Fahamu namna ya kupata 'Loss Report' kwa njia ya mtandao (Online)

18Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Fahamu namna ya kupata 'Loss Report' kwa njia ya mtandao (Online)

‘LOSS REPORT’ ni taarifa ya upotevu wa mali au nyaraka ambayo hutolewa na Jeshi la Polisi katika vituo vya polisi mara mwananchi anapotoa taarifa ya upotevu wa mali katika Kituo cha Polisi,-

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, (SACP) David Misime. PICHA: JESHI LA POLISI

ili aweze kupata msaada wa kuipata mali yake au kupewa nyingine kama vile kitambulisho na namba ya simu.

 

 

Jeshi la Polisi nchini, katika kuhakikisha linarahisisha upatikanaji wa huduma ya ‘loss report’, mnamo mwezi Mei, 2019 lilianzisha mfumo wa kutoa taarifa ya upotevu wa mali (Loss Report)  kwa njia ya mtandao kwa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kwa sasa huduma hii imeenea nchi nzima kupitia tovuti ya loss report ambayo https://lormis.tpf.go.tz.

 

Akielezea mfumo huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, (SACP) David Misime, alisema kuwa Lormis ni kifupi cha Loss Management Information System. 

 

Mfumo huu ulioanzishwa na Jeshi la Polisi utamwezesha mwananchi kutoa taarifa za upotevu wa mali au nyaraka kwa kupitia mtandao na kuweza kupata ‘loss report’ bila kufika Kituo cha Polisi, isipokuwa kwa anayetoa taarifa ya upotevu wa kitabu cha kumiliki silaha, kadi ya gari, hati ya kiwanja au shamba, huyu itamlazimu kufika kituo cha polisi.

 

“Wananchi mtumie mfumo huu kwani unaokoa muda na ni wa uhakika na unarahisisha upatikanaji wa huduma ya loss report.” SACP Misime alisema.

 

Aidha, Jeshi la Polisi limeanzisha mfumo huu ili kuitikia wito uliotolewa na serikali kuwa ifikapo Juni 30, 2019 taasisi zote zinazokusanya maduhuli ya serikali ziwe zimefanya hivyo kwa njia ya kielektroniki kupitia GePG – Government Electronic Payment Gate way.

 

Hivyo kupitia mfumo huo mwananchi anaweza kutoa taarifa ya kupotelewa mali au nyaraka kwa kutumia kompyuta au simu yenye ‘internet’.

 

Taarifa hiyo inaweza kutolewa akiwa mahali popote pale ilimradi awe na kifaa cha kielektroniki chenye mtandao atakachotumia kutolea taarifa.

 

Ili kutoa taarifa bila kufika kituoni inambidi mwananchi kutembelea tovuti ambayo nimeitaja awali https://lormis.tpf.go.tz inayopatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

 

Akishaingia kwenye tovuti atabonyeza kitufe cha “Sajili Mali Iliyopotea” na ataendelea kujaza fomu  atakayoipata. Baada ya kujaza fomu hiyo atatakiwa kufanya malipo.

 

Aidha, mfumo huu wa malipo wa loss report unaowawezesha wananchi kulipa malipo hayo kupitia mfumo wa kielektroniki yaani Government electronic Payment Gateway (GePG) unapatikana kwenye mitandao yote ya simu na kwenye benki.

 

Mwananchi anapojaza fomu ya Loss report kwenye mtandao atapata namba ya malipo (Control number) ambayo kupitia tovuti hiyo ya polisi inaanzia na 99108 na kuendelea/ kufuatiwa na namba nyingine.

 

Endapo mwananchi ataamua kufanya malipo kupitia benki, anachotakiwa ni kwenda  na  namba ya malipo (control number) na hapo  watamsaidia kufanya malipo.

