Miaka 15 iking’ara na makubwa Mfuko wa Wanawake - WFT-T

08Mar 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Miaka 15 iking’ara na makubwa Mfuko wa Wanawake - WFT-T
  • • Kati ya vyombo pekee 44 kimataifa

NI mfuko unaotoa ruzuku kwa ajili ya kuendesha utetezi wa haki za wanawake, wasichana na watoto nchini (Women Fund Tanzania-Trust-WFT-T), ukihesabu mafanikio makubwa tangu ulipoanzishwa miaka 15 iliyopita.

 

Kuna hatua  ya kuwezesha mashirika ya utetezi yafanyayo kazi katika jamii, kuendesha shughuli zake, ambazo zimezaa matunda na kuacha alama muhimu inayoelimisha jamii kuhusu haki za wanawake, wasichana na watoto.

Mwenyekiti wa WFT-T, Prof. Ruth Meena, anasema mafanikio yamewezekana, akifafanua kwamba “ndani ya miaka 15 WFT-T, imejenga taasisi na mifumo imara, inayowezesha mfuko kukua na kuwa endelevu katika nyanja ya rasilimali watu na fedha, pamoja na ajenda yake ya kifeminia.”

.Anatoa mfano, katika muda mfupi, ruzuku za WFT-T ziliongezeka na sasa ni  takribani asilimia 60 za ruzuku zikielekezwa ngazi ya jamii, kuwezesha vikundi vya wanawake kuendeleza vuguvugu la utetezi wa haki zao kiuchumi, kijamii na kisiasa, wakipinga yote yanayoendelea kuwabagua katika kufikia, kutumia na kunufaika na rasilimali za taifa.

Kwa mujibu wa Prof. Ruth ruzuku inayotolewa na WFT-T inawalenga watu wa kawaida na wasiofikiwa kutokana na mifumo ya ubaguzi kwenye utoaji ruzuku na kufikia rasilimali za taifa.

Mwenyekiti huyo, msomi wa sayansi ya siasa na utawala wa umma, anaendelea: “Masharti ya utoaji ruzuku ni rafiki na mfuko unawezesha walioonyesha dhamira na nia ya kuleta mabadiliko na wanapewa uwezo wa kutayarisha andiko.

Anafafanua: “Ruzuku zilizotolewa, zimeonyesha matokeo chanya kijamii na hata kitaifa.”

Mafanikio ya WFT-T yaliwekwa wazi na wadau mbalimbali, kwenye maadhimisho ya miaka 15 yaliyofanyika Dar es Salaam, Februari mwaka huu.

Anataja mfano hai ni shirika la MUMITIE linalotetea haki za wanawake, wasichana na watoto katika ngazi ya jamii, huko Loliondo mkoani Arusha, likiwatetea na kutoa funzo kwa wanaume wanaotenda ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, hata kuangukia mikasa ya jinai.

 

VIONGOZI WANENA

Akizungumza katika sherehe hizo za kuadhimisha miaka 15 ya WFT-T, Mkurugenzi

Mtendaji wa MUMITIE, Rose Njiro, anasema shirika lake lilifanikiwa kuendesha kesi

mahakamani, katika matukio mwanaume aliyeshirikiana na mwenzake kijinsia, kumpiga

mke na kisha kumtupa porini katika mazingira ya kudhuriwa na wanyama. Hukumu ilipotoka, mshtakiwa akaangukia kifungo kirefu jela. Mkurugenzi Mtendaji wa MUMITIE, anasimulia mke huyo aliokolewa na wasamaria wema.

Shirika lingine linalofanya kazi ngazi ya jamii na lilipata ruzuku kwa nyakati tofauti kutoka WFT-T, imetoa matunda yanayoonekana ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), mkoani Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIKI, Janeth Mawiza, anasema wamekuwa wakiendesha kampeni ‘nyumba kwa nyumba’ kuipa jamii uelewa wa rushwa ngono inavyoathiri maendeleo yao kwa ujumla.

Anasema, ni kampeni inayowahusu wanafunzi, ikijulikana kwa jina ‘Safari Salama Kwa Mtoto wa kike Bila Rushwa ya Ngono.”

Mawinza anasema: “Kampeni hii imeanza kushika kasi mkoa wa Dar es Salaam, tumewafikia madereva wa pikipiki na makondakta wa daladala katika maeneo kadhaa ikiwepo Gongolamboto,

Mbagala na Kinondoni.”

Kwa mujibu wa Mawinza, ni kampeni inayochukua hadhi ya kipekee, ikiwezesha kufanyika utafiti wa rushwa ya ngono katika taasisi za vyuo vikuu na athari zake.

