Simulizi umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa mabinti wadogo Zanzibar

15May 2023
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Simulizi umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa mabinti wadogo Zanzibar

Asha Daudi (sio jina halisi) hajawahi kupata elimu ya hedhi salama tokea avunje ungo na wala hafahamu masuala ya afya ya uzazi huku akiwa na umri wa miaka 17.

Jamila Mahmoud, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA).

Anakumbuka kuwa alivunja ungo na kuanza kupata hedhi kwa mara ya kwanza alikuwa anaangalia luninga kwa jirani yao. Anasimulia kuwa wakati ananyanyuka kuelekea nyumbani, mama mwenye nyumba ambae ni jirani alimuita na kumwambia aende chooni ambako aligundua kuwa nguo yake ina damu. 

Baada ya kufika nyumbani anasema: “Mama aliniambia mwanangu umekuwa mkubwa kauli iliyonishtua kwa sababu niliona ni kitu kigeni kwangu wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 12. Hata hivyo, nilifundishwa jinsi ya kujihifadhi,”anasema.

Msichana huyo anasimulia kuwa alivyofikisha miaka 15 aliingia kwenye mahusiano kwa kuwa hakuwa makini alipata ujauzito ujauzito.

Anasema kuwa ujauzito wake ulibainika baada ya wazazi wake kupata wasiwasi baada ya kuona mabadiliko yake, ikiwemo kutapika mara kwa mara, kutoweza kula huku akilala hovyo.

ASHA HAYUKO PEKE YAKE

Kukosa elimu ya hedhi salama na elimu ya afya uzazi hupelekea wasichana kupata mimba zisizotarajiwa, ambapo takwimu kutoka Wizara ya afya Zanzibar zinaonesha kuwa kwa miaka mitatu 2020/ 2022 wasichana 9,116 walipata ujauzito.

Takwimu hizo ni kwa wasichana waliofika hospitali kupata huduma mbalimbali na kugundulikana kuwa wanaujauzito ambapo kwa mwaka 2020 walikuwa 3061, mwaka 2021 walikuwa 3180 na mwaka 2022 walikuwa 2875.

Ukosefu wa elimu ya hedhi salama unaifanya jamii kuwa na aibu kuzungumzia hedhi salama kwa wasichana. Iwapo itatolewa kikamilifu, elimu hiyo itamsaidia msichana kujua mzungo wake wa hedhi na siku hatari anazoweza kupata ujauzito iwapo atajihusisha na jimii (ngono).

Elimu hiyo ya hedhi salama inatakiwa iende sambamba na elimu ya afya ya uzazi ambapo ni muhimu kutolewa kwa wasichana na wavulana.

Hata hivyo hedhi kwa wanawake ni jambo lisilozungumzwa hadharani katika jamii nyingi visiwani Zanzibar kutokana na imani za kidini na kitamaduni.

UTAMADUNI NI PINGAMIZI 

Kutokana na kukosa elimu hiyo baadhi ya wasichana visiwani Zanzibar hasa maeneo ya vijijini huficha kutoa taarifa pale wanapokua na mabadiliko katika miili yao au kutokwa na hedhi kwa mara ya kwanza (kubata ukubwa).

Kwa kuwa wanaliona ni jambo la kawaida, hata wanaotoa taarifa baada ya kuvunja ungo, baadhi ya wazazi hawana utamaduni wa kukaa na watoto wao kwa ajili ya kuwapa elimu inayo husiana na mabadiliko ya kimwili.

Jamila Mahmoud, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), anasema hedhi salama kwa wasichana ni muhimu katika jamii kwa sababu walezi wingi wamekua na usiri na kuona ni jambo la aibu. “Tumekua na itikadi fulani kuwa kumfundisha mtoto suala la hedhi salama na afya ya uzazi ni kuwafundisha mambo mabaya kwa hiyo wazazi tumekua kimya kisasi ambacho mtoto anaweza kupata hedhi bila ya kujua nini afanye,”anasema Jamila.

