Ni kwa sababu ameondoka kwenye soka la Bongo na kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Denmark, la hasha.
Sababu ni moja tu. Kuwepo kwa mshambuliaji Donald Ngoma.
Kabla ya ujio wa mshambuliaji huyu wa Yanga raia wa Zimbabwe aliyemaliza Ligi Kuu msimu uliomalizika akiwa na magoli 17, Okwi ndiye aliyekuwa gumzo nchini.
Kwa kizazi cha sasa, hakukuwa na mshambuliaji wa kigeni aliyeweza kuwakuna Watanzania kama mchezaji huyo aliyejiunga Simba mwaka 2009 akiwa bado kinda na kuondokea kuwa tishio baadaye.
Vitu alivyofanya aliwateka wadau wote wa soka wakiwemo viongozi, kiasi cha kugombaniwa huku na huko, ndiyo maana hata Simba ilipomuuza kwenda Etoile du Sahel nchini Tunisia, kivuli chake kiliendelea kuwepo nchini.
Ndiyo maana haikuwa ajabu, Yanga ikamrudisha tena nchini msimu wa 2013/14, wakimsajili kutoka SC Villa ya Uganda aliporejea baada ya mgogoro na timu yake hiyo.
Aliichezea timu hiyo kwa msimu mmoja, kabla ya kuvunja mkataba na kuamua kurejea klabu yake ya zamani Simba.
Bado alikuwa mfalme wa soka Bongo na hata Simba ilipomuuza kwa mara ya pili, pengo lake lilionekana wazi si kwa klabu yake hiyo, bali Tanzania nzima hususan Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hakukuwa tena na mshambuliaji msumbufu anayeweza kuwaweka roho juu mabeki.
Mzimu wa Okwi bado uliendelea kuwepo hata alipoondoka Denmark baada ya kuwepo taarifa kuwa huenda angerejea nchini kuichezea Simba.
Ngoma ameonekana kuwa ndiyo dawa iliyozima mzimu wa mashabiki wa soka Tanzania kumuota Okwi kila kukicha.
Uwezo wake mkubwa aliouonyesha kwenye Ligi Kuu msimu wa kwanza tu, tayari wadau wote wa soka wanamuelezea kuwa ni mshambuliaji hatari zaidi nchini kwa sasa.
Viongozi wa klabu kubwa kama za Simba, Yanga na Azam sasa wanakaririwa kusema wanatafuta washambuliaji wenye uwezo kama Ngoma au zaidi na si Okwi tena kama ilivyokuwa zamani.
Awali, klabu zilikuwa zikimtaka Okwi, au mchezaji anayekuwa anakaribiana naye.
Hii inaonyesha kuwa Mzimbabwe huyo ameuzika mzimu wa Okwi uliokuwa ukiwasumbua Watanzania kwa muda mrefu.
Utofauti wa wachezaji hawa ni mdogo tu. Ni kwamba Okwi hatumii nguvu, lakini ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kuwahadaa mabeki, akiwavuruga anavyotaka yeye, huku akiwafuata pale walipo. Hii ilisababisha baadhi kumchezea rafu na wengine hata kukwepa kumfuata.
Alikuwa na uwezo wa kuamua mechi au kuibeba timu kwenye mgongo wake pale inapozidiwa, kwenye mechi za Ligi Kuu au za kimataifa.
Ngoma pia ana sifa kama hizo, lakini yeye anatumia zaidi nguvu na hana kipaji cha kupiga sana chenga, ila analazimisha mabeki akitumia mwili aliojaaliwa.
Msimu huu amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga kutwaa ubingwa, Kombe la FA na hata kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).
Wakati kwenye ligi akifunga magoli 17, kwenye michuano ya kimataifa amepachika mabao matatu mpaka sasa.
Amekuwa mfano kwa wachezaji wa kigeni nchini, lakini pia fundisho kwa viongozi wanaoleta wageni nchini.
Alizaliwa nchini Zimbabwe Septemba 23, 1989 na Yanga ilimsajili kutoka klabu ya FC Platinum ya nchini humo.
----------------------------------------------










