UVIKO-19 janga lilioacha makovu kwa Wajasiramali Zanzibar

15May 2023
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
UVIKO-19 janga lilioacha makovu kwa Wajasiramali Zanzibar

WAKATI Dunia ikijikwamua kutoka kwenye janga la UVIKO-19 ni lazima kuhakikisha kwamba matarajio na haki za watu wenye ulemavu zinajumuishwa.

Kutokana na janga hilo, uchumi wa Dunia uliteterereka na Zanzibar ikiwa ni sehemu ambayo ilikumbwa na hali hiyo ambayo ilipelekea baadhi ya wajasiriamali wakiwemo watu wenye ulemavu kupoteza biashara zao.

Katika kupunguza makali ya ugonjwa huo ambao ulipelekea shughuli nyingi za kiuchumi kudorora serikali ilipata mkopo wa fedha shilingi bilioni 230 kutokashirika la fedha la kimataifa IMF.

Katika fedha hizo wizara inayohusika na masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ilitengewa fedha ya Shilingi bilioni 31 kwa ajili ya wajasiriamali visiwani Zanzibar.

Muamko ni mdogo wa kuitumia fursa hiyo ya mikopo kwa watu wenye ulemavu ikilinganishwa na wasio na ulemavu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo vikwazo vya masharti ya mkopo huo.

Kutokana na vikwazo, idadi ya waliopata mkopo ni ndogo na kati ya vikundi 90 vya wajasiriamali wenye ulemavu Zanzibar, vilivyosajiliwa ni vikundi 12 vilivyopata mkopo huo unaotokana na fedha za UVIKO-19.

Fatma Mgwali Khamis, Katibu wa kikundi cha watu wenye ulemavu Mkoa wa Kaskani Unguja (safiniayako) mwenyeulemavu wa uoni, anasema upatikanaji wa mikopo hiyo imekuwa na changamoto kubwa hasa kwa watu wenye ulemavu.

Anasema kikundi chao chenye wanachama 20 ambao wanajishughulisha na kazi za mikono za ufumaji, ni mwaka pili sasa tokea kuomba mkopo huo hawajaingiziwa fedha.

“Tumeshakamilisha taratibu zote za kuomba mkopo huu mwaka wa pili hatujaingiziwa fedha na shuguhli zetu za uzalishaji zimesita tumejaribu kufuatilia benki lakini wanasema hakuna fomu yetu ya maombi iliyopelekwa,”anasema.

Anasema shughuli hizo zimesita kutokana na kutokua na fedha ya kununua malighafi ambayo hutumia kwa ajili ya shuguhli zao za ufumaji.

Anasema malighafi wanazotumia ni kamba za usumba kwa ajili ya ufumaji wa mazulia na mikoba ambapo soko lao kuu ni katika sekta ya utalii.

Anasema fedha hizo walitarajia kuongeza mtaji katika kazi yao hiyo ili kuzalisha bidhaa nyingi na kuwa na soko la uhakika.

“Hivi sasa tunapata tenda ya kuuza bidhaa zetu lakini hatuna bidhaa kwa sababu ya kukosa zana na nyenzo za kufanyia kazi kama tungepata hii fursa ya kupata mkopo tungeendeleza bidhaa zetu” anasema Fatma.

Fatma ambae pia ni Diwani wa Viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja anaiomba serikali fedha hizo kupelekwa katika baraza ya miji ili kusaidia katika wilaya kuliko utaratibu uliowekwa.

Fatma anaungwa mkono na Njuma Ali kutoka kikundi cha watu wenyeulemavu kiitwacho safinia ambacho kinajishughulisha na kazi ya ufinyanzi.

Njuma, anasema siku zinayoyoma, fedha za mkopo hawajapata licha ya kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ikiwemo kuwa na akaunti namba ya kikundi na kujaza fomu ya mkopo na wamekamilisha taratibu hizo na umepita muda wa mwaka mmoja sasa hakuna fedha waliyopata.

Anasema walishajihika kuomba mkopo huo baada ya Rais Dk Mwinyi kusisitiza kuitumia fursa ili kujikwamua kiuchumi kulikoathiriwa na janga la maradhi ya UVIKO-19.

Mjasiriamali Nasra Hamad mwenye ulemavu wa viungo anayefanya biashara ya mama lishe, anasema kuna usumbufu mkubwa wa kuomba mkopo na kupelekea kukata tamaa mapema kuomba mkopo kutokana na vikwazo.

