Shinyanga yaja na sheria ndogo ili kutokomeza vifo vya uzazi

18Jun 2019
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Shinyanga yaja na sheria ndogo ili kutokomeza vifo vya uzazi
  • Kutoza faini wajawazito wanaojifungulia nyumbani

VIFO vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi bado vinaendelea kuwa changamoto mkoani Shinyanga.

Wadau wa afya mkoani Shinyanga wakiwa katika kikao cha kutunga sheria ndogo za kutokomeza vifo vya uzazi. PICHA: MARCO MADUHU

Hiyo inatokana na baadhi ya wajawazito kuendekeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, kwa kutohudhuria kliniki na hivyo kujifungulia nyumbani ama kwa wakunga wa jadi.

Kitendo hicho kimeendelea kuwa moja ya changamoto zinazosababisha vifo vitokanavyo na uzazi mkoani humo kutotokomezwa licha ya kupungua.

Sasa serikali ya mkoa wa Shinyanga imekuja na mikakati ya kutokomeza tabia ya wajawazito kutohudhuria kliniki na kuendekeza wakunga wa jadi.

Mkakati mmojawapo ni kutunga sheria ndogo ambazo zitawabana wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati pamoja na kujifungulia kwenye vituo vya afya.

Kwamba kwa watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo, basi watatozwa faini ya shilingi 20,000.

MGANGA MKUU

Dk. Rashid Mfaume, ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Anasema bila ya utungwaji wa sheria ndogo za kuwabana wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitali kwa lazima, kamwe vifo vitokanavyo na uzazi mkoani humo havitaweza kutokomezwa.

Anasema wao kama wadau wenye wajibu mkubwa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi mkoani Shinyanga, wameona ni vyema wakabuni mbinu ya kuvikomesha kabisa.

“Na ndiyo maana tumekuja na mikakati hii ya sheria ndogo zitakazolazimisha wajawazito kuhudhuria kliniki na kwenda kujifungulia hospitalini,” anasema.

MAPENDEKEZO YA SHERIA

Dk. Mfaume anataja mapendekezo ya sheria hizo ndogo ambazo zitatungwa na kuanza kutumika kuanzia ngazi ya kijiji kuwa ni pamoja na kuorodhesha wajawazito wote kwenye maeneo husika.

“Baada ya hapo kuwafuatilia kama wanahudhuria kliniki na kuhakikisha wanajifungulia hospitalini, na wale watakaokwenda kinyume basi watatozwa faini ya Sh. 20,000,” anasema.

Anabainisha kuwa sheria hizo zitakuwa zikisimamiwa na wenyeviti wa vijiji, ambao ndio wako karibu na wananchi, wakifahamu kaya moja hadi nyingine.

Kwamba wenyeviti hawa pia watakuwa na orodha yote ya wajawazito, na watakuwa wakiwahoji wanafamilia sababu za mjamzito kutohudhuria kliniki kabla ya kuwatoza faini.

“Sheria hizi ndogo ni mapendekezo tu ya awali ambapo zingine zitatungwa huko kwenye ngazi ya kijiji kwa kushirikiana na wanasheria wa halmashauri,” anasema na kuongeza:

“Endapo kila mmoja akawajibika kwenye nafasi yake vizuri na kusimamia sheria hizi ndogo, nina uhakika kabisa vifo vitokanavyo na uzazi mkoani hapa vitabaki historia, labda vile tu kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu.”

Dk. Mfaume, anasisitiza kuwa vifo vingi mkoani Shinyanga vinatokana na uzembe wa kutopenda kuhudhuria kwenye huduma za kiafya.

Anabainisha kwamba ni pale tu wajawazito wanapokuwa wamezidiwa wakati wakijifungua majumbani ama kwa wakunga wa jadi, ndipo wanaamua kukimbilia hospitali kupatiwa huduma.

“Wakati huo inakuwa tayari wameshachelewa, na wengi wao hufariki dunia kutokana na kuwa wamevuja damu nyingi,” anasema.

MRATIBU HUDUMA UZAZI

Kwa upande wake Joyce Kandolo ambaye ni mratibu wa huduma ya uzazi na mtoto mkoani Shinyanga, anasema mama anapokuwa ameshika mimba anatakiwa kuhudhuria kliniki ndani ya wiki 12.

“Ni ili aanze kupatiwa vipimo na kinga juu ya kulinda ujauzito wake pamoja na kupewa ushauri nasaha ikiwamo kuzingatia lishe bora,” anasema.

