Mtihani wananchi waliosababisha maji ya bahari kuyavamia makazi -2

06Nov 2022
Mary Geofrey
Mtwara
Nipashe Jumapili
Mtihani wananchi waliosababisha maji ya bahari kuyavamia makazi -2
  • Serikali yaanika mikakati kukabili athari

Ofisa Mazingira Halmashauri ya Minispaa ya Mtwara Mikindani, Tumaini Mosha anabainisha wamejiwekea utaratibu wa kuotesha miti 16,000 kila mwaka katika maeneo mbalimbali wakati wa msimu wa mvua ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mtaa wa Kisungule A, Mikindani mkoani Mtwara, Moza Ahma, akionyesha namna wanavyotumia taka kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi yao. PICHA: MARY GEOFREY

Kuhusu tatizo la uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo, ofisa huyo alisema unafanyika kinyume cha Sheria ya Madini inayowataka wanaofanya kazi hiyo kuwa na leseni.

"Hatujapata malalamiko ya uchimbaji wa mchanga eneo hilo. Wanaofanya hivyo, wanavunja sheria, hivyo tukiwabaini tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria," anaonya.

HATUA ZA MKOA

Ofisa Maliasili na Mazingira Mkoa wa Mtwara, Ronald Panga, anabainisha misitu inayopatikana eneo la bahari pekee ni hekta 14,000 na kwa Mkoa wa Mtwara inapatikana katika vijiji vitano, ikiwa ni pamoja na Mikindani.

Anasema misitu ya mikoko inatumika kuzuia mmomonyoko wa udongo, chakula cha viumbe wakiwamo samaki na kuhifadhi bahari, akiyataja maeneo makuu yaliyoathiriwa na shughuli za ukataji wa mikoko kuwa ni Mikindani na Shangani.

Panga anasema kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002, hairuhusiwi mtu yeyote kukata miti ya msitu bila kibali maalum, hivyo waliokuwa wanakata mikoko walifanya uvunaji haramu.

Anasema shughuli hizo zilifanyika usiku kwa sababu wanajua ni kosa na kazi kubwa, akibainisha kuwa miti hiyo ilitumika kama fito za kujengea nyumba na kuni za kuchomea matumbawe.

Ofisa huyo anataja hatua walizozichukua kudhibiti uharibifu huo ni kutoa elimu ya umuhimu wa misitu hiyo, njia mbadala ya kututumia kujengea badala ya miti na athari za ukataji miti, yakiwamo mabadiliko ya tabianchi.

Anasema moja ya athari za ukataji wa miti hiyo ni kupwa na kujaa kwa bahari na maji kuingia kwenye makazi ya watu.

Panga anasema eneo la Mikindani limeathiriwa zaidi kwa kuwa nyumba zake nyingi zipo ndani ya mita 60 kutoka baharini kinyume cha Sheria ya Mazingira.

"Wengi wa wakazi wa Mikindani wapo ndani ya maji, wengine mita 10, wengine mita tano kinyume cha sheria," anabanisha.

Panga anasema Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanazuia shughuli hizo na kutoa elimu kwa jamii na kueleza faida za misitu hiyo.

Ofisa huyo pia anabainisha kuwa katika eneo la Mikindani wanatekeleza mradi wa kuongeza fukwe na kuzuia mmonyoko wa udongo kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

Panga pia anakiri kuwapo shughuli za uchimbaji mchanga kufuatia malalamiko aliyopokea kutoka kwa wadau wa maendeleo katika eneo hilo, akiahi kufanyia kazi kwa kushirikiana na uongozi wa halmashauri hiyo.

Anasema wanaendesha kampeni ya kuotesha mikoko katika maeneo ambako imekatwa ili kurejesha hali ya zamani.

KAULI YA NEMC

Meneja wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mkoa wa Mtwara, Boniphace Guni, anasema hana taarifa ya shughuli ya uchimbaji mchanga katika eneo hilo, akisisitiza ni kinyume cha sheria.

Guni anaahidi kufuatilia taarifa hiyo aliyoipokea kutoka Nipashe na baadaye kutoa taarifa kuhusu suala hilo.

Nipashe pia inatua mezani kwa Ofisa wa Mkazi Wizara ya Madini Mkoa wa Mtwara, Ephraim Mushi ambaye anasita kutoa taarifa kuhusu tatizo la uchimbaji mchanga katika eneo la Mikindani, akisisitiza ni sharti apate kibali kutoka ngazi ya juu ya wizara hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Mkoa wa Mtwara, kwa sasa mkoa huo una leseni 386, leseni 17 za utafiti, leseni moja ya uchimbaji mkubwa, leseni nne za uchimbaji wa kati na leseni 364 za uchimbaji mdogo.

MIKOKO KITAIFA

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii (1991 na 2015), kumekuwapo na kupungua kwa mikoko katika ukanda ya kaskazini na kusini kutoka hekta 11,159 hadi 1,701 na kutoka hekta 35,159 hadi 30,981 katika mwaka 1991 hadi 2015 mtawalia.

Hata hivyo, taarifa hiyo inabainisha kumekuwapo na ongezeko la mikoko kutoka hekta 68,390 mwaka 1991 hadi hekta 125,418 mwaka 2015 katika Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Juni mwaka huu ilizindua Mpango Kabambe wa Taifa wa Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira.

Lengo Kuu la Mpango Kabambe huo ni kutoa mwongozo wa hatua za kuchukuliwa kutatua shida za mazingira nchini kwa kuzingatia sehemu husika na hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa.

Malengo mahsusi ya Mpango Kabambe ni kuainisha hali ilivyo ya shida za mazingira ikiwamo visababishi, athari zake, hatua zilizoendelea kuchukuliwa na vikwazo.

Vilevile, kutoa mwelekeo wa kimkakati wa mabadiliko yanayohitajika kuleta matokeo chanya, kuainisha maeneo ya vipaumbele na kuainisha hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na shida za mazingira husika.

Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na ni miongoni mwa nchi zilizowasilisha mchango wake wa kukabiliana na athari hizo katika Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi Julai 30 mwaka jana.