Ruwasa inapopania ‘kuwatua mama ndoo’ vijijini

05Nov 2022
Joseph Mwendapole
Dar es salaam
Nipashe
Ruwasa inapopania ‘kuwatua mama ndoo’ vijijini
  • Miradi mipya 1,258 yaanzishwa 604 yakamilika

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imefanikiwa kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji wananchi wa vijijini ikiwa ni miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019.

1; Baadhi ya visima vya maji vinavyochimbwa kuwakomboa wananchi wa maeneo ya vijijini kutoka kwenye shida ya maji.

 

Hivi karibuni Mkurugenzi wa usambazaji RUWASA, Bwire Mkama, amezungumzia changamoto, mafanikio na nini mpango mkakati wa kuhakikisha wanafikisha asilimia 100 kwa wananchi waishio maeneo hayo.

Ametoa maelezo hayo wakati wa kikao kazi baina ya wakala na wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Mkurugenzi huyo anaanza kwa kusema kwamba majukumu ya RUWASA ni kupanga, kusanifu, kujenga na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi na uchimbaji wa maji chini ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kusafisha visima, kufanya upimaji wa wingi wa maji na ukarabati wa visima.

Anataja majukumu mengine kuwa ni kufanya usanifu na ujenzi wa mabwawa ya aina tofauti, ikiwa ni pamoja na kupima aina ya miamba na udongo kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa na kazi zingine za kihandisi ikiwemo kufuatilia na kutathimini utendaji wa vyombo vya utoaji huduma ngazi ya jamii.

Mhandisi huyo anaeleza wakati wakala inaanzishwa mwaka 2019 asilimia 64, ya wananchi wa maeneo ya vijijini ndiyo ilikuwa ikipata maji safi na salama lakini kufikia Desemba mwaka 2020 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia asilimia 70.

Anasema hadi Juni mwaka huu idadi ya wananchi wa vijijini waliokuwa wakipata maji iliongezeka na kufikia asilimia 74 na kwamba lengo ni kufikia kiwango kilichoainishwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), inayotaka asilimia 85 ya wananchi wa vijijini wawe wamefikiwa na huduma hiyo ifikapo mwaka 2025.

Mhandisi Bwire anasema wakala inatekeleza miradi mingi ambayo mingine inagharamiwa kwa fedha za ndani na mingine mashirika mbalimbali ya kigeni kama mradi wa uboreshaji wa miongozo na mifumo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Anasema ujenzi wa miundombinu ya maji unafanywa kwa fedha za ruzuku na fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) wakati ujenzi wa miundombinu ya maji, kuimarisha mifumo, kujenga uwezo wa utoaji wa huduma vijijini unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Pia mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji na kujenga uwezo wa utoaji wa huduma vijijini unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UK AID) ambalo kwa sasa linafahamika kama (FCDO).

Mhandisi Bwire anaeleza pamoja na mafanikio yote hayo RUWASA inakabiliwa na upungufu wa watumishi 822 wa kada mbalimbali wakiwemo waendesha mitambo na madereva.

Anasema hadi Oktoba mwaka huu Ruwasa ina jumla ya watumishi 1,660 sawa na asilimia 66.7 ya mahitaji halisi ya watumishi 2,482, hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 822.

Anasisitiza kwamba upungufu wa watumishi hao uko kwenye kada za kimkakati kama vile za ununuzi, uhasibu, ofisa maendeleo ya jamii, waendesha mitambo na madereva.

Anasema pamoja na changamoto hiyo, RUWASA bado inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mipya na iliyorithi kutoka katika halmashauri mbalimbali za Wilaya.

Mhandisi Mkama anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, RUWASA imerithi miradi 632 kutoka halmashauri hizo ikiwa haijakamlika lakini hadi mwaka huu miradi 607 imeshakamilika ambayo ni sawa na asilimia 96.

Anasema vijiji vinavyonufaika na miradi hiyo ni 1,027 na jumla ya wananchi ambao wanaendelea kunufaika na kukamilika kwa miradi hiyo ni 1,901,854 wakati gharama halisi iliyotumika kutekeleza miradi hiyo imefikia Sh bilioni 154.1.

Mhandisi Bwire anasema RUWASA ilirithi miradi ya maji 177 iliyokamilika lakini ilikuwa haitoi maji, mpaka sasa wamefanikiwa kukamilisha miradi 147 inayotoa maji ambayo ni sawa na asilimia 83.

Anaongeza kwamba vijiji vinavyonufaika na miradi hiyo kwa sasa ni 203 na wananchi 657,264. Gharama iliyotumika kurekebisha miradi hiyo ya maji ni Sh. bilioni 6.2.

Anasema katika kipindi cha miaka mitatu RUWASA imekuwa ikifanya utafiti wa kutafuta maji ardhini, na ilipanga kuchimba visima 1,358 lakini imefanikiwa mpaka sasa kuchimba visima 627, visima vinavyoendelea kusambaza maji ni 435.

Gharama iliyotumika kuchimba visima vyote hivyo ni Sh bilioni 18.8 na kuongezaa kuwa tangu kuanzishwa kwake RUWASA imeshaibua miradi mipya 1,258 ambayo 604 imeshakamilika.

Anasema vijiji vilivyonufaika na visima hivyo ni 1,673 na wananchi ambao wananufaika na maji hayo ni 2,820,180 wakati gharama iliyotumika kuchimba ni Sh bilioni 240.4.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala, Mhandisi Clement Kivegalo anasema ili kuondoa malalamiko ya ucheweshaji wa malipo ya wakandarasi wakala imekuja na teknolojia mpya itakayomwezesha mkandarasi kufuatilia malipo yake kidijitali.

Anasema wanaandaa mfumo huo kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Maji na kwamba lengi ni kuondoa ukiritimba na ucheleweshaji wa malipo ya makandarasi.

Aidha, anasema wakala imeamua kuja na mfumo huo baada ya malalamiko ya makandarasi kucheleweshewa malipo yao hali ambayo inaweza kuathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji na kusababisha malalamiko ya watu.

Anasema kupitia mfumo huo ambao uko kwenye majaribio, mkandarasi anaweza kuingia kwenye mfumo kupitia simu yake ya mkononi na kuangalia malipo yake yamefikia sehemu gani bila ya kufunga safari kwenda RUWASA au kupiga simu mara kwa mara.

“Tunataka mkandarasi akishakabidhi hati zake za madai RUWASA asilazimike kurudi tena au kupiga simu mara kwa mara. Kupitia mfumo huu ambao tunaufanyia majaribio kwenye mikoa mitano mkandarasi atakuwa na uwezo wa kuchungulia kupitia simu yake malipo yake yako sehemu gani,” anasema

Anasema wamemua kufanya hivyo ili kuweka uwajibikaji kwa watumishi wa wakala wanaohusika na malipo kubaini atakayezembea kufanya malipo hayo kwa wakati uliopangwa aweze kuwajibishwa na kutoa maelezo kwanini ameshindwa kutimiza wajibu wake.

“Huu utaratibu wa mtu kuamua amlipe nani na wakati gani ni ukiritimba ambao unasababisha hisia za rushwa na umeleta malalamiko mengi, lakini sasa mwarobaini wa haya yote ni mfumo huu mpya kwa sababu mhusika hatalazimika amwone mtu ana kwa ana ndipo amlipe,” anasisitiza.