JUKWAA LA MWANAMKE DK. GRACE MZENGI

08Mar 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
JUKWAA LA MWANAMKE DK. GRACE MZENGI
  • Daktari aliyepata saratani ya matiti Anaeleza alivyopokea vipimo *Inatisha anaifahamu, athari na hatima yake

SARATANI ni tatizo linaloumiza maelfu ya wanawake duniani. Inashambulia matiti, shingo ya kizazi na viungo vingine mwilini. Kama sehemu ya Siku ya Wanawake Duniani, Nipashe inaelezea uzoefu wa wataalamu wa afya ambao wamepata tatizo hilo.

 

Nini hutokea madaktari wabobezi wanapokuwa wagonjwa wa saratani ya matiti? Jibu linatoka kwa Dk. Grace Mzengi na Profesa Julie Makani, katika mahojiano waliyofanya na Mtandao wa Medicopress.

Makala inaanza na Dk. Grace, anayeeleza kuwa ilikuwa Novemba 2007, wakati akiwa na miaka 43, alihisi uvimbe usio na maumivu tena mlaini kwenye titi la kushoto. Aliuguza na kuuchunguza kwa mkono jambo ambalo alikuwa analifanya  tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya udaktari miaka ya 1990. "Sikuwa makini sana, ingawa nilidhani ni mabadiliko ya homoni na huenda ikawa uvimbe tu,’’ anasema Dk. Grace akijibu swali kwanini hakuchukua juhudi za haraka kushughulikia titi mapema. Anasema katika hatua hiyo, kila kitu kilikuwa sawa, lakini  aliendelea kufuatilia uvimbe kuangalia mabadiliko, ukubwa na mitoki chini ya kwapa. Hakukuwa na tatizo akafikiria siyo saratani, mwaka 2008 hakuchukua hatua .

 

OCEAN ROAD

Anasema 2009 anafika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, alifanyiwa upasuaji unaojulikana kama Fine Needle Aspiration (FNA) kuchukua sehemu ya uvimbe kwa uchunguzi.

“ Matokeo yalionyesha kuwa hakuwa na saratani, badala yake kuna  uvimbe usio kansa unaojulikana kama ‘fibroadenoma’. Nilifurahi sana," anasema.

 

UKWELI UNAOSIKITISHA

Kituo cha kazi cha Dk. Grace kilikuwa Chuo cha Afya Mafinga wilayani Mufindi,  alikuwa mkuu wa taasisi na  Septemba 2010, kulikuwa na timu ya madaktari wageni kutoka Ubelgiji ambao walikuwa wakifanya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari wa ndani wilayani Mufindi.

"Inapendekezwa kitaalamu kuondoa uvimbe wa matiti kwa wanawake zaidi ya miaka 40, niliamua kuuondoa kwa kutumia mabingwa wa upasuaji," anasema, akielezea jinsi alivyoendelea kuuguza jeraha lake la upasuaji huku akidumisha usiri wake.

“Katika kipindi hicho nilikuwa na faragha kwa sababu wanafunzi wangu walikuwa likizo. Lakini katika hatua hii, matokeo ya yale ambayo daktari wa upasuaji alipata baada ya kuondoa tishu za matiti yake yalikuwa bado kunifikia.”

Mnamo Oktoba 2010, daktari wa upasuaji aliyemfanyia Dk.Grace operesheni alitoa ripoti ya ugonjwa, akimtumia email na yalionyesha saratani katika hatua ya pili (2), inayojulikana kama ‘adenocarcinoma’ inayosambaa sehemu nyingine za mwili.

 

KUUKUBALI UKWELI

“Ilikuwa baada ya saa za kazi, nilikuwa peke yangu ofisini niliposoma ripoti kutoka kwenye email. Haikuwa rahisi, nilihisi kizunguzungu na kulia. Ilikuwa kana kwamba niliambiwa kwamba “maisha yako yamebakiza miaka michache tu.”

“Kukaa na taarifa hizi kulinitia wasiwasi zaidi. Niliamua kumshirikisha rafiki yangu wa karibu ambaye ni daktari anayefanya kazi Dar es Salaam. Nilimpigia simu nikamjulisha. Nilishangaa jinsi alivyokuwa mtulivu, na akaniambia nisiwe na wasiwasi ikiwa matibabu yataanzishwa mapema nitapona,” anasema Dk. Grace.
Siku iliyofuata, nilimweleza msaidizi wangu kazini habari hizo, akaisoma ripoti hiyo na kuniambia, "katika hatua hii ukipata matibabu utakuwa poa." Kusikia kutoka kwa madaktari wenzangu maneno hayo, nilianza kuona nuru mbele na tumaini jipya.”

"Kwa kifupi, kuwa mtaalamu wa matibabu ambaye anaelewa michakato ya ugonjwa, hakuna tofauti katika hisia juu ya utambuzi. Nilijifunza kutoka kwa wengine ambao walisimulia hadithi zao za saratani, wengi wetu mwanzoni, tumekutana na kuguswa na uchungu kama vile kuelezea hofu na kulia.”

KILICHOFUATA?

 

“Baada ya kugunduliwa, sikuamua ni lini nianