Jiji Tanga lawapima wanafunzi Ukimwi kwa hiari

12Apr 2016
Lulu George
Dar
Nipashe
Jiji Tanga lawapima wanafunzi Ukimwi kwa hiari

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Pasadit la Kanisa Katoliki Tanga zimewapima kwa hiari Virusi vya Ukimwi wanafunzi wa shule na kutoa elimu kuhusu lishe bora.

Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mosses Kisibo.

Takriban wanafunzi 135 wa shule 18 za Msingi na moja ya sekondari Jijini hapa wamekutwa na tatizo la ukosefu wa lishe bora na kupata utapiamlo.

Wanafunzi 1,927 walikutwa na dalili ya utapiamlo wavulana ni 1,125 na wavulana 802 kati ya hao 135 walikuwa na utapiamlo.Wasichana ni 53 na wavulana 82.

Mpango huo ulihusisha wanafunzi
10,879.Wavulana ni 5,338 na wasichana 5,541.Kwa upande wa upimaji wa hali ya lishe wanafunzi 8,808 hawakukutwa na utapiamlo yaani wavulana ni 4129 na wasichana 4679.

Utapiamlo.

Utapiamlo ni ukosefu wa lishe bora unaosababisha udumavu wa mwili unaoshambulia sana watoto, hivyo ni muhimu kuangalia madhara yake ili kuweza kukabiliana nao kwa usalama na afya ya watoto.

Utapiamlo unaathiri ukuaji wa mwili na akili ya
mtoto.Idadi ya watoto wanaopata ugonjwa huo hapa nchini inakadiriwa kuwa ni asilimia 42 na inahofiwa kuongezeka. Mara nyingi huwapata watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Utapiamlo hushambulia mwili ambao haupati vyakula bora vinavyohitajika mwilini ili kuurutubisha na kuwa na afya bora.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya utapiamlo husababishwa na ukosefu wa vitamini na madini ya kutosha katika chembe za mwili. Hali hiyo husababishwa na mambo mawili ambayo ni ukosefu wa protini, nishati, vitamini na madini.

Mtoto anapokuwa na ugonjwa kama vile kuharisha, surua, malaria, na magonjwa ya kupumua hudhoofisha sana mwili na kupunguza vitamini na madini.

Hali hiyo humfanya mgonjwa apoteze hamu ya kula na endapo atakula basi atakula chakula kidogo sana ambacho hakitoshelezi mwilini na kumdhoofisha mtoto hivyo kupata utapiamlo.

Kwa upande mwingine, mtoto asiyepata chakula cha kutosha anaweza kuambukizwa magonjwa kwa urahisi. Jambo hilo huongeza idadi ya watoto wanaokufa kwa sababu ya kukosa vyakula vinavyojenga mwili.
Aidha, ugonjwa huo huwashambulia sana watoto kutokana na hali yao ya kukua haraka hivyo kuhitaji nishati na protini nyingi zaidi.

Upimaji wanafunzi

Baadhi ya wanafunzi waliopimwa hali ya utapiamlo na virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi Mosses Kisibo ni Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Jiji la Tanga Mosses anasema kuwa, katika mpango huo wa upimaji hali ya lishe, lilienda sambamba na upimaji wa Virusi vya Ukimwi kwa wanafunzi 5,527 wavulana 2,544 na wasichana 2,983.

Ilibainika kuwa wanafunzi 15 walikuwa wakiishi na maambukizi na tayari wameanza kutumia dawa.Kati yao wasichana sita na wavulana tisa.

Kisibo anasema kuwa, kati ya wanafunzi hao 30 waliokutwa na maambukizi mapya wavulana 21 na wasichana tisa sawa na asilimia 0.5.

Katika utekelezaji wa mpango huo, wanafunzi waliokutwa wameathirika walipewa kadi za kuchukulia dawa kwenye hospitali na vituo vya afya vya Jijini humo.

“Utashangaa kuona vijana hawa wanajitambua, kwani ukiwahoji wanakwambia hatuwezi kufanya mapenzi kiholela na kupata maambukizi mapya vingionevyo tutajiumiza wenyewe, lakini wengine wanapewa dawa na wazazi wao bila
hata kujua wanakunywa dawa kwa kujitibu nini,”anabainisha Kisibo.

Mpango huo, ulihusisha wanafunzi wenye umri kati ya miaka mitano hadi 18 kutoka shule zilizopo kwenye Kata za Nguvumali,Pongwe, Maweni, Usagara, Mnyanjani ,Duga, Mzingani na Chumbageni.

“Kimsingi tumeona hali ya maambukizi kwa watoto bado ipo chini ukilinganisha na ile ya watu wazima, hivyo bado ipo nafasi kubwa ya wazazi kuweza kuwalinda watoto wao na kuwapa elimu ya afya ya uzazi katika makuzi yao,”anasisitiza.