Joyce afafanua kwamba vifo vingi vya wajawazito mkoani humo hutokana na kuvuja damu nyingi wakati wa kijifungua, kifafa cha mimba, pamoja na kupasuka mfuko wa kizazi.

“Na hiyo inatokana na kutozingatia ushauri ambao wanapewa na wataalamu wa afya na kitendo chao cha kutekeleza mambo yao ya mila na desturi za kizamani na hivyo kujikuta wakipoteza maisha,” anasema.

TAKWIMU ZA VIFO

Joyce anataja takwimu za vifo vya uzazi kwa upande wa kina mama, ambapo mwaka 2017 walifariki kinamama 73, mwaka jana 56 na mwaka huu kuanzia Januari hadi Aprili wameshafariki kinamama 18.

Pia anataja takwimu za vifo vya watoto wachanga ambapo mwaka 2017 walifariki dunia watoto 913, mwaka jana walikuwa 815, na mwaka huu 2019 kuanzia Januari hadi Aprili wameshafariki watoto 218.

“Ili vifo hivi vikome, ni lazima wajawazito wapende kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya afya…wasiendekeze kujifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi,” anasema.

RC

Zainabu Telack ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, anakubaliana na mbinu ya kutunga sheria ndogo za kubana wajawazito kuhudhuria kliniki, lakini pia kujifungulia kwenye huduma za kiafya.

“Zijadiliwe haraka zije kwangu nizibariki ili zianze kufanya kazi,” anasema.

Telack anasema ili kumaliza tatizo la vifo vya uzazi mkoani Shinyanga, ni lazima kuachana na tabia ya kubembelezana.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya wamekuwa wakipiga kelele na kutoa elimu ya wajawazito kujifungua kwenye huduma za kiafya, lakini bado hali inaonekana kuwa ngumu, hivyo lazima nguvu itumike,” anasema na kuongeza:

“Pamoja na sheria hizi kuanza kutumika, pia endeleeni kutoa elimu.”

Mkuu huyo wa mkoa anasema serikali inajitahidi kuboresha huduma za afya, ili pamoja na mengine kukomesha vifo vya uzazi, lakini anasema anasikitika kwamba wajawazito wanakuwa wagumu kwenda kupatiwa huduma stahiki.

Telack anasema mwaka jana mkoa huo umejenga vituo 11 vya afya na tisa vipo tayari kuanza kutumika.

“Nasikitika pamoja na juhudi hizo zote, tunaonekana kama vile tunacheza,” anasema.

MKUU WA WILAYA

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ni miongoni mwa washiriki waliohudhuria kikao cha mapendekezo ya utungwaji wa sheria hizo ndogo za wajawazito.

Anasema licha ya sheria hizo kupitishwa na kuanza kutumika pia wahudumu wa afya nao wanatakiwa wawe na kauli nzuri wanapokuwa wakitoa huduma ya uzazi.

Anabainisha kwamba kumekuwa na malalamiko toka kwa kinamama kuwa hukumbana na lugha za matusi wanapokwenda hospitali na ndiyo moja ya sababu za wao kuamua kujifungulia nyumbani ama kwa wakunga wa jadi, mahali ambapo hakuna matusi.

“Sasa ili sheria hizi ndogo zilete matokeo chanya, ni lazima wahudumu wa afya muachane kabisa na matumizi ya lugha chafu, pale mnapokuwa mkiwahudumia wajawazito…tumieni lugha laini itakayowahamasisha wapende kujifungulia hospitali, ndipo tutafanikiwa kwa asilimia 100,”anasema.

WAZIRI

Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee, na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, anakemea tabia ya wahudumu wa afya kuendelea kutoa lugha chafu kwa wajawazito pale wanapokuwa wakiwapatia huduma ya uzazi.

Dk. Ndugulile anakemea tabia hiyo alipokuwa mkoani Simiyu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani mwaka huu.

Anasema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupunguza tatizo la vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi na ndiyo maana imekuwa ikiboresha huduma za afya pamoja na kutenga bajeti kubwa.

“Nawaomba wahudumu wa afya na wauguzi, wakunga mtoe huduma zinazostahili kwa wajawazito na kuacha kuwatolea lugha chafu ili kuwahamasisha kwenda katika vituo vyetu vya afya, mahali ambapo ni salama na hivyo kupunguza vifo vya uzazi,” anasema.

RAIS

Na kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Feddy Mwanga, anawataka wauguzi wakunga kuzingatia maadili ya taaluma yao, kwa kutoa huduma stahiki kwa wajawazito ili kupunguza vifo vya uzazi.