Aidha anasema baadhi ya watoto wanapopata hedhi wanaogopa kutoa taarifa kwa sababu ni jambo geni kwake na mzazi anakuja kushtuka mtoto ameshapata ujauzito. Anasema wazazi na walezi wakati umefika kuwa wawazi kwa watoto wao kwa sababu maisha yamebadilika watoto wana marafiki wingi, hivyo baadhi ya watu huitumia nafasi hiyo kumuharibia utu wake.

“Baba hua hana nafasi mtoto wake anapovunja ungo kukaa na kuzungumza nae kuhusu hedhi salama na baba anazuka pale mtoto anapopata ujauzito kwa kumlaumu mama”anasema.

Shufaa Hemed mwanaharakati wa haki za wanawake, anasema kukosekana kwa elimu ya hedhi salama kunapelekea mimba za umri mdogo na wasichana kushinndwa kujikinga.

Anasema hata vitendo vya udhalilishaji vinaongezeka visiwani Zanzibar kutokana na watoto kukosa elimu ya kujieleza na kujitambua.

“Bado baadhi ya wanajamii hasa vijijini ni wagumu hata kuwaruhusu watoto wao kuwapatia elimu hii maana mimi binafsi hupita vijijini kutoa elimu ya hedhi salama na afya ya uzazi lakini wanadhani kwamba tunawafundisha mambo maovu”anasema.

Riziki Ali ambaye ni mzazi wa watoto watatu mkaazi wa kijiji cha Fukuchani, anasema wakati wa ujana wake elimu ya hedhi salama ikitolewa shuleni na madrasa lakini hivi sasa elimu hiyo inakosekana.

“Elimu hii hivi sasa inakosekana sio ,shule, madrasa hata katika jamii wakati watoto wanahitaji kupewa elimu hii na kujua mabadiliko yao ya mwili ili kujikinga na vishawishi mblimbali ambavyo vitapelekea kupata ujauzito”anasema.

Anasema elimu hiyo inapaswa kutolewa kwa watoto wote wa kike na wakiume ili kila mmoja kuwa mlinzi kwa mtoto wa mwezake katika kumkinga na vitendo vya udhalilishaji na kuepuka na mimba za umri mdogo na kuwa na familia bora.

DINI NA HEDHI SALAMA 

Abdulrahman Omar Bakari, Kiongozi wa dini ambae pia ni kadhi wa mahakama ya kadhi Mwera Unguja, anasema uislamu unazingatia makuzi ya mtoto kujua yupo katika mazingira gani hivyo ni jukumu la mzazi kumtayarisha kiakili kuwa anakaribia kubaleghe.

“Ni jukumu la mzazi au mlezi kumfundisha mtoto anaekaribia kubaleghe kuwa kuna dalili hizi na hizi zitakujia hivyo mtoto dalili hizo anapozipata hua hashangai na anapovunja ungo hutoa taarifa”anasema.

Bakari anasema taaluma hiyo isiishie baada ya mtoto kuvunja uongo bali iendelee kutolewa ambapo alitolea mfano nchi ya Maleshia elimu hiyo hutolewa kwa watoto ili kuwalinda na mimba zisizotarajiwa na vitendo vya ubakaji.

Hata hivyo anasema watunga sera katika jamii lazima kuangalia namna ya kupanga silbasi za masomo ya watoto shuleni ambayo yatawasadia katika makuzi yao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, linatoa usaidizi wa kuokoa maisha kwa wasichana na vijana, wanawafikia kutoa elimu ya hedhi salama na afya ya uzazi kwa kushirikiana na wizara ya afya, wizara ya elimu na wizara ya jinsia Zanzibar.

Amina Kheria, Afisa wa shirika hilo anaeshughulikia afya ya uzazi na vijana Zanzibar, anasema elimu hiyo huitoa kwa wanafunzi shuleni na wanatumia mbinu mbalimbali ikiwemo kupima uwelewa kwa vijana kwa sababu bado uwelewa wao upo chini.

