Hakuna mwenye jibu ila viongozi wa Bara la Afrika wanaijua sababu ni nini.
Wiki iliyopita wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wa Umoja wa Afrika (AU) wanakutana jijini Addis Ababa Ethiopia, makao makuu ya Muungano wa Afrika na mambo makubwa yanayotikisa na njaa, uasi na ukosefu mkubwa wa usalama.
Wakati kikao kinafanyika, ukosefu wa amani umesambaa kwenye ukanda wote wa Sahel kwenye mataifa ya Burkina Faso, Cameroon, Chad, Gambia, Guinea, Mauritania, Mali, Niger, Nigeria na Senegal.
Hali ya usalama katika Sahel ni mbaya na vikundi vya kigaidi vinazidi kutishia maeneo ya kaskazini mwa pwani ya Afrika Magharibi.
Aidha, kukosekana utulivu wa kisiasa katika nchi kadhaa za Sahel na mivutano kati ya Mali na majirani zake umedhoofisha ushirikiano kati ya nchi tano za ukanda huo.
Mtandao wa ‘Global Terrorism Index’ unaeleza kuwa makundi ya 'wanajihadi' yanayofanya kazi katika nchi za Sahel ni pamoja na tawi la al-Qaeda, huko Mali ambalo pia linatishia amani Burkina Faso na Niger. Lakini, lipo Dola la Kiislamu nchini Mali. Aidha, taarifa za kuwapo kwa wanaharakati wa ISIS huko Chad nazo ni za kuhofisha.
MGOGORO DRC
Wakati wakuu wa mataifa ya muungano wa AU yanakutana Addis hali si shwari Congo ambalo ni taifa la pili kwa ukubwa Afrika, makundi ya wanamgambo zaidi ya 120 na vikundi vyenye silaha vinafanya kazi za uhalifu wa kivita hatari zaidi ikitoka kwa M23 inayotwaa kwa mabavu mikoa ya Goma, Kivu Kaskazini na Kivu Mashariki.
Kufikia 2008, vita vya DRC na matokeo yake vilisababisha vifo vya watu milioni 5.4, kutokana na magonjwa, njaa pamoja na vita yenyewe na kuifanya kuwa mbaya zaidi tangu Vita vya Pili. Watu wengine 1,000,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani au waomba hifadhi nchi jirani.
UHASAMA ETHIOPIA
Taifa hili ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika. Ni hifadhi ya wakimbizi takriban 924,000 kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wakiwamo pia wanaotafuta hifadhi wakitokea Sudan Kusini, Somalia na Eritrea.
Kuanzia Novemba 2020, mapigano yalizuka kati ya serikali ya Ethiopia na kikosi cha waasi wa Tigray, wakiongozwa na Chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF).
Mzozo umekuwa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya Waethiopia kuwa wakimbizi wa ndani. Takriban watu 59,000 waliikimbia Ethiopia wakipata hifadhi mashariki mwa Sudan, inasema taarifa ya mtandao wa UNHCR.
Mwaka 2011, taifa jipya la Sudan Kusini lilizaliwa ikiwa ni sherehe na shamrashamra huko Juba, ni baada ya mateso na kudhalilika kwa miongo mingi kutoka kwa Sudan ya Omar Al Bashir,
Sudan Kusini ilitarajiwa kuwa na amani na matumaini lakini miaka minane baada ya uhuru. Balaa lilizuka
Desemba 2013, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalizuka Juba baada ya Rais Salva Kiir kumshutumu makamu wake Dk. Riek Machar, kupanga jaribio la mapinduzi. Uasi uliendelea kati ya vikosi vya serikali vilivyo watiifu kwa kila moja.
Njaa, umaskini, vita, rushwa na uongozi usioaminiana vimeiacha Sudan Kusini kwenye fedhea kubwa na hata sasa ni eneo lisilo na amani, mbaya zaidi likizungukwa na majirani wenye vita kama DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Ethiopia.
