Miongoni mwa makundi yaliyo pembezoni kwa mujibu ya Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) ni ya wanawake na wasichana.
Ndiyo maana kwa miongo sasa, dunia imesimama pamoja kutetea haki za wanawake na wasichana dhidi ya ukandamizaji ambao umekuwa ukifanywa kwa kundi hili.
Kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wasichana na hivyo kufifisha ndoto zao za kimaisha na pia mchango wao kwa jamii.
Katika Bara la Afrika, Tanzania ikiwamo wanawake na hususani wasichana bado ni waathirika wa ndoa na mimba za utotoni.
Takwimu kutoka vyanzo mbalimbali zinaonyesha kwamba maelfu ya wasichana wanakosa haki ya elimu kwa mfano kutokana na sababu hizo.
Katikati ya madhira hayo, kuna janga la ukeketaji ambalo limepigiwa kelele na linaendelea kupigiwa kelele na dunia hadi sasa ili litokomezwe.
Linapigiwa kelele kwa sababu ya madhara yake kwa wasichana, jamii na dunia kwa ujumla.
Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinabainisha kwamba mmoja kati ya wasichana 20, amefanyiwa ukeketaji.
Maana ya takwimu hizo ni kwamba, jumla ya wanawake milioni 200 kote duniani wamefanyiwa ukeketaji kwa maana ya kukatwa, kubadilishwa ama kuondolewa sehemu zao za siri.
KWA NINI DUNIA INAPAZA SAUTI
Dunia kwa maana ya UN inapaza sauti dhidi ya kitendo hiki kutokana na madhara yake kwa wasichana na wanawake kwa ujumla.
Vyanzo mbalimbali vinataja baadhi ya madhara ya ukeketaji ni pamoja na matatizo ya kimaungo na kiakili ambayo humwathiri mwanamke katika kipindi chote cha maisha yake.
KWA NINI UNAFANYIKA?
Sasa pamoja na juhudi kubwa za kutokomeza janga hili kuchukuliwa kwenye uga wa kimataifa katika sekta mbalimbali ni kwa nini unaendelea kutendeka, ni swali ambalo wengi wanajiuliza.
Hata hivyo, baadhi ya sababu kubwa zinazotajwa kuwa chanzo cha kuendelea kushamiri kwa ukeketaji hata katika zama hizi za utandawazi ni kukubalika katika jamii, dini, imani potofu juu ya usafi wa mwili na kuhifadhi ubikira.
Na kubwa zaidi kwenye makabila na jamii zinazoendeleza mila hii ni kumwezesha mwanamke aolewe.
Kwamba ameshaingia katika utu uzima na anafaa kuwa mke wa mtu mwenye heshima kimila.
HALI IKOJE NCHINI?
Yumkini juhudi za wadau yakiwamo mashirika mbalimbali yanayopinga ukeketaji na unyanyasaji wa wasichana na wanawake hapa nchini, zimewezesha serikali kutunga sheria ambazo zinatoa adhabu za faini au kifungo cha hadi miaka 30 kwa anayekamatwa.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mila hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, bado ukeketaji unaendelea kufanyika, lakini kwa kificho.
Unafanyika kwa kificho kwa mbinu mpya baada ya serikali kutunga sheria ya kuzuia ukeketaji na adhabu ya hadi miaka 30 kwa mzazi au mlezi atakayekutwa amefanya hivyo.
Kabila la Wakurya lililoko katika mkoa wa Mara, linatajwa kuendeleza ukeketaji likitumia mbinu mpya za kificho.
Linatajwa kuendeleza mila hiyo kwa imani kuwa binti ambaye hajakeketwa katika jamii anahesabika ni laana na mkosi kwa ukoo wake.
AKIPATA MIMBA
Na inapotokea msichana amepata mimba kabla ya kukeketwa hutengwa na familia au ukoo wake na kutupwa mbali ili afe, mwili wake uoze na kuliwa na wanyama au uishe wenyewe.
SUALA LA KUZIKWA
Mwili wa binti ambaye hajakeketwa hauzikwi na familia husika kwa kuwa wakifanya hivyo wanaamini kabisa itakuwa ni kukaribisha mkosi kwa familia husika na kuharibu ukoo wao.
Na inapotokea msichana husika amepata mimba, hutengwa na familia au ukoo wake kwa kutupwa mbali ili afe, mwili wake uoze ili uliwe na wanyama au uishe wenyewe.
VALERIAN MGANI
Valerian Mgani, ni Meneja Mradi wa shirika lisilo la kiserikali la Association for Termination of Female Genital Mutilation (ATFGM), lenye makao yake makuu Masanga, Tarime mkoani Mara, ndiye anayebainisha haya ya jamii ya Wakurya na ukeketaji.
“Mwili wa binti anayefariki ambaye hajakeketwa hauzikwi na familia husika kwani wakifanya hivyo wanaamini kabisa itakuwa ni kukaribisha mkosi katika familia yao na kuharibu ukoo wao,” anasema.
