Yalikuwa ni mabao matatu yaliyofungwa na wachezaji wawili wa Kitanzania, Mudathir Yahaya akipachika mawili, moja Farid Mussa, huku lingine likifungwa na mchezaji wa kimataifa kutoka Zambia, Kennedy Musonda.
Mwamuzi Omari Mdoe, alipopuliza filimbi ya kuashiria mechi hiyo kumalizika na Yanga kuibuka na ushindi huo, iliashiria kuwa pointi tatu ambazo ilizipata zimeifanya kuwa jumla ya pointi 74, ambazo haziwezi kufikiwa na timu zote 15 zilizobaki za Ligi Kuu.
Ilikuwa hoi hoi nderemo na vifijo kwa wachezaji, wanachama, mashabiki na viongozi waliohudhuria mechi hiyo ambao wengi walikwenda na familia zao, wakiongozwa na Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi Said, ambaye aliungana na wachezaji na viongozi wenzake kushangilia ubingwa huo.
Yanga imetwaa ubingwa huo ikiwa imebakisha mechi mbili mkononi dhidi ya Mbeya City na Prisons.
Kwenye makala haya, tunakuletea takwimu za rekodi mbalimbali za Yanga kuhusu ubingwa wa ligi, pamoja na historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara, haya sasa...
1. Inaongoza kwa kutwaa mara 29
Yanga imetwaa ubingwa mara 29 sasa kwenye vipindi na misimu tofauti na inaendelea kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi tangu kuanza kwa mfumo wa ligi Tanzania mwaka 1965.
Yanga ilianza kuutwaa ubingwa wa Tanzania mwaka 1968, ikishindwa kulipata lilipoanzishwa mwaka 1965 lilipochukuliwa na Simba wakati huo ikiitwa Sunderland mara mbili, mwaka 1965 na 1966, klabya mwaka 1967 kuchukuliwa na Cosmopolitan.
Wakati Yanga ikiwa inaongoza kwa kutwaa ubingwa mara nyingi, Simba inashika nafasi ya pili kwa kutwaa mara 22, Mtibwa Sugar imetwaa mara mbili mwaka 1999 na 2000.
2. Mara nne kutwaa mfululizo ('back to back')
Inakuwa ni mara ya nne kwa Yanga kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo. Ingawa imeshawahi kutwaa mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1968 hadi 1972, lakini hapa tunazungumzia mara mbili mfululizo tu.
Ilianza kufanya hivyo mwaka 1996 na 1997, ikarudia tena 2005 na 2006, ikatwaa tena msimu wa 2007/08 na 2008/09, kabla ya kurudia ilichokifanya mara tatu, msimu uliopita na huu.
3. Inaziongoza timu za Dar
Yanga imeendeleza rekodi ya timu za Dar es Salaam kutwaa ubingwa mara nyingi zaidi kuliko za mikoa mingine.
Kwa jumla timu za Dar es Salaam zimechukua ubingwa mara 54, Yanga ikitwaa mara 29, Simba mara 22, Pan African na Cosmopolitan na Azam FC ambazo zote zimechukua mara moja, dhidi ya mara tano ya timu za mikoani ambazo ni Mtibwa Sugar iliyotwaa mara mbili 1999 na 2000, Mseto ya Morogoro iliyotwaa mwaka 1975, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union ikilichukuwa mwaka 1988.
4. Miaka 58, timu tisa
Ingawa timu ni nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara tangu lianzishwe mwaka 1965, lakini mpaka sasa ni timu tisa tu ambazo zimetwaa ubingwa huo.
Ni miaka 58 imepita, lakini ambazo zimeshaonja raha ya kulibeba ni Yanga, Simba, Mseto, Cosmopolitan, Pan African, Tukuyu Stars, Coastal Union, Azam, na Mtibwa Sugar tu.
5. Ligi Kuu Bara ilivyoanzishwa
Lilikuwa ni wazo la Kocha wa Timu ya Taifa ya wakati huo raia wa Yugoslavia, Milan Celebic, mnamo mwaka 1964 ikiwa ni njia ya kupata wachezaji wa timu ya taifa.
Alitaka ianzishwe ligi ya klabu, badala ya mashindano ya Sunlight Cup (baadaye Taifa Cup) yaliyokuwa yanazishirikisha timu za majimbo baadaye mikoa.
Ingawa timu za Simba wakati huo ikiitwa Sunderland na Yanga zilikuwapo, lakini zilikuwa zikicheza na timu za mikoa ya Pwani tu ambayo sasa ni Dar es Salaam.
Mwaka 1965, Chama cha Mpira wa Miguu (FAT), kikaanzisha Ligi ya Taifa ikiwa inashirikisha timu nane na hapa ndio ukawa mwanzo Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ilikuwa ikipitia hatua mbalimbali za mifumo, ikianza kwa mtindo wa mtoano mwanzo hadi mwisho, baadaye makundi, mpaka aina hii ya ligi tuliyonayo leo.










