Hoja ya nani bora kati ya wachezaji hawa wawili itadumu miongoni mwa mashabiki kwa miaka mingi ijayo. Kutokana na idadi ya mabao yaliyofungwa, mataji na rekodi zao binafsi, Ronaldo na Messi wanapambana kila mara.
Ronaldo hajawa katika kiwango cha juu msimu huu. Nyota huyo wa Manchester United ameanza taratibu akiwa na mabao matatu pekee na asisti moja katika mechi 14 alizocheza.
Kwa upande mwingine, Messi anaonekana hatimaye amerudi kwenye ubora wake katika maisha ya Ufaransa na Paris Saint-Germain. Nyota huyo wa zamani wa Barcelona amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akifunga mabao 11 na asisti 12 katika mashindano yote hadi sasa.
Kukosekana kwa Ronaldo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuanza kwake polepole msimu huu, kumemwezesha Messi kuzifikia baadhi ya rekodi za nyota huyo wa Ureno na pia kuzipita nyingine.
Bila kuchelewa, makala haya yanaangalia rekodi tatu za Ronaldo ambazo zimevunjwa na Messi hadi sasa msimu huu...
#1. Amezifunga timu nyingi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (40)
Lionel Messi kwa sasa anashikilia rekodi ya kufunga dhidi ya timu nyingi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina, amefunga dhidi ya timu 40 kati ya 44 alizokutana nazo kwenye michuano hiyo barani Ulaya tangu alipoanza kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Mwanzoni mwa msimu wa sasa, Messi na Ronaldo walikuwa wamefungana kwa idadi ya timu walizofunga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (38). Hata hivyo, fowadi huyo wa PSG alimpita mpinzani wake alipofunga katika ushindi wa 3-1 wa klabu yake dhidi ya Maccabi Haifa, Septemba 14, mwaka huu.
Kisha akaendeleza rekodi hii alipofunga bao pekee la PSG katika sare ya 1-1 na Benfica.
#2. Mabao mengi yasiyo ya penalti (681)
Ronaldo na Messi ni wachezaji wawili waliofunga mabao mengi zaidi katika historia ya soka. Gwiji huyo wa Manchester United ndiye mfungaji bora wa muda wote katika soka la wanaume akiwa na jumla ya mabao 818, huku nyota huyo wa PSG akiwa na mabao 785 katika maisha yake ya soka.
Hata hivyo, ni nahodha huyo wa zamani wa Barcelona ambaye amefunga mabao mengi zaidi yasiyo ya penalti. Wachezaji hao wote walikuwa wamefungana kwa idadi ya mabao yasiyo ya penalti (671) mwanzoni mwa msimu wa 2022-23, lakini Muargentina huyo alimpita Ronaldo alipofunga bao la ushindi la PSG dhidi ya Olympique Lyon, Septemba 18, mwaka huu.
Kwa bao lake dhidi ya Lyon, Messi aliwapita Pele na Cristiano Ronaldo kwa mabao mengi yasiyo ya penalti katika historia ya soka.
Kwa sasa ana mabao 681 yasiyo ya penalti, nane zaidi ya Ronaldo, ambaye ana 673.
Wachezaji wote wawili wamekuwa na uwezo mkubwa wa kupiga penalti, jambo ambalo limeongeza idadi yao ya mabao. Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid kwa sasa ana mabao 145 ya penalti huku Muargentina huyo akiwa na mabao 104 aliyofunga kutokana na penalti.
#3. Mabao mengi nje ya eneo la hatari Uefa (23)
Kukosekana kwa Ronaldo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kumetoa mwanya kwa Messi kuziba pengo hilo na kumpita kwenye baadhi ya rekodi za mashindano hayo.
Mshindi huyo mara saba wa Ballon d'Or, hivi majuzi alimpita mpinzani wake kwa mabao ya nje ya eneo la hatari kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (23). Yuko mbele ya Ronaldo kwa bao moja, ambaye ametikisa nyavu mara 22 kutoka nje ya eneo la hatari.
Tangu mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2004-05, Messi amefunga mabao mengi kutoka nje ya eneo la hatari kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye mashindano hayo (23, moja zaidi ya Cristiano Ronaldo).
Alipata mafanikio hayo alipofunga bao la nne la PSG katika ushindi wa 7-2 dhidi ya Maccabi Haifa.