Anasema wanatumia mbinu hizo ikiwemo mabonaza ili kuwafikia vijana kupata taarifa sahihi ambapo zitawasadia kujiepusha na mambo mbalimbali ikiwemo mimba za umri mdogo na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Aidha anasema taarifa ni njia moja wapo ya kujikinga na kufanya mamauzi sahihi tofauti na ukiwa huna taarifa.

Anasema kwa kushirikiana na wizara ya afya wanavituo rafiki kwa kila wilaya kwa ajili ya vijana ikiwemo wasichana kupata uelewa wa masuala ya hedhi salama na afya ya uzazi ili kupata huduma.

Amina anasema masharikiano hayo ya kutoa elimu yamesaidia kupunguza idadi ya mimba za utotoni,na takwimu kutoka idara ya takwimu kwa muda wa miaka mitano iliyopita inaonesha kuwa zimeshuka kwa asilimia 4 kutoka asilimia 8 mwaka 2015.

Afisa huyo anawashauri wazazi kuwa karibu na watoto wao hasa wale wanaofikia umri wa kubaleghe na kuwa wawazi katika kuwaelezea masuala ya hedhi salama na afya ya uzazi ili kujiepusha na vitendo vya ngono ambavyo vinaathari nyingi.

Sihaba Saadati, mkurugenzi, kinga na utafiti wa Tume ya Ukimwi Zanzibar anasema, umuhimu wa elimu ya hedhi salama kwa wasichana inawasadia kutunza sehemu zao za siri, kujitambua, kujihifadhi lakini pia kujikinga kutopata ujauzito na maradhi ya kujamiana ikiwemo maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

“Yapo maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa wasichana na watoto wanapoingia katika umri wa baleghe kama hawajapata elimu nzuri wanaweza kujikuta wanaingia katika vitendo vya ngono kutokana na vishawishi mbalimbali, unapofanya vitendo vya ngono unaweza kupata mimba katika umri mdogo, mamaukizi ya VVU na maradhi mingine ya kujamiana”alisema.

Aidha anasema ni vyema mtoto akapata elimu mapema kwa sababu kwa mujibu wa utafiti waliofanya tume ya ukimwi, mtoto anaweza kufanya ngono kuazia umri wa miaka 10, ili kuwasaidia wasichana kujilinda na mimba na virusi vya

UKIMWI

Serikali kuchukua hatua Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui, anasema kukosekana kwa elimu ya hedhi salama na afya ya uzazi pia kunapelekea watoto kupata maradhi na kufanyiwa udhalilishaji.

Anasema mikakati ya wizara ni kujenga vituo rafiki katika hospitali ili wasichana kwenda kueleza shida zao kuhusu hedhi salama na afya ya uzazi na kusaidiwa.

Anasema wizara hiyo kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa wanatoa elimu ya hedhi salama na afya ya uzazi kwa wanafunzi mashuleni ambapo elimu hiyo ni muhimu aze kutolewa kwa watoto kuazia miaka 10.

“Elimu hii itolewe kwa watoto wote wa kike na kiume mfano wezetu nchini Ethopia wanatoa elimu hii kwa watoto wa kike na kiume mashule”anasema.

Waziri wa ustawi wa jamii, jinsia, wazee na watoto Riziki Pembe, anasema jamii haina utamaduni wa kuwaeleza watoto kuhusu hedhi salama na ndio maana baadhi ya watoto anafikia hatua ya kupata hedhi hafahamu chochote na kuona ni kama jambo la ajabu.

“Ingawa saivi masuala ya utandawazi yanasaidia kidogo lakini sio kwa watoto wote kwa hili wizara yetu tunashirikiana na wizara ya elimu kutoa elimu kwa watoto wa kike kuhusu hedhi salama na elimu ya kujitambua”anasema.

Anasema msichana anaepata hedhi bila ya kuwa na vifaa salama huwa na hofu na hupelekea udhalilishaji kwa sababu anaweza kupata mwanaume akamwambia atampa vifaa hivyo na kumtumia vibaya.

“Pia kuna baadhi ya wanaume waharibifu huwatumia wasichana na kuwataka watumie liwati ili kulinda bikira zao na binti kwa kutojua kwake na kutojielewa anakubali hilo”anasema.