Sikukuu bila nguo mpya hapatoshi enzi hizo

05Nov 2022
Adam Fungamwango
Dar es salaam
Nipashe
Sikukuu bila nguo mpya hapatoshi enzi hizo
  • Watoto wanaulizana, waliowahi kununuliwa ni kama siku haziendi

"DOLI Doli, nimenunuliwa nguo ya sikukuu na viatu." Ni wimbo ambao utakuwa unaimbwa kwa mbwembwe na mmoja kati ya watoto ambaye wazazi wake wamemnunulia nguo ya sikukuu.

 

Anaweza kuangaliwa jicho baya au kununiwa na watoto wenzake ambao wao mpaka muda huo kwao 'bila bila' yaani hata wazo la kununuliwa bado.

Angalau kwa mbali anaweza kusapotiwa na wale ambao wazazi wake wamewaambia wasubiri mwisho wa mwezi huu.

"Na sisi baba kasema atatununulia. Tena kasema na viatu vizuri kushinda hata vya kwako." Mmoja atampa jibu hilo.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha ya zamani watoto kinapokuja kipindi kama hiki kuelekea kwenye sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Ni kipindi ambacho wazazi wa zamani walikuwa kwenye pilikapilika ya aina yake kutafuta pesa kwa ajili ya kuwanunulia watoto nguo za sikukuu, pamoja na kula chakula kizuri siku hiyo.

Kuna wakati mzazi hata kama hana pesa, lakini atalazimika kujitutumua kwa ajili tu ya kutowafanya watoto wake wajisikie vibaya siku hiyo.

Tatizo kwa watoto ni kwamba watanunuliwa lini, ndilo lililokuwa linawasumbua. Wakiona wenzao wamenunuliwa wao bado basi roho juu.

Kwa wakati huo mama ndiyo atasumbuliwa zaidi na watoto, akiulizwa maswali ya kwa nini mpaka siku hiyo bado tu hawajanunuliwa.

Nasema wakati huo kinamama walikuwa wakisumbuliwa zaidi kwa sababu, kwenye miaka ya 1990 kurudi nyuma kulikuwa aina tofauti ya akinababa na wa sasa. Wa siku hizo ni wanademokrasia.

Miaka hiyo hakuna mtoto yoyote hata akili yake tu imtume asimame mbele ya baba yake amuulize ni kwa nini mpaka wakati huo hawajanunuliwa nguo za sikukuu. Kitakachompata kwenyewe atasimulia.

Sasa ukute kipindi kama hiki mtoto amekuwa wa 30 shuleni au wa pili kutoka mwisho, baba anagoma kabisa kununua nguo. Anasema hawezi kumnunulia nguo mtoto ambaye 'hana akili' darasani.

Kwa bahati mbaya sana, nimesema kina baba wa zamani walikuwa wakisema wamesema. Ni kweli hatomnunulia mtoto ambaye hakufanya vema darasani. Atanunua tu kwa yule ambaye amefanya vizuri.

Hapo sasa jukumu la kununua nguo kwa waliobaki linabaki kwa mama. Ni kinamama tu ndiyo waliokuwa hawakubali kuona mtoto au baadhi ya watoto wake hawajapata nguo za sikukuu kwa sababu tu hawajafanya vema shuleni.

Atabania pesa ya kula anayoachiwa, atakopa au kuazima, ili mradi tu arekebishe hilo tatizo. Halafu akishanunua ndiyo mtoto atakoromewa kuwa asiwe mvivu wa shule, awaige wenzake, na atatishiwa kuwa mwakani au sikukuu ijayo hatununuliwa tena kama akiendelea kuwa 'kichwa maji'.

Twende kwa wale ambao watanunuliwa mapema nguo za sikukuu. Hao ni wale wanaonunuliwa kama mwezi huu wa Novemba yaani nguo tayari zipo sandukuni.

Pamoja na kwamba wana uhakika, lakini hawa nao utawaonea huruma. Yaani safari za kwenda sandukuni haziishi. Atafungua ataiangalia mara tatu tatu, atafunga. Atarudi tena ataviangalia viatu. Wakati mwingine atavijaribu. Na nguo atavaa na kujiangalia alivyopendeza. Anatamani sikukuu iwe hata kesho, siku wanaona haziendi. Anataka siku hiyo ifike upesi ili avae apendeze akawakosoe wenzake.

Hali hii wakati mwingine inasababisha ugomvi na mama. Yeye anakuwa ameshazipiga pasi na kuzikunja vizuri, ameshaweka na kidonge cha dawa ya mende, halafu tena kuna mtu anakwenda kufunguafungua.

Ingawa hili lipo kwa miaka ya sasa, lakini siyo kama ilivyokuwa enzi zile. Ni kwa sababu miaka ya leo, mtoto anaweza kuvaa nguo za zamani na mwingine akavaa nguo mpya wala mtu asijue zipi mpya na zipi za zamani.

Sababu kubwa ya kipindi kile watoto kuhitaji zaidi nguo za sikukuu kwa sababu kulikuwa na uhaba wa nguo. Pia hawakuruhusiwa kuvaa nguo zinazoonyesha  kuwa ni bora. Hizo ziliwekwa kwa ajili ya safari, kanisani, au sherehe za kijamii. Kuna nguo fulani hivi ambazo kinamama walikuwa wamezirasimisha kama ni za watoto wao za kushindia nyumbani tu. Hata hizo za sikukuu ikishamalizika, hazikuruhusiwa tena kuvaliwa mpaka siku maalum kama hizo nilizozitaja mwanzo.

Wazazi au kinamama wa sasa wanawapiga watoto zao 'pamba' za nguvu hata wakiwa tu nyumbani. Halafu watoto wa kisasa si watundu sana kama wa zamani. Zamani unaweza baadaye kumkuta yupo kifua wazi na shati keshapoteza huko alikokwenda kucheza mpira wa wenzake.

Kuwepo kwa nguo nyingi zenye ubora unaofanana umefanya kusiwepo sana mahitaji ya lazima ya watoto kununuliwa nguo za sikukuu. Mtoto anaweza kuwa alinunuliwa tu nguo mwezi uliopita na hiyo hiyo akaitumia kwenye sikukuu ikawa haitofautiani na ya wenzake walionunuliwa kwa ajili hiyo.

Nitaweka meseji chache za wadau waliochangia hili kwenye mtandao wa kijamii.

"Nakumbuka nilinunuliwa suruali nisiyoipenda nililia toka nyumbani hadi kanisani, tuliporudi ikabidi wazazi waende tena dukani kunichukulia suruali ya  mchele mchele ndiyo nikanyamaza," alikumbuka mdau mmoja kilichomtokea miaka mingi nyuma akiwa mtoto.

"Hili suala limenikumbusha enzi za utotoni. Kweli ilikuwa raha sana. Mkiwa mnacheza mnaulizana vipi nyie mmeshanunuliwa nguo za sikukuu? Watoto ambao wazazi wao wanachelewa kununua huwa wanakosa raha kabisa. Siku hizi sipendi kabisa kuzoesha watoto wangu hiyo tabia," aliandika mwingine.

"Mkuu kwa kweli nakumbuka wakati tukiwa wadogo kwetu kijiji kuna nguo ilikuwa huwezi kuvaa mpaka usafiri. Sisi tulikuwa na nguo za kuvaa tukienda Dar es Salaam tu. Kwa sasa kila nikikumbuka natabasamu tu." Mdau mwingine akachangia.