Anasema serikali ilitakiwa kuwakutanisha watu wenyeulemavu na kuwapa elimu jinsi ya kuomba mkopo huo ili kuondokana na usumbufu wanaokumbana nao.

“Kila siku tumekua tukirejeshwa kuwa maombi yetu hayajakamilika mara nenda huku mara kule hali ambayo imenikatisha tamaa”anasema.

Anasema watu wenyeulemavu wanahitaji mikopo nafuu kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini lakini pia itasiadia kuondosha wimbi la ombaomba mitaani ambapo watu wenyeulemavu ndio wanaongoza katika wimbi hilo.

WALIOPATA MKOPO WAJUTIA

Katibu wa kikundi cha Yajayo Yanafurahisha huko Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Muhammed Abdallah, anasema nia ya serikali ya kutoa mkopo huo ni nzuri lakini haujawanufaisha watu wenyeulemavu.

Anasema kikundi chao waliomba mkopo wa milioni 15 na kupatiwa million nane ambapo waliingiziwa fedha mwezi wa Machi mwaka jana.

Alikiri kuwepo kwa changamoto katika kuomba mkopo huo hadi kuupata ikiwemo masharti makubwa, harakati nyingi za kuanza usajili hadi kupata mkopo huo.

“Kuna vipengele vingi tokea usajili nenda rudi ni nyingi lakini mkataba wao wa kurejesha malipo unatisha na sio rafiki kwa watuwenyeulemavu kama sisi tunajishughulisha na kazi ya ushoni tunatakiwa tukamilishe marejesho ya fedha tulizokopa ndani ya mwaka mmoja na nusu”anasema.

Aidha anasema muda huo ni mdogo hasa ikizingatiwa kuwa mauzo wanayouza si yakiwango kikubwa na lazima wanatakiwa kurejesha fedha hizo za mkopo benki kila mwezi shilingi laki nne na elfu arubaini.

Anaongeza kwa kusema”Fedha tuliyopatiwa yote tumenunulia vifaa vya kazi pamoja na mali ghafi….huu mkopo kwa kweli umetuweka roho juu maana hatuna faida tunayoipata, fedha tunazouza bidhaa inatulazimu tuchangishane wanachama tuijalize ili turejeshe mkopo benki kwa sababu mauzo yetu hayafiki laki nne kwa mwezi”.

Hata hivyo anasema hawatoendelea tena kukopa mkopo huo, baada ya kukamilisha deni wanalodaiwa kwa sababu wanapitia katika wakati mgumu.

Katibu mtendaji wa baraza la watu wenyeulemavu Zanzibar Ussi Khamis Debe, anasema mikopo ya fedha za UVIKO-19 hasa kwa watu wenyeulemavu ni changamoto kubwa licha ya Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi kutoa maagizo kuwa watu wenyeulemavu wapatiwe mikopo,kupitia fedha hizo.

“Sisi kama baraza tumechukua jitihada za kutengeneza vikundi vya watu wenyeulemavu maana vilikuwa vichache na hadi sasa naongea na wewe kuna vikundi 90 Unguja na Pemba, tulivyovisajili ili kutimiza masharti na tukaviunganisha na wakala wa uwezeshaji, changamoto ipo katika utoaji wamikopo kuna nenda, rudi nyingi”anasema.

Aidha anasema katika vikundi 90 vya watuwenyeulemavu vilivyoomba mkopo huo vikundi 12 ndivyo vilivyopata na baadhi ya vikundi vyengine vinakataa kukopa kwa kuogopa kufilisiwa au kushtakiwa endapo watashindwa kulipa.

Anasema juhudi zinahitajika, kubadilisha mitazamo hasi ya vikundi hivyo ili kuitumia fursa ya kupata mikopo itakayowasaidia kujiendesha kiuchumi na kuondokana na tabia ya ombaomba.

Asha aboud mwanaharakati wa kutetea haki za watu wenyeulemavu, anasema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi zao za kupata maendeleo.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo ni ukosefu wa kupata mitaji ya fedha kwa ajili ya kuendesha biashara kwa sababu wengi wao hawakopesheki kutokana na uwezo mdogo walionao.

Anasema zipo taasisi za fedha ambazo zinatoa fedha za mikopo kwa makundi mbalimbali kuendesha shughuli za ujasiriamali lakini kwa makundi ya watu wenye ulemavu hadi sasa hayajafikiwa vizuri.

