Savio wamaliza 'uteja' kikapu Dar

20Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Savio wamaliza 'uteja' kikapu Dar

KAMA ilivyozoeleka timu za majeshi zimekuwa zikitesa katika mashindano ya ndani na nje ya nchi na hata wachezaji wengi wanaocheza kwenye timu mbalimbali wengi wao wamezalishwa kwenye timu za majeshi.

timu ya kikapu ya savio

Timu za majeshi zimekuwa na sifa ya kufanya vizuri hasa kwenye michezo ya netiboli, kikapu na mpira wa mikono, na mara kwa mara kwenye mashindano ya hapa nchini timu za majeshi zilikuwa zikipokezana kutwaa ubingwa.

Hata hivyo mambo yamekuwa tofauti kwenye mashindano ya mwaka huu, katika kikapu yaliyoandaliwa na Chama cha mchezo huo mkoa wa Dar es Salaam (BD) ambapo timu za majeshi zimeangukia pua na kushindwa kufurukuta mbele ya timu za kiraia.

Katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu za Dar es Salaam pekee, Jeshi iliingiza timu timu nne ikiwemo moja ya wanawake, timu hizo ni pamoja na Jeshi Stars iliyoingiza timu mbili ya wanawake na wanaume, JKT pamoja na timu ya Magereza.

Hata hivyo hakuna timu iliyotwaa ubingwa miongoni mwao na hivyo kutoa ishara ya kupita kwa zama za timu hizo za majeshi.

Ubingwa wa mashindano hayo kwa wanaume na wanawake umekwenda kwenye timu za Savio iliyotwaa makombe yote kwenye mashindano hayo.

Akizungumza mara baada ya mashindano hayo Mwenyekiti wa BD, Mwenze Kabinda, alisema pamoja na changamoto ilizokuwa nazo timu za uraiani lakini safari hii zimewagalagaza wapinzani wao kutokana na maandalizi waliofanya kabla ya mashindano hayajaanza.

Alisema timu nyingi zimekuwa zikishindwa kuzifunga timu za majeshi lakini safari hii wamevunja mwiko na kuvunja na
badala yake kuwanyang'anya ubingwa timu hizo.

"Kwangu nafikiri kuna kitu kimepungua kwenye timu hizi za majeshi..., na kingine kwa mwaka huu timu za uraiani zimeonekana zilifanya maandalizi makubwa na siku zote hiyo ndio siri ya mafanikio," anasema Kabinda.

Alisema ushindi wa kwa timu za uraiani utafungua mlango wa timu nyingine kufanya maandalizi ya uhakika.

"Na pia kwa timu zetu za majeshi ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya mchezo huu lazima zitathmini upya," anaongezea kusema Kabinda.

Aidha, anasema maandalizi ya chama chake kuendesha mashindano hayo kumefanikisha mashindano hayo kuwa yenye upinzani na kuongeza mvuto mwaka huu.

Aliongeza kuwa sasa wanajipanga kuhakikisha mashindano yajayo yanafanyika kwenye kiwango bora zaidi kuliko michuano hii iliyomalizika.