Mgani anayabainisha haya kwenye mkutano wa mashirika zaidi ya 12 yanayopinga ukeketaji na unyanyasaji wa wasichana na wanawake yalikutana hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkutano ambao ulizaa umoja wa kuunganisha nguvu nchini kwa minajili ya kukabiliana na mbinu mpya za ukeketaji wa wasichana na wanawake, zinazofanyika sasa.
Mgani anasema kwamba katika kabila hilo la Wakurya ambao bado wanaendeleza mila hiyo kwa siri, ukeketaji hufanyika kwenye mwaka unaogawanyika kwa mbili.
“Lakini ukeketaji na tohara ya majaribio hufanyika mwezi Oktoba na ikitokea binti wa kwanza kufanyiwa amefariki, wazee wa kimila wa ukoo huupaka mwili dawa nyingi wakiamini ni kuondoa mkosi wa kifo kwenye ukoo na kisha huutupa mbali kwenye ukoo mwingine,” anasema.
BWIREGE
Mgani anautaja ukoo wa Bwirege kwa Wakurya kuwa ni maarufu sana katika utekelezaji wa mila hii.
“Wameishikilia na hawataki kuiacha, lakini wanafanya mengine ambayo hayana utu ndani yake,” anasema.
YASIYO YA KIUTU
Mgani anatoa mfano wa namna walivyomuokoa binti mmoja wa familia hiyo ya Bwirege hivi karibuni ambaye alipata mimba kabla ya kukeketwa.
Anasema binti huyo alichukuliwa na kupakwa dawa nyingi kwa madai ya kuondoa mkosi kwenye ukoo huo ambayo yalimfanya kuwa kama zezeta.
“Baada ya kumpaka dawa walikwenda kumtupa eneo la Nyamwanga Serengeti karibu na mto Mara… tulipata taarifa kutoka kwenye vyanzo vyetu tukashirikiana na polisi kufuatilia na siku ya pili tulimkuta akiwa kwenye kichaka na upande wa pili kuna wazee wa mila wanafanya mila zao,” anasema na kuongeza:
“Kwa kawaida wazee hao baada ya kumaliza mila zao humchukua msichana na kumrusha mto Mara ambako huliwa na wanyama na kupotea… kwa kufanya hivyo wanaamini wameteketeza mkosi ambao ungeweza kuuandama ukoo.”
Mgani anabainisha walimchukua binti huyo akiwa hajitambui na kumhifadhi kwenye kituo cha wasichana.
“Na hivi karibuni amejifungua mtoto wa kiume, lakini kazi kubwa sasa itakuwa ni kumuunganisha na familia yake,” anasema.
KIPIGO WASIOTAKA KUKEKETWA
Katika hili, Mgani anatoa mfano wa mabinti wawili waliopigwa na kaka zao kwa kushirikiana na mama zao kwa madai kwamba walikataa kukeketwa na bado wamelazwa hospitalini hadi sasa.
“Sababu za kaka zao kuwashushia kipigo ni ile hofu ya wao kukosa ng’ombe za kuolea kwani hakuna mwanaume anayeoa mwanamke ambaye hajakeketwa,” anasema.
KIFO MJAMZITO ASIYEKEKETWA
Meneja huyo anasema inapotokea binti amefariki kabla ya kukeketwa na alikuwa mjamzito, mwili wake hauzikwi na ukoo husika kwa imani kwamba kufanya hivyo ni kukaribisha mkosi kwenye familia.
“Binti akifa wenye familia hunyamaza… wazee wa mila huupaka mwili dawa za kienyeji ili usiharibike haraka na inapofika usiku vijana huubeba mwili huo na kwenda kuuweka kwenye koo zingine,” anasema na kuongeza.
“Wanaweza kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 40 kwa ajili ya kwenda kuutupa…kunapokucha, familia ambapo mwili huo umeachwa nayo husubiri giza liingie, kisha vijana wa familia hiyo nao huubeba mwili huo kwenda kutupa kwingine.”
Kwa mujibu wa Mgani, katika kukwepa laana, mwili huo huishia kuachwa porini na kuoza.
“Yote hayo yakichagizwa na wazee wa kimila ambao huiaminisha jamii mambo hayo ambayo kimsingi ni unyanyasaji wa mtoto wa kike,”anasema.
MCHANGO WA NGARIBA
Meneja huyo wa Shirika la ATFGM, anasema katika utafiti wao wamebaini kwamba mila hiyo inaendelea kutokana na kuwa na mahusiano na imani za kishirikina, utajiri na ngariba kupata mali.
Anasema inahusishwa na ushirikina kwa kuwa wanaamini kinyama kinachokatwa kwenye sehemu ya mwanamke kikutupwa kwenye zizi la mifugo, itaongezeka.
