milioni 15 kusaidia ujenzi wa bwalo la chakula na kupatiwa
miche ya miti ya matunda na kivuli, ili
kufanya mazingira ya shule kuwa ya kuvutia.

Shule nyingine ya sekondari iliyonufaika na msaada wa NCAA ni Mlimani Sumawe, iliyojengewa madarasa sita, na kupewa mabati 216 ya kuezekea, vifaa vya maabara na miche ya miti zaidi ya 200 ya miti.

Ofisa Maendeleo Hallu, anasema NCAA, imewawezesha wasichana waliokatishwa masomo kwa sababu ya mimba, kujiendeleza na masomo ya ufundi na maarifa kwa gharama ya zaidi ya Sh.
milioni 20.

MAPATO YA NCAA

Akizungumzia mapato, Mhifadhi Mkuu Dk. Manongi anasema mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 63, ambacho ni kiasi kikubwa kufikiwa tangu ianzishwe miaka 55 iliyopita.

Anasema watalii wengi wanaokuja nchini wanapenda kutembelea mamlaka hiyo na vivutio vikubwa ni wanyama simba, tembo, faru, nyati na chui.

“Hakuna mgeni makini anakuja nchini bila kuja hapa. NCAA ni urithi wa dunia inayotambuliwa na Unesco,” anatamba mkurugenzi huyo.