SAMIA RAIS TANZANIA, NJE YA MIPAKA

08Mar 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
SAMIA RAIS TANZANIA, NJE YA MIPAKA
  • Kuingia kazini tu, akaanza kung’ara kitaifa na kimataita ‘kazi ikaendelea’ • Bajeti ya tabasamu; akadhibiti UVIKO-19 • Siasa kaimudu, sifa yake ‘mama hana shida’

NYOTA ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeng’ara mwaka huu akionyesha kuwa ni mwanamke na kiongozi wa shoka nyumbani Tanzania na barani Afrika.

 

Anaanza kuvuta hisia za Waafrika pale anapokabidhiwa jukumu la kuuongoza ujumbe wa pamoja wa Afrika katika mkutano wa jukwaa la uchumi na biashara duniani (WEF) huko Davos Uswizi.

Ni tukio la Januari mwaka huu lililowaleta pamoja wakuu wa nchi, viongozi wa serikali kutoka mataifa mbalimbali na Afrika ikiwa ina sehemu yake.

Awali ilitarajiwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, angekuwa mkuu wa msafara wa wajumbe wa Afrika akisaidiwa na Rais Samia.

Hata hivyo, changamoto za umeme zilimkwamisha Ramaphosa na Mama Samia akaiongoza Afrika.

 

KWANINI KUKUBALIKA?

Rais Samia anakubalika kimataifa kutokana na mwelekeo wake ndani na nje mipaka ya Tanzania. Tangu kuchukua jukumu la kuliongoza taifa,  ametaka maridhiano na uhimilivu wa kisiasa akiondoa katazo au zuio la miaka saba kwa vyama vya upinzani kuwa na hadhara za kisiasa na kuendesha mikutano yoyote kwa maelezo kuwa kinachohitajika ni kuchapakazi.

Kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu ameviruhusu kufanya mikutano na kuendelea na hadhara za kisiasa zilizokuwa zimezuiliwa na uongozi wa John Magufuli.

Rais Samia amefanikisha kuwapo kwa utulivu katika siasa nchini na kutekelezwa kwa maridhiano hayo kumeonekana, mosi, mara kwa mara anakutana na viongozi wa vyama vya siasa, anasikiliza na kufanyia kazi masuala yao.

Anataka utulivu wa kisiasa kama kupitia sheria zinazolalamikiwa kwenye uchaguzi, ameunda kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, akilenga muda wote kuwa na uongozi na kufanyakazi kwa uwazi.

 

MTANGAMANO EAC

Rais Samia ni sura ya Afrika, baada ya kuanza kuongoza nchi, alifanya ziara nchini Kenya na amekuwa mstari wa mbele kutaka kuimarishwa biashara baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akiwa Nairobi ameshiriki kuondoa vizuizi vya kibiashara na nchi za Afrika Mashariki na anakubaliana na viongozi wenzake kuhusu kuwa na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Tanzania kuwa mshiriki anayeuza bidhaa na huduma.

Itakumbukwa kuwa Machi 2018 Umoja wa Afrika ulikubaliana na kutia saini mkataba wa makubaliano ya kuwa na AfCFTA, jukumu lililofanyika jijini Kigali Rwanda.

Rais Samia, anasimamia na anaunga mkono kuwapo kwa Soko Huria la Afrika na anataka ushiriki wa Tanzania katika soko hilo mambo yanayozidi kumpa sifa za kuongoza ujumbe wa Afrika Davos.

Rais Samia ni kiongozi ambaye wakuu wengine wa mataifa ya Afrika hawana mashaka naye na pia ni mtu anayesimamia  sura halisi ya Afrika ikiwa ni utetezi wa demokrasia, uwekezaji, haki za binadamu hasa wanawake, watoto na kuongeza uwiano kwenye masuala ya kijinsia.

Akiwa ofisi ya Makamu wa Rais, amekuwa mstari wa mbele kwenye mijadala ya mabadiliko ya tabianchi hatari inayoinyemelea dunia leo na uwezo mkubwa kwenye masuala ya kitaifa, kimikakati na kimataifa yote yakimpa jukumu la kuisimamia vyema Afrika.Inapozungumzwa Afrika, sura halisi ya bara hilo inaweza isionekana kikamilifu iwapo Rais Samia hataonekana.

Nyota yake inang’ara na anaonyesha kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza na sasa ndiye Rais pekee mwanamama barani Afrika, anayeongoza serikali.

KUINYANYUA TANZANIA

Rais Samia amekuwa shujaa kwenye matumizi ya fedha za UVIKO-19, ambazo ni zaidi ya Shilingi trilioni moja zilizotolewa na IMF kukabiliana na janga la Corona.Hakufanya ajizi Tanzania ilizipokea na kufanya uwekezaji mkubwa si wa kununua vitakasa mikono, wala barakoa kama anavyoeleza Balozi Pindi Chana, akizungumzia uwekezaji kwenye utalii, badala yake amezifanyia kazi kubwa.Ni pamoja na kujenga miundombinu na kutoa huduma zinazoonekana kuanzia madarasa mapya ya msingi na sekondari, kadhalika kuongeza vituo vya afya, ujenzi wa hospitali zanye vifaa tiba na huduma za kisasa.Aidha, kuboresha sekta karibu zote ikiwamo ya utalii kwa kutumia fedha hizo za kusaidia Afrika kutatua changamoto za kiuchumi zinazosababishwa UVIKO-19 na athari za vita vya Ukraine na Urusi.

Kwa mfano Tanzania imeng’ara karibu maeneo mengi mfano kuboresha sekta ya utalii  na kwa kutumia fedha za UVIKO, Wizara ya Mali Asili na Utalii, imekarabati na kuboresha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege hifadhini, kununua vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya shughuli za ulinzi na uhifadhi, kujenga  mageti ya kuingilia na kutoka hifadhini, yote hayo yameongeza idadi ya watalii nchini kwa kipindi kifupi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu watalii wa kigeni 1,175,697 walitembelea Tanzania kati ya Januari na Oktoba mwaka 2022, ikilinganishwa na watalii 716,741 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.

Watalii walioongezeka ni 458,956 sawa na ongezeko la asilimia 64 sababu kubwa ikiwa ni juhudi za kuendeleza utalii baada ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19 na vita.

 

KUKATAA UHASAMA

Rais Samia anagusa mioyo ya Watanzania kwa kuondoa migogoro na uhasama iliyosababisha wanasiasa Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti CHADEMA Bara kuishi uhamishoni.

Aidha, uhasama umemalizika na sasa Lissu amerejea nyumbani, huko wana CHADEMA wakishuhudia mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akirudi nyumbani kwa amani kutoka uhamishoni Canada.

Halikadhalika, Lema amefutiwa kesi zilizokuwa zinamkabili na sasa yuko huru kunguruma majukwaani kuendeleza haraka za demokrasia ya vyama vingi.

Wanawake wanaposherehekea siku yao leo wana kila sababu ya kusisitiza mshikamano na serikali ili kazi bora iendelee.