Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Taifa wa chama hicho, Shani Kitumbua, anasema sera hiyo inapitishwa hivi karibuni na mkutano mkuu na kwamba sasa wanajipanga kuhamasisha umma.
Ni katika mazungumzo na gazeti hili, makao makuu ya chama hicho, Tandika Dar es Salaam, anapofafanua kwa nini wameamua kuwa na sera hiyo."Tumepitisha sera hii baada ya kupata mafunzo yaliyotolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) kuhusu umuhimu wa kuwa nayo.
Wamepata mafunzo mwaka jana na kwamba wameamua kuridhia uwepo wa sera hiyo katika chama chao na kujiona kuwa walichelewa sana kuwa na sera hiyo."Ninaamini kupitia sera hii, idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi kwenye chama chetu itaongezeka, kwa sasa tunakwenda kuhamasisha wanachama watambue umuhimu wake," anasema Kitumbua.
Anataja baadhi ya yaliyomo katika sera hiyo kuwa ni kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishwaji ndani ya chama, ambapo watu wote hasa wanawake na vijana na wenye mahitaji maalum watashirikishwa."Sera hii pia inalenga kuondoa aina zote za ubaguzi na ukatili wa kijinsia ndani ya chama, kuanzisha hatua maalum za kuhakikisha ushiriki wa makundi hayo katika utawala na utendaji, mifumo na michakato ndani ya chama," anasema.Mwenyekiti huyo anaongeza kuwa, sera hiyo inawezesha utekelezaji wa masuala ya jinsia ndani ya chama katika ngazi zote za utawala, lakini kuwa na mwongozo wa wazi wa afua zinazokuza usawa wa kijinsia."Tutaitambulisha rasmi kwa wananchi na wanachama Machi 17, mwaka huu, tutakapozindua mkutano wa hadhara jijini Dodoma ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuondolewa zuio la mikutano ya kisiasa," anasema.
WADAU WAVUTIWAOfisa Habari wa TGNP ambaye ni Mratibu wa Mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi, Monica John, anasema utambulisho wa sera hiyo katika vyama umeanza tangu 2021."TGNP ilitekeleza mradi huu unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa na ngazi za maamuzi kwa kushirikiana na WiLDAF kuanzia Novemba 2021 hadi Septemba mwaka jana," anasema Monica.Anafafanua kuwa, katika mradi huo, TGNP inajikita zaidi kuwajengea uwezo vyama vya siasa ili kuingiza masuala ya jinsia katika sera, mipango na miongozo yao ili kutengeneza mazingira rafiki yatakayowezesha ushiriki mpana na wenye tija wa wanawake, katika siasa ikiwamo kuingia katika ngazi za maamuzi za vyama hivyo."Tanzania kuna vyama 19 vyenye usajili wa kudumu, ambapo kutokana na orodha ya viongozi wa taifa wa vyama hivyo hadi Augosti mwaka 2021, kulikuwa na wanawake wenyeviti watatu pekee sawa na asilimia 15.7.
Vyama vya CCM, SAU, huku ACT- Wazalendo kulikuwa na mwanamke anayekaimu nafasi hiyo, na kwa upande wa makatibu wakuu wanawake walikuwa ni wawili pekee sawa na asilimia 10.5 wa kutoka NCCR- Mageuzi na UDP anasema Monica.
Anasema hali bado si nzuri kwa uongozi wa ngazi za chini pia kwamba kulingana za ripoti TGNP za uwasilishi wa wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi Tanzania ya 2005-2020.
Anatoa mfano kwa mwaka 2019, katika ngazi ya wilaya, wenyeviti wanawake wa vyama vya siasa walikuwa ni wawili kati ya 29 ambayo ni asilimia 7 na makatibu wakuu wanawake walikuwa watano kati ya 30 ikifikia asilimia 17."Ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa na kupunguza pengo hili la uwakilishi mdogo wa wanawake, Februari mwaka jana, TGNP iliratibu vikao vya mashauriano na vyama vya siasa, kupitia Baraza la Vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa vilivyolenga kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya ushindani, katika siasa ili kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye michakato ya uchaguzi," anasema.Aidha, anasema Juni 12 Juni mwaka jana, TGNP iliratibu kikao kingine na uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa, ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya majadiliano vya kuhamasisha vyama vya siasa kuingiza masuala ya jinsia katika sera, mipango na miongozo yao, ili kuridhia masuala ya usawa wa kijinsia kuwa moja ya agenda zao za kisiasa.Anasema kikao hicho kilifuatiwa na mkutano maalumu wa baraza Juni 13 mwaka jana ili kuweka vipaumbele vya mapendekezo yaliyotolewa na baraza hilo kupitia vikao vya mashauriano kuhusu namna bora ya kushughulikia pengo la kijinsia katika sera zao za ndani, miongozo, na taratibu."Pamoja na kupitisha rasimu za sera ya jinsia kwa vyama vya siasa kama hatua muhimu ya kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wanawake kushiriki katika michakato ya kisiasa na kugombea, kwa usawa katika nafasi mbalimbali za uongozi na ngazi za maamuzi," anasema.