“Lakini pia, familia yenye watoto wa kike na kiume hutegemea kupata ng’ombe wengi kutoka kwa watoto wa kike ambao hutumiwa na kaka zao kwenda kuoa kwenye mji mwingine na hivyo familia kutosumbuka kutafuta fedha kwa ajili ya vijana wao kuoa,” anasema.
Mgani anasema familia hufurahi kupata mali nyingi kwamba kunapokuwa na watoto wa kike inahesabika ni utajiri na wanapomwangalia mtoto wa kike hawaoni daktari, mwalimu au mfanyakazi wa baadaye bali mifugo ambayo kwao ndio utajiri.
Mgani anasema kwenye eneo wanalofanyia kazi kuna ngariba 82 ambao kwa msimu mmoja wa ukeketaji hupata wastani wa Sh. milioni 27 hadi 28 kutegemeana na mabinti ngariba aliowakeketa.
“Ngariba anayepata fedha nyingi hivi kwa msimu mmoja ambao ni mara moja kwa mwaka, ukimwambia aache kazi hii bila kipato mbadala kwake ni ngumu sana,” anasema.
CHANGAMOTO ZINGINE
Kwa mujibu wa Mgani eneo kuwa mpakani ni changamoto kubwa kwa maana jamii ya Kikurya inapoona imebanwa kwa upande wa Tanzania, hukimbilia kutekeleza mila hiyo upande wa Kenya.
Ili kutatua changamoto hii anasema inatakiwa nchi zote mbili kuamua kwa pamoja kushirikiana kuunganisha nguvu ya kupambana na jambo hilo, kwani wakiona wamebanwa upande mmoja wanakimbilia upande mwingine.
Aidha, viongozi wa kimila ambao hunufaika na mila hiyo kwa kupewa ng’ombe na heshima yao kuzidi pale ukeketaji unapofanyika, ni changamoto pia.
Anabainisha kuna wakati serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, iliwasainisha makubaliano nao kwamba jamii hiyo itaacha mila hiyo na watashirikiana na wadau pamoja na serikali kuielimisha jamii.
“Lakini viongozi hao wa kimila walipoona msimu wa ukeketaji umekaribia, walienda upande wa Kenya kila mtu kwa sababu zake tofauti tofauti, huku nyuma wakiacha maelekezo ya kukeketa wasichana na wavulana kutahiriwa… tulipowauliza walisema si wao, bali wamefanya wanajamii wenyewe, anasema.
Aidha, anabainisha, wakati wa msimu wa ukeketaji urafiki na wanaopinga suala hilo huisha, kwani vijana wa Kikurya hupakwa dawa za kienyeji ambazo huwafanya kuwa kama vichaa fulani hivi.
“Na ukifanya mchezo wanaweza kukukata mapanga…ikifika wakati huo tunajificha kabisa…hata hivyo wanaopinga kutoka kwenye jamii yao tuliowafundisha, hutumia mbinu kuwaokoa baadhi ya wasichana,” anasema na kuongeza:
“Jambo hili ni gumu sana lakini bado tutandelea kuokoa mabinti wanaopitia changamoto hizi.”
MABINTI WAKIMBILIA KANISANI
Akizungumzia juu ya idadi ya mabinti wanaotoroka kukeketwa, meneja huyo anasema mwaka jana zaidi ya mabinti 300 wa upande wa Kenya, walikimbilia kanisani katika usharika wa Kebaroti.
“Walikutwa wakiwa chini ya mti kila mmoja akitokea eneo tofauti akijaribu kuokoa maisha yake kwani upande wa Kenya, mila hiyo haijapigwa marufuku kama Tanzania,” anasema.
WANAVYOSAIDIA
Mgani anabainisha wameunda vikundi vya ngariba na wasichana ambao wameelimishwa na kupewa mtaji wa cherehani ili wafanye shughuli za kuwaingizia kipato mwaka mzima, ikiwa ni pamoja na elimu ya mara kwa mara ya madhara ya ukeketaji.
LHRC
Kwa upande wake, Ofisa Programu Jinsia, Wanawake na Watoto wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Getrude Dyabene, anasema sheria ya elimu haizuii mtu mzima kukeketwa kwani imemtaja mtoto ni aliye chini ya miaka 18.
Anasema upo umuhimu wa kuwa na sheria ya kulinda makundi yote kwani kinachofanywa sasa na baadhi ya jamii ni kukeketa watoto wa kike waliozidi umri wa miaka 18 na wengine wakiwa darasa la kwanza.
MKURUGENZI
Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga, anasema ili kukabiliana na mbinu za wanajamii katika dhima ya kupinga ukeketaji kunahitajika nguvu ya pamoja ya mashirika na jamii husika, kwani kila siku zinaibuka mbinu mpya za kutekeleza mila hii.
“Mila hii ni sugu kwenye baadhi ya jamii za wafugaji kwani wao wanamuona mtoto wa kike ni mali na si anayetakiwa kwenda shule ili atoe mchango kwa jamii yake,” anasisitiza.