Mratibu wa jumuiya ya watu wenyeulemavu wasiona Zanzibar, Adil Muhammed anasema watu wenye ulemavu wameitumia fursa hiyo ya mikopo lakini wingi wao hawakuzipata licha ya kufuata taratibu na kukata tama.

Adil alishauri zinapotokea fursa kama hizo kuwepo na ukondowishaji kwa kila nyanja na kujumuisha watu wenyeulemavu.

“Sekta nyingi zinapuuza katika kuwashirikisha watu wenyeulemavu hali ambayo hupelekea kuwepo kwa athati kubwa kwao lazima tushirikishwe katika utoaji wa ruzuku”anasema Adil ambae anaulemavu wa uoni.

Aidha anasema watu wenyeulemavu hawana vipato wanatumia muda mkubwa na gharama kubwa kuliko watu wasio na ulemavu.

“Unapofatilia jambo lolote kwetu sisi tusiona huwa na changamoto kubwa sababu inatulazimu tuongozane na mtu ambae atatuongoza kwa kila jambo na mtu huyo inabidi umugharamie nauli sasa unapofuatilia fursa kama hizi ukaambiwa njo kesho njoo kesho inatuvunja moyo”anasema.

Hata hivyo anasema jitihada za ziada zinahitajika kuondoa mitazamo hasi kwa jamii kuhusu watuwenyeulemavu kuwa hawakopesheki na hawatoweza kulipa jambo ambalo linaathiri maendeleo yao.

Kassim Haji Mrisho kaimu mkurugenzi wa idara ya mitaji kutoka wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, anasema wajasiriamali na watu mbalimbali wamehamasika kuomba mikopo ya fedha za UVIKO-19 lakini kundi la watuwenye ulemavu ni wachache.

Anasema awamu ya kwanza wametoa mkopo wa fedha wa shilingi bilioni 15 kwa vikundi mbalimbali vya wajasiria mali ikiwemo vya watu wenye ulemavu.

“Katika fedha tulizozitoa kwa awamu ya kwanza vimo pia vikundi vya watu wenyeulemavu ingawa sio vingi ikilinganishwa na wasio na ulemavu…… hii mikopo ni kwa ajili ya watu wote niwaombe watuwenye ulemavu kuichangamkia fursa hii”anasema.

Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa kwanza wa rais, Harusi Suleiman anasema serikali, imejipanga kuhakikisha sheria ya watu wenye ulemavu inatekelezwa kikamilifu ambapo lengo ni kuona haki za makundi hayo zinapatikana ikiwemo fursa za kiuchumi.

Waziri huyo anasema, serikali imekuja na sheria ya watu wenyeulemavu ya mwaka 2022 ambayo lengo lake kwenda na wakati wa mabadiliko yaliopo sasa ya dunia ikiwemo mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo inalinda haki za makundi hayo.

Anasema uwepo wa sheria mpya ya watu wenye ulemavu itahakikisha makundi hayo yanapata fursa na haki sawa kwa mujibu wa sheria.

Aidha anasema ukosefu wa mitaji kwa watu wenye ulemavu, kumepelekea kuwepo kwa kundi kubwa la ombaomba ambapo baadhi ya watu huwatumia watu wenye ulemavu kama kitega uchumi chao.

“Jambo hili halipendezi hata kidogo unamtumia mtu mwenyeulemavu kinyume na sheria unamtembeza mji mzima kuomba na fedha inayopatikana inawanufaisha watu wingine”anasema.

Waziri huyo anasema serikali inafahamu kuwepo kwa matukio ya aina hiyo ambapo tayari baadhi ya watu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kuwatumiya watu wenye ulemavu.

Anasema watu hao waliokamatwa wamekutwa, wakiwahifadhi watu wenyeulemavu katika nyumba moja visiwani Zanzibar na huwasambaza katika maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar kwa ajili ya kuomba ili kupata fedha.

Makamu wa pili wa rais Hemed Suleiman Abdullah, anasema watu wenyeulemavu wanaweza kufanikiwa kimaisha kama watu wingine kwa kuzitumia fursa zinazotolewa na Serikali na mashirika ya umma ambazo zinaweza kubadilisha maisha kuwa bora.

Anasema Serikali ya Zanzibar inalifahamu ukubwa wa tatizo la watu wenyeulemavu na ndiyo maana imejipanga kulipatia ufumbuzi kwa njia mbalimbali ikiwemo kuzitambuwa haki na fursa kwa mujibu wa sheria.