Shule ya Msingi Bombo -Tanga Yatimiza miaka 100 na kuporomoka.

12Apr 2016
Lulu George
Tanga
Nipashe
Shule ya Msingi Bombo -Tanga Yatimiza miaka 100 na kuporomoka.

SHULE ya Msingi Bombo iliyopo jijini Tanga, ni miongoni mwa shule zilizojengwa tangu utawala wa kikoloni mwaka 1902 yaani zaidi ya miaka 100 iliyopita.

jengo la shule ya bombo likiwa limebomoka , baada ya kudumu kwa zaidi ya miaka 100 bila kufanyiwa ukarabati.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule zenye sifa nzuri na kuongoza katika kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba.

Kwa sababu ya majengo ya shule hiyo kujengwa miaka mingi bila kkufanyiwa ukarabati kwa kipindi chote hicho shule hiyo sasa imeanguka hatua iliyolazimisha wanafunzi wote kuhamishwa kwenye Shule ya msingi Mkwakwani ili waendelee na masomo.

Shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 1,063 na walimu 25 ambao wote sasa wanalazimika kutumia jengo moja la shule ya Darajani hata kusababisha mlundikano mkubwa wa wanafunzi darasani na walimu ofisini.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Bombo ,Mushi Denis anasema kwa sasa zaidi ya wanafunzi 2,000 wanatumia jengo la shule moja idadi ambayo imesababisha darasa moja kuwa na wanafunzi 100 hatua ambayo iliyosababisha mlundikano mkubwa wa wanafunzi darasani.

Denis anasema shule yake yenye umri wa zaidi ya miaka 100 tangu ilipojengwa mwaka 1902 ilianza kubomoka kushuka kwa paa kwenye ofisi ya walimu, hali iliyoendelea kwenye vyumba vya madarasa vya wanafunzi hivyo kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Kutokana na hali hiyo anasema kwamba walifikisha taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga aliyeagiza kuhamishwa kwa wanafunzi na walimu tangu mwezi Julai mwaka jana ili kusubiri taratibu za ujenzi wa shule hiyo kuendelea.

“Tumehamishwa tangu mwaka jana tupo hapa Mkwakwani, lakini hali si nzuri kwa kweli kwani kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba mwaka jana kilishuka sana kutokana na msongamano wa walimu na wanafunzi katika shule hii ,”anasema Mwalimu Mkuu huyo.

Kwa mujibu wa Mwalimu huyo ni kwamba, hali hiyo ya msongamano wa wanafunzi darasani imesababisha wanafunzi kushindwa kufuatilia masomo kwa umakini na hivyo kushuka kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi
waliomaliza darasa la saba mwaka jana.

“Mfano tu ni matokeo ya darasa la saba mwaka jana, kati ya watahiniwa 106 wanafunzi 97 ndio waliofaulu wastani wa 130 tofauti na mwaka juzi ambao kulikuwa na ufaulu kwa wastani wa 141 hili ni tatizo na tunaomba
serikali ya wilaya ya Tanga iharakishe katika ujenzi wa shule yetu,” anafafanua Mwalimu Mushi.

Anaiomba serikali kuharakisha ufumbuzi wa tatizo kwani limekwamisha sana utendaji wa shughuli za maendeleo ya wanafunzi wa shule hiyo zinazotakiwa kufanyika kila siku.

“Tulijaribu kuwapanga ili waingie kwa shifti lakini bado pia siyo suluhu ya tatizo, kimsingi elimu bora inaanzia kwenye mazingira halisi ya majengo, hata walimu wanashindwa kufanya kazi zao vizuri kwani staff room hii wanayotumia kwa sasa haitoshelezi.

Wageni tupo 25 ukilinganisha na wageni hali hiyo inafanya wengine walazimike kukaa nje chini ya mti,”anasema.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanasema uamuzi wa kuhamishwa ulikuwa ni mzuri lakini bado changamoto ni kubwa hasa ya mlundikano darasani.

“Kwenye dawati mnakaa zaidi ya wanne sasa kuandika ni shida. Hata wakati mwingine kwa wale wanaokaa nyuma hawasikii mwalimu kasema nini tunaomba tupate majengo yetu ili tusome vizuri,” anasema mmoja wa
wanafunzi hao.

Akizungumzia hali hiyo Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mustapha Mhina anasema kuwa, katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa awamu iliyopita walipitisha bajeti ya sh. Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Mhina anasema kuwa, Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa sasa inaendelea na mzungumzo na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu mkoani humo ili kunusuru hali hiyo.

“Pia tunafanya mazungumzo na wamiliki wa shule ya Burhan ili tuone kama kuna namna yoyote ya kutumia jengo lao kwa muda kwanza ,” anafafanua Meya huyo.

Anasema katika mwaka wa fedha wa 2014-2015 Halmashauri ya Jiji la Tanga imeshindwa kufanya miradi yoyote ya maendeleo kutokana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kuikabili sekta ya elimu mkoani Tanga na kwa upande wa walimu kuna upungufu wa walimu 186 katika shule 77 za serikali zilizopo Jijini Tanga huku walimu 80 wakiripotiwa
kuwa ni wagonjwa hivyo hawatoi huduma ipasavyo na kwa wakati kutokana na kulazimika kwenda kwenye hospitali za rufaa mara kwa mara kwa ajili ya matibabu.

Akizungumzia changamoto hizo za sekta ya elimu mkoani Tanga Ofisa Elimu Mkoani, Mayasa Hashim anasema kuwa, kwa upande wake mkoa changamoto kubwa iliyojitokeza ni uhaba wa madawati ambapo zaidi ya madawati 41,992 yanahitajika ili kukidhi mahitaji yaliyopo sasa.

Hashim anasema, kutokana na hali hiyo ameshatoa agizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha kuwa, mbinu walizotumia katika kukamilisha ujenzi wa maabara zinatumika kupata madawati mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

“Madawati haya tunayahitaji sana sasa kama wanaomba kibali cha kukata miti waombe na wafanye hivyo mara moja tumekamilisha zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza maana yake mahitaji ya samani ni muhimu kuwepo shuleni kwa wakati,”anasema.

Kuhusiana na upungufu wa walimu anasema wamepokea mwongozo kutoka Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( Tamisemi )ambao
wameusambaza kwenye Halmashauri ili kuainisha mahitaji ya walimu kishule na aina ya masomo wanayohitajika.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, katika suala zima la utendaji kwa kipindi cha siku 100 tangu kuanza kwa awamu ya tano ya utawala wa Rais John Magufuli kwa upande wa mkoani Tanga baadhi ya mafanikio yameanza kuonekana ikiwemo kupatiwa fedha za uendeshaji wa shule za msingi na sekondari kutoka Hazina takriban kiasi cha sh.milioni 782.9.

Kiasi hicho cha fedha Sh. milioni 263.2 kwa ajili ya shule za msingi na zaidi ya sh.milioni 519.7 ni za shule za sekondari.
Kwa upande wa uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa mwaka huu watoto 50,852 wameandikishwa kati ya 64,513 sawa na asilimia 79 ambapo wavulana ni 25,423 na wasichana ni 25,429.