Hii inakuja baada ya mapema mwaka huu Timu ya Soka ya Taifa ya Wasichana wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), kufanikiwa kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya Kombe la Dunia mwezi uliopita huko nchini India.
Katika fainali hizi za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, Simba Queens inapeperusha bendera ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kutwaa taji hilo katika michuano ya ukanda huo iliyofanyika Dar es Salaam, Agosti mwaka huu.
Simba Queens ilianza fainali hizo kwa kuchapwa bao 1-0 na wenyeji ASFAR FC ya Morocco lakini ikaamka katika mechi ya pili kwa kuifunga Determine Girls kutoka Liberia mabao 2-0 na juzi usiku ilikuwa na kibarua kizito cha kuikabili Green Buffalo kutoka Zambia ambayo yenyewe ilihitaji matokeo ya sare ya aina yoyote ili isonge mbele katika michuano hiyo lakini ikajikuta nayo ikichapwa 2-0.
Mechi za hatua ya nusu fainali sasa zitachezwa keshokutwa, Jumatano na Simba Queens itakutana na timu iliyoshika nafàsi ya kwanza katika Kundi B ambao ni Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Mamelodi Sundowns Queens kutoka Afrika Kusini huku ASFAR FC ikikutana na mshindi wa pili wa kundi hilo.
Katika fainali za kwanza za michuano hii zilizofanyika mwaka jana huko Misri, CECAFA iliwakilishwa na Mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Kenya, Vihiga Queens ambao waliishia hatua ya makundi.
Kocha abadili kikosi
Katika kuhakikisha timu yake inafanya vizuri na hatimaye inasonga mbele, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula, aliamua kupangua kikosi chake wakati anaivaa Green Buffalo ambayo ni mabingwa wa Ukanda wa COSAFA.
Lukula aliamua kuwaweka benchi Vivian Corazone Odhiambo, kiungo Mkenya ambaye hakuonekana kuwa na mchezo mzuri katika mechi mbili zilizotangulia dhidi ya ASFAR FC na Determine Girls, lakini nyota huyo aliingia kuwakabili Wazambia akitokea benchi na kufufua makali kwenye kikosi hicho cha Malkia wa Wekundu wa Msimbazi.
Kocha huyo pia aliamua kumweka nje mshambuliaji raia wa Burundi, Asha Djafari, kama mwenzake, alipoingia alicheza mpira wa kasi, akipoteza nafasi ya kufunga ya kwanza aliyoipata, akajiuliza na kuendelea kulisakama lango la wapinzani na kufanikiwa kufunga bao la kwanza na kuwainua mashabiki wa timu yake waliokuwa wakiwafuatilia wawakilishi hao.
Mshambuliaji mwenye nguvu na mwili mkubwa kutoka Ghana, Philomena Abaka alianza kwa mara ya kwanza juzi, lakini alishindwa kuonyesha makeke yake baada ya kuumia na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Asha.
Haikuwa siku nzuri sana kwa winga, Pambani Kuzoya ambaye alishindwa kuonyesha cheche kama alivyofanya katika michezo miwili iliyopita sawa na Olaiya Barakat ambaye alianzishwa kwa mara ya kwanza, aliisaidia timu lakini si kwa kiwango alichocheza wakati Simba Queens inawafungwa Determine Girls.
Nahodha, Oppa Clement na mabeki, Fatma Issa 'Fetty Densa', Daniella Ngoyi pamoja na golikipa chaguo la kwanza la timu hiyo, Gelwa Yonna, waliendelea kuzitendea vema nafasi zao na wametoa mchango mkubwa kuifikisha timu katika hatua ya nusu fainali.
Kiungo Joelle Bukuru, si tu amejua kuiongoza vema timu yake, lakini ndiye kiungo anaongoza kwa kucheza pasi nyingi kwenye mechi za hatua ya makundi ya fainali hizi.
Akizungumza na gazeti hili, Lukula, alisema anawaamini wachezaji wake wote na bado moyo wake unamwambia watacheza fainali za michuano hii.
Lukula alisema mechi zote ni ngumu kwa sababu wanakutana na ingwa kutoka nchi mbalimbali, hivyo hakuna mchezo atakaoudharau katika fainali hizi zinazotarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 13, mwaka huu.
"Mimi nimekuja kushiriki mashindano, sitaki kurudi nyumbani mapema, tuko hapa Morocco mpaka siku ya mwisho," hayo ni maneno ambayo kocha huyo wa zamani wa She Corporate ya Uganda alikuwa akiyarudia mara kwa mara anapozungumza na wachezaji.
Kocha huyo aliongeza kuwa anatamani kuona malengo yake ya kubeba ubingwa wa Afrika yanatimia ikiwa ni mara yake ya kwanza anashiriki katika fainali hizi.
"Tumekuja kushindana, tumekuja kusaka heshima ya Simba, Tanzania, CECAFA, na sisi wenyewe kama wachezaji na mimi kocha wenu, tunataka kumaliza safari tuliyoianza Dar es Salaam, tunaweza, uwezo tunao," Lukula alisema.
Aliongeza anafahamu kufanya vizuri katika mashindano haya kutapandisha heshima na thamani ya klabu yao ambayo kwenye michuano ya kimataifa kwa upande wa wanaume inaogopwa.
Naye nahodha wa Simba Queens, Oppa alisema kujituma kwa kila mmoja wao ndio siri ya mafanikio na wanaahidi wataendelea na kasi hiyo kwenye mechi itakayofuata.
"Hatujamaliza kazi, tumekuja kupambana na hatujaja Morocco kusindikiza, tunazidi kumshukuru Mungu kwa hatua tuliyofikia, kazi ilikuwa kubwa na ngumu," alisema mshambuliaji huyo.
Bingwa wa michuano hii inayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), atapata Dola za Marekani 400,000 wakati mshindi wa pili ataondoka na kitita cha Dola za Marekani 250,000. Timu zilizoingia nusu fainali yaani itakayomaliza nafasi ya tatu na nne kila moja itaambulia Dola za Marekani 200,000.
Timu nyingine zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye hatua ya makundi kila moja itapata Dola za Marekani 150,000 na kifuta jasho cha Dola za Marekani 100,000 kitakwenda kwa walioburuza mkia kwenye hatua hiyo.