 

Kama mwananchi atatumia mitandao ya simu za mkononi atakapoandika kodi ya namba ya kufanyia miamala ya fedha ya kampuni ya simu, baada ya hapo atachagua namba 4(lipa bili), halafu atachagua namba 5 (Malipo ya Serikali) na kisha ataingiza namba ya malipo (Control number) yake na kulipa kiasi cha 500/=

 

Kwa wale wananchi waliopoteza laini za simu, kadi za benki  au vitambulisho na kujaza maombi yao kwa kutumia kadi zao za NIDA au namba ya NIDA  hawahitajiki kwenda Kituo cha Polisi kwani mfumo huu wa Loss report umeunganishwa na mfumo wa NIDA ambao una uwezo wa kuthibitisha  taarifa za vitambulisho hivyo moja kwa moja (online).

 

Kwa maana hiyo mwananchi mwenye kitambulisho cha NIDA au namba na akawa amepoteza laini za simu ana uwezo wa kujaza fomu online na kupata loss report yake online. 

 

Kwa wale ambao watatumia vitambulisho vingine na kujaza fomu ya loss report watahitajika kufika Kituo cha Polisi ili kufanya uthibitisho.

 

Kufika Kituo cha Polisi ni kwa sababu zifuatazo:- Moja ni ili Polisi waweze kuthibitisha kwamba aliyetoa taarifa ni yeye kutokana na kwamba kitambulisho alichotumia hakijaunganishwa na hakitumiwi na watoa huduma wengi kama cha NIDA.

 

Aidha, wengine wanaotakiwa kufika kituoni ni wale waliopoteza mali zikiwamo vitabu vya  kumiliki silaha, kadi za gari na hati za nyumba au mashamba hizi zinahitaji uchunguzi wa polisi ufanyike kabla ya ‘Loss Report’ haijatolewa kwa mhusika.

 

Pia ambao wanatakiwa kuendelea kutoa taarifa zao katika vituo vya polisi ni wale ambao hawana simu au kompyuta zenye ‘internet’ itakayowezesha kutoa taarifa ya kupotelewa na mali au nyaraka kwa njia ya mtandao (online). 

 

Kwa wananchi wa aina hii, wakuu wa vituo na wahasibu wameshapata mafunzo na maelekezo ya namna ya kuwahudumia. 

 

Mfumo huu wa kulipia kwa njia ya mtandao (online) na kupata loss report kama nilivyosema tulianza na Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, napenda kuwajulisha kuwa mfumo huu unatumika kwa nchi nzima sasa.

 

Hivyo ninapenda kuwapa taarifa watoa huduma za mawasiliano kuwa kuanzia sasa wawape huduma wananchi wote wanaofika kwao wakiwa na loss report ya kielektroniki.

 

Watoa huduma pale watakapokuwa na mashaka wanaweza kuthibitisha/ kuhakiki kama Loss report ya mwananchi ni halali au ya kughushi kwa kutumia njia mbili:-

 

Njia ya kwanza ni kutembelea tovuti ya loss report ya Jeshi la Polisi ambayo ni https://lormis.tpf.go.tz na kwenda kwenye kitufe cha “Angalia Ripoti yako” hapo ataingiza namba ya malipo (Control Number) ambayo atapewa na mwananchi pamoja na namba ya kitambulisho chake,  ripoti ikitoka itakuwa ni sahihi na isipotoka itakuwa ni ya kughushi.

 

Njia ya pili,   kwa wale watoa huduma ambao wana mifumo ya kielektroniki na wangependa  kujiunga na mfumo huu tunatoa ‘Application Program Interface’ (API) ambayo itaweza kuwaunganisha na hapo wataweza kuwahakiki wateja wao kwa njia ya kielektroniki bila ya kufika au kutembelea tovuti yetu.

 

Ili kupata hii API wawasiliane na Mkuu wa Tehama wa Jeshi la Polisi kwa barua pepe gabriel.mkungu@tpf.go.tz, au incharge wa kitengo cha mifumo ya TEHAMA (godfrey.kapinga@tpf.go.tz).

 

Imetolewa na:-

Kitengo cha Uhusiano,

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi,

Dar es Salaam,

habariphq@gmail.com