Ni mchakato wa kidemokrasia unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii Februari 25, ukiwapeleka wapigakura kuamua ni nani wanayetaka awaongoze.
Wagombea maarufu wanaowania nafasi ya kumrithi Rais Buhari (79), ni Atiku Abubakar, wa Chama cha People's Democratic Party (PDP) na Bola Ahmed Tinubu wa chama tawala cha All Progressives Congress.
Buhari, hatagombea tena uchaguzi amefikia kikomo cha uongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.
WANAOUTAKA URAIS
Tinubu (70), aliliongoza Jimbo la Lagos ambalo ni mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria kuanzia 1999 hadi 2007, amewashinda watia nia wengine 13, akiwamo Naibu wa Buhari, Makamu wa Rais Profesa Yemi Osinbajo, katika mchakato wa kura za mchujo wa chama cha APC.
Tinubu anajulikana kama 'godfather' wa kisiasa katika eneo la kusini-magharibi, ana ushawishi mkubwa, ingawa amekuwa akikabiliwa na madai ya rushwa kwa miaka mingi na afya mbaya, ambayo yote anakanusha.
Wengine wanasema kauli mbiu yake ya kampeni Emi Lokan, ambayo ina maana ‘ni zamu yangu’ katika lugha ya Kiyoruba, inaonyesha hali ya kustahiki.
Atiku Abubakar ni makamu wa Rais mstaafu, akiwa na miaka 76, anagombea kwa niaba ya chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP), ambacho ndicho cha Rais mstafu Olusegun Obasanjo. Amewahi kugombea kiti cha urais mara tano na zote ameshindwa.
Kwa kiwango kikubwa, kazi yake imekuwa katika ukanda wa madaraka, akiwa amefanya kazi kama mtumishi wa juu wa serikali, makamu wa rais chini ya Olusegun Obasanjo na mfanyabiashara maarufu.
Kama vile Tinubu, naye anashutumiwa kwa ufisadi na kuweka urafiki mbele jambo ambalo analikanusha.
Mwingine ni Peter Obi (61), mwenye matumaini ya kuvunja mfumo wa vyama viwili, ambavyo vimetawala Nigeria tangu mwishoni mwa utawala wa kijeshi mwaka 1999 na anagombea kwa chama kidogo kisichojulikana cha Labour.
Ingawa alikuwa katika PDP hadi mwaka jana, anaonekana kama sura mpya na anafurahia kuungwa mkono kwenye mitandao ya kijamii na vijana wa Nigeria.
Mfanyabiashara huyo tajiri amewahi kuwa gavana wa Jimbo la Anambra kusini-mashariki kuanzia mwaka 2006 hadi 2014.
Wafuasi wake, wanaojulikana kama ‘Obedients’ au watiifu wanasema ndiye mgombea pekee mwenye uadilifu, ila wakosoaji wake wanaamini kuwa kumpigia kura Obi ni kuipoteza kwa sababu hakuna uwezekano wa kushinda.
Ojei Chichi, mgombea pekee wa kike, kupitia Chama cha Allied People’s Movement (APM), kama ilivyo kwa nchi zingine za Kiafrika, hana tofauti na wagombea wengine wa kike waliomtangulia na kuonekana kiti cha urais wa Nigeria ni kwa ajili ya wanaume.
Sarah Jubril kutoka kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka 2003, alipata kura 157,560 ambazo ndizo za juu zaidi ambazo mwanamke yeyote hajawahi kufikia hadi sasa nchini humo.
Mitazamo ya kitamaduni juu ya wanawake katika jamii mara nyingi haidumishi usawa kwa wanawake wa Kiafrika.
Uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii ikiwa hakuna mshindi, duru ya pili itafanyika ndani ya wiki tatu.
Pia uchaguzi huu unakwenda sambamba na wa magavana wa majimbo wenye nguvu nchini humo utakaofanyika, Jumamosi ya Machi 11, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC), Mahmood Yakubu, anapuuzia mbali mapendekezo kwamba kura inaweza kucheleweshwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama.
Nigeria, ndilo taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika, pamoja na utajiri wa rasilimali za kutosha yakiwamo mafuta, linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo ukosefu wa usalama ulioenea nchi nzima.
Makundi ya waasi yameendelea kutesa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa, tatizo kuu ni mzozo mkubwa wa kiuchumi na usawa duni unaoendelea.
Kadhalika kuna mgawanyo wa kidini na kikabila nchini humo. Kulingana na makubaliano haya ya kimya kimya, ni kwamba uchaguzi wa urais lazima ubadilishe kila mihula miwili kati ya mgombea kutoka kaskazini, awe Muislamu au kusini, Mkristo.
Lengo la makubaliano hayo ya siri, ni kudumisha uwiano katika nchi yenye makabila zaidi ya 250 tena kuliko na mivutano kati ya jamii za wenyewe kwa wenyewe.
Rais Buhari anayemaliza muda wake, anatoka kaskazini, nafasi ya urais inapaswa kuendeshwa na mgombea kutoka kusini, sasa. Ingawa PDP iliamua kupuuza kugawa maeneo kwa kumteua Abubakar, anayetoka kaskazini mashariki.
Chama tawala APC, kinatoa tiketi kwa Tinubu, anayetoka kusini, alichaguliwa mgombea mwenza.
KAMPENI LALA SALAMA
Mwezi Februari wakati kampeni zikielekea ukingoni joto liliongezeka, huku matusi na shutuma zikipamba moto baina ya wagombea hao wa kiti cha urais.
Mwishoni mwa Septemba mwaka jana, Serikali ya Nigeria, ilitangaza kuanza kwa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais. Wagombea 18 waliingia kwenye mitano ya kampeni ya kuonyesha nia ya kuchukua uongozi.
Kampeni za kichafuana miongoni mwa wagombea zilitamba hivi karibuni, hasa wiki iliyopita, huku baadhi wakikashifiana kuhusu afya, za wagombea urais ambalo ni suala nyeti nchini Nigeria.
Inakumbukwa Rais Buhari alizua gumzo kubwa kwa kutokuonekana ikulu kwa miezi kadhaa wakati wa muhula wake wa kwanza akitibiwa nchini Uingereza maradhi yasiyojulikana.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC), Mahmood Yakubu, anawahakikishia Wa- Nigeria wiki iliyopita kwamba, uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa Jamamosi Februari 25.
Mkuu wa tume huyo, anasema vituo 240 vya kupigia kura havitatumika katika uchaguzi huo, kwa kuwa hakuna aliyevichagua kutokana na ukosefu wa usalama katika maeneo hayo.
Vurugu za watu wanaojitenga na magenge ndio wasiwasi mkubwa kwa Wanigeria wanapopiga kura Februari 25, kwa ajili ya wabunge wapya na mrithi wa Rais Buhari.
Wapigakura wapya wanapojiandikisha nchini Nigeria, wanaruhusiwa kuchagua kituo cha kupigia kura. Watu wengi huchagua eneo la karibu zaidi na wanapoishi kwa sababu idara za usalama hupunguza harakati za usafiri siku ya uchaguzi.
Chanzo: BBC, RFI, VOA, DW