Kimsingi kwa sasa halmashauri inaendelea kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu umuhimu wa wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki mapema ili kama ameathirika aweze kupata mbinu za kumkinga mtoto wake asipate maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Zoezi hili itakuwa endelevu kwani tumepanga kufikia shule zote zilizopo ndani ya halmashauri ya Jiji la Tanga kikubwa ni kutambua kwamba ili mtu aliyeathirika na Ukimwi aweze kuishi vizuri lazima afya yake iende sambamba na uhakika wa upatikanaji wa lishe bora, “anasema
Mratibu huyo.

Changamoto zilizojitokeza
Kwa mujibu wa Mratibu huyo ni kwamba, Idadi kubwa ya wanafunzi ambao
wamekutwa kwenye mpnago huo tayari wanatumia dawa bila wao kujua wanakunywa dawa za kutibu ugonjwa gani kutokana na wazazi wao kuwaficha.

Anasema ni hatari kwa mtoto kutumia dawa bila kujua jambo ambalo linaweza kusababisha hatari za kuambukiza wengine bila kujijua.

“Watoto wakitambua kuwa wanaumwa nini wanakuwa wepesi sana kujilinda hata kulinda wengine, lakini kwenda kuwachukulia dawa kimya kimya na kuwalazimisha wameze bila kujua ni za nini tunatengeneza Taifa la watu
ambao hawajitambui na watashindwa kujisimamia hili ni tatizo
tulilolibaini ambalo lipo ndani ya jamii zetu kwa sasa,”anasema.

Changamoto nyingine walizopambana nazo wakati wa utekelezaji wa mpango huo ni baadhi ya wazazi kuwatorosha watoto wao na kuwakataza kufika shule siku za uetekelezaji wa mpango huo.

“Hali hii ilitupa kiashirio kwamba, wazazi wanajua watoto wana tatizo gani na ndiyo maana wakawaficha, lakini sisi tulitaka kuwaelimisha zaidi na kuhakikishia jamii kwamba, watoto hawa wapo salama ila wanahitaji kuimarishiwa ulinzi kwa maana ya mama kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na hawa wanaokua kupewa elimu ya afya ya uzazi ili waweze kuepuka vishawishi vya mwili wakati wa makuzi yao,”anasema Kisibo.

Hali ya Maambukizi ya VVU jiji la Tanga
Hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa Jiji la Tanga ni asilimia 3.8 ikifuatiwa na wilaya ya Muheza kwa asilimia 2.7.Kimkoa ni asilimia 2.4 kwa takwimu za mwaka 2015/2016 .

Mambukizi ya Ukimwi Kitaifa Maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini yameongezeka kwenye kundi la vijana wenye umri wa miaka kati ya 19 hadi 24 tofauti na ilivyokuwa miaka minne iliyopita.Kundi lililokua limeathiriwa zaidi lilikuwa miaka kati ya 25 hadi 34, imeelezwa.

:Licha ya kwamba kiwango cha maambukizi mapya ya virusi hivyo nchini kimeshuka kutoka asilimia 7 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 5.3 mwaka 2015, takwimu za baadhi ya mikoa ikiwemo Singida, Kigoma, Arusha, Mtwara, Kilimanjaro na Kagera zimeonekana kuongezeka.

Hata hivyo ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yamepungua kwenye maeneo mengi ya nchi kutokana na jitihada za serikali, wadau na wananchi kwa ujumla.

Licha ya mikoa kadhaa kuendelea kuandamwa na maambukizi hayo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo shughuli za maendeleo na mwingiliano wa watu, mikoa ya Tanga na Manyara ndiyo yenye takwimu chache za maambukizi zikiwa na asilimia nne pekee.

Mikakati ya Kitaifa katika udhibiti wa Ukimwi Serikali imepanga mikakati na kusimamia juhudi zinazofanywa na kuendelezwa na wadau wa Ukimwi kuhakikisha kuwa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yanapungua hadi kufikia sifuri ifikapo mwaka 2025.

Hivi karibuni Mwenyekiti Mtendaji kutoka Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk. Fatma Mrisho amekaririwa akizungumza wakati wa mkutano wa serikali na wadau wa Ukimwi kupitia utekelezaji wa programu
za Ukimwi uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dk. Florens Turuka amesema kuwa, serikali imedhamiria kuanzisha mfuko utakaokua unashughulikia masuala ya Ukimwi wakati wa bajeti ya mwaka 2015/2016 wenye lengo la kuondoa maambukizi mapya ya Ukimwi nchini.

Jamii ilitakiwa kutowanyanyapaa waathirika wa Ukimwi bali wawapende na kuwapa moyo ili waendelee kuwa na afya bora kwani serikali inawapigania na kuhakikisha kuwa, wanatumia dawa za kurefusha maisha ili kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Pasadit imefanya zoezi hilo chini ya ufadhili wa World Education International kwa uhisani wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani ( USAID )na Halmashauri ya Jiji inawajibika kutoa wataalamu wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.