Ni viwanja vya machafuko barani Afrika vinavyoongezeka kila mwaka na kusababisha mamilioni ya raia kuteseka kwenye bara tajiri kuliko yote.
AU INAOGOPA KIVULI
Muungano wa Afrika una mikataba mingi ya kuleta amani, kuongeza chakula, kuachana na silaha na kudumisha haki za binadamu.
Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora ACDEG ni waraka uliopitishwa na AU Januari 30, 2007.
ACDEG imesheheni masuala mengi ya kidemokrasia, siasa safi, uongozi, uchaguzi huru na haki, uchumi na kijamii. Hata hivyo, nchi nyingi hazijausani na kuuridhia ikiwamo Tanzania.
Ndiyo maana nyakati za uchaguzi barani humu zimekuwa ni vilio, malalamiko, mauaji na kupinga matokeo na kuifanya Afrika kuwa nchi isiyotaka demokrasia.
KUKOMESHA BUNDUKI
Ni mkataba unaofahamika kama ‘Silencing the Guns in Africa by 2020” Hoja ni kuondoa uasi, ugaidi na kupokonya bunduki na silaha ndogo ndogo, ili kuimarisha amani na utulivu. Afrika hilo ni jambo muhimu katika Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika, inayotaka kuwapo kwa Afrika yenye amani na utulivu wa kisiasa, kiuchumi na utangamano usio na mipaka wala pasi. Ndiyo kufikia Agenda 2063, Afrika Tunayoitamani.
Kampeni ya AU ifikapo 2020 inalenga kuwa na bara lisilo na migogoro, kuzuia mauaji ya halaiki, kuleta amani kwa wote na kuondoa vita na ukiukaji wa haki za binadamu.
Mkataba huo ni kama umebakia kwenye mashelfu kila mahali kuna vita na mauaji kuanzia DRC, Ethiopia, Afrika ya Kati na ukanda wote wa Sahel. Kwanini hakuna utekelezaji?
KUKUZA KILIMO
Ni Azimio la Malabo la AU lilitolewa na Wakuu wa Nchi na Serikali katika kikao cha 23 huko Malabo Equatorial Guinea, Juni 2014. Viongozi waliibuka na kaulimbiu ya ‘Mwaka wa Kilimo wa Afrika na Usalama wa Chakula: "Kubadilisha Kilimo cha Afrika kwa Pamoja ...
Hadi sasa hakuna mafanikio licha ya kukubaliana kutenga fungu kubwa la bajeti kwenye kilimo asilimia 10, Afrika ina njaa.
Katika Mkutano wa Addis Ababa, masuala ya ukosefu wa amani, hali duni na machafuko ya kisiasa, umaskini, njaa na utapiamlo ndizo ajenda kuu zinazotawala, licha ya mikataba hiyo.
Mfano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anatangaza kutoa dola milioni 250 kutoka mfuko mkuu wa dharura (CERF) kukabili njaa na kushughulikia dharura zisizo na ufadhili wa kutosha.
Anatoa tangazo hilo kwa wanahabari jijini Addis Ababa wakati wa kikao cha viongozi wa AU, kwa mujibu wa UN NEWS.
Guterres anasema ni fedha nyingi kuwahi kutolewa na CERF na ni kutokana na ongezeko la idadi kubwa ya watu takribani milioni 339, wanaohitaji misaada ya kibinadamu na kwamba kati ya nchi wanufaika 18, mataifa 12 ni ya Afrika.
Ukiangalia Afrika kila kitu kipo kwenye mipango, mikataba na maazimio yapo ila kinachokosekana ni kuridhia mikataba wanayokubaliana na kuitekeleza. Kama AU haitasimamia mipango, maazimio, mikataba kikamilifu na kuachia kila mwanachama kuamua inavyotaka, Afrika itaendelea kuzama kwenye umaskini, migogoro ya kisiasa, njaa, vita na magonjwa licha ya kuwa ni bara tajiri zaidi duniani.










