Pole Kapombe, pole Azam FC

11Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Pole Kapombe, pole Azam FC

Shomari Kapombe hakucheza mechi ya jana Kombe la Shirikisho dhidi ya Esparence ya Tunisia.

Shomari Kapombe.

Alikosa pia mechi mbili za viporo Ligi Kuu Bara zilizomalizika kwa sare. Hakuwapo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans (1-1), hakucheza pia timu yake ilipokuwa nyumbani dhidi ya Ndanda FC (2-2).

Mechi yake ya mwisho Kapombe kucheza ilikuwa dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini. Beki huyo kwa sasa yuko Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu. Pole Kapombe, tunatumaini utajaliwa afya njema na kurejea nchini.

Mabingwa hao wa Bara msimu wa 2013/ 14, Azam FC walicheza viporo viwili kati ya vitatu walivyonavyo na matokeo yake hayaridhishi.

Katika mechi hizo ambazo Kapombe hakucheza, Azam ilionekana kuyumba na kukosa ushindi. Ni wazi kuwa, Kapombe ni moja ya wachezaji muhimu Azam FC.

KAPOMBE MAJERUHI
Beki huyo alianza kuumwa baada ya kumalizika kwa mechi ya marudiano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini iliyomalizika kwa ushindi wa mabao 4-3.

Kapombe alilazimika kukaa nje na kuanza matibabu huku awali akionekana anasumbuliwa na malaria.
Baada ya kurejea jijini Dar es Salaam, beki huyo hakuonekana tena uwanjani kuikabili Ndanda FC na hapo ndipo uongozi ulipochukua hatua ya kumpeleka Afrika Kusini kupata matibabu zaidi.

Ni wazi kwamba kukosekana kwa Kapombe katika mechi hizo mbili kumeiathiri Azam FC na kulazimika kumtumia Waziri Salum na David Mwantika ambao muda mrefu walikuwa benchi. Pole kwa Azam FC!

Kapombe ndiye beki bora wa kulia kwa sasa mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia.

Kapombe, beki wa zamani wa Simba na Polisi Morogoro amefunga mabao nane kwenye Ligi Kuu na mawili kwenye Kombe la FA na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.

Kapombe pia jana alikosekana katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Esperance.

WAWA AMECHOKA AU AMESHUKA ?
Kiwango cha beki kisiki wa timu hiyo, Pascal Serge Wawa aliyetua Azam FC akitokea El Mereikh ya Sudan hivi karibuni kinaonekana kushuka tofauti na alivyokuwa msimu uliopita.

Kama sio kiwango kimeshuka, basi beki huyo raia wa Ivory Coast anahitaji kupumzika kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo tangu alipotua katika klabu hiyo Desemba 2014.

Baada ya kurejea kwa beki Aggrey Moris ambaye alikuwa anasumbuliwa na majeraha ya goti, benchi la ufundi la timu hiyo linaweza kumpumzisha Wawa ili iweze kumtumia vizuri katika mechi za hatua ya lala salama ya ligi ya Bara.

MAKALI YA KIPRE YAPOTEA ?
Mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Azam FC , Kipre Tchetche msimu huu anaonekana kupoteza makali yake tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita.

Kipre ambaye wiki iliyopita aliumia kifundo cha mguu katika mechi dhidi ya Ndanda FC, bado hali yake haijarejea kwenye kiwango chake cha kawaida na kushindwa kuisaidia timu hiyo kupata ushindi.

"Sijapotea, bado naisaidia timu yangu kufanya vizuri, najua sijafunga magoli mengi, lakini furaha yangu ni kuona tunapata pointi," alisema mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast.

Hata hivyo Kipre ndiye mchezaji wa Azam FC aliyefunga mabao mengi (10) akifuatiwa na nahodha John Bocco (9) huku Kapombe amezifumania nyavu mara saba.