Mwenyekiti wa WFT-T, Prof. Ruth Meena, anaeleza kuwa wahanga wa rushwa ya ngono walivunja ukimya, kwa kueleza ukweli wa matukio hayo na athari zake kwa wanafunzi wa kike.

Prof. Meena ambaye ameshafundisha katika vyuo vikuu, anaeleza:“Yamewezesha TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) kuendesha kampeni ya kitaifa ya kupambana na rushwa ya ngono katika sekta ya elimu.”

 

UPEKEE WA MIFUKO

Mwanzilishi Mwenza, Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa WFT-T, Mary Rusimbi, anasema mifuko ya udhamini wa wanawake ni kitu kipya kilichobuniwa duniani miaka ya karibuni, kuwezesha ufadhili katika kazi za utetezi wa haki za wanawake, ndani ya zama za utandawazi.

Anaeleza ubunifu huo ulivyoanza na mfuko wa kimataifa, pia nafasi ya kumdhamini mwanamke, sasa duniani kote kumeshaanzishwa mifuko 44, katika mabara tofauti, ikiwamo WFT-T ya  Tanzania.

Rusimbi anasema, mifuko ya udhamini wa wanawake, inaongozwa na mawazo na inaaminika kupatia ufadhili wa mashirika ya utetezi wa haki za wanawake, wasichana na watoto, ikitajwa ni njia sahihi ya kuleta usawa wa jamii na kutokomeza ukatili wanaofanyiwa mamilioni ya wanawake, wasichana na watoto duniani.

Kihistoria, WFT-T ilianzishwa kutokana na mahitaji ya wanawake na baada ya kufanyika utafiti wa mtandao wa jinsia mwaka 2008, ulionyesha hitaji kubwa la fedha za uendeshaji shughuli za utetezi wa haki za wanawake, wasichana na watoto katika ngazi zote.

Ngazi ya pili ya ruzuku za WFT-T, inaelekezwa kujenga nguvu za pamoja kwa mitandao na majukwaa ya mashirika ya wanawake, yanapounganishwa kufanya kampeni kitaifa kutetea haki za wanawake, wasichana na watoto.

Prof. Meena, mwanazuoni wa haki za binadamu, anasema WFT-T imewezesha kujenga na kuimarisha mitandao, majukwaa na kutoa utetezi wa haki za wanawake, wasichana na watoto, ikijenga vuguvugu la utetezi wa mabadiliko ya mifumo kandamizi katika sheria, sera, mipango na bajeti zisizo na mrengo wa kijinsia.

NGAZI ZA MAFANIKIO

Hapo anatoa mfano wa maeneo, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, kwa kuongozwa na Shirika la Msichana Initiative, iliendesha kesi katika Mahakama Kuu mwaka 2015, ilipobatilisha Kifungu cha 14 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka1971, kinachokinzana na haki kikatiba za mtoto wa kike.

Mahakama ya Rufani mwaka 2019, nayo ilikazia hukumu hiyo, baada ya pingamizi ya serikai kushindwa na sasa anasema, wanaendelea na kampeni ya kitaifa, kulishawishi Bunge lifanye marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.

“Kwa kweli tunahitaji nguvu kubwa ya pamoja kuendesha harakati kuhakikisha Sheria ya Ndoa Mwaka 1971, inafanyiwa marekebisho kuondoa Kifungu Namba 14, kinachoruhusu msichana mwenye umri miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi wake”, anasema Rebecca Gyumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative.

Vilevile, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, ulitoa mchango mkubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, kwa kuchangia kukishawishi chama tawala, kuona umuhimu wa kumteua mwanamke kugombea nafasi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye sasa ni Rais.

La tatu wanalojivunia, katika mafanikio ni WFT-T ilipokutanisha watu 300 kuanzia tarehe 24 hadi 26, mwezi uliopita, wakapanga mikakati ya kuiwezesha Tanzania kufikia usawa kati ya wanawake na wanaume kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mtazamo huo unalenga kabla ya miaka 50 kuanzia sasa, ikiangazia kukoma vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto vitakuwa imetokomezwa.

Anaitaja mikakati hiyo, inajumuisha mashirika yanayotetea haki za wanawake, wasichana na watoto kupata nguvu za pamoja kutafuta fedha za kutekeleza mipango yao, jambo muhimu kwa kila mdau wa maendeleo, ikiwamo serikali na wafadhali.

Pia, hapo kunatajwa shughuli za maendeleo na vyombo vya habari, vinavyounga mkono juhudi za WFT-T, zikilenga kuleta maendeleo ya kweli nchini, kwa kuzingatia usawa kati ya wanawake na wanaume kiuchumi, kisiasa na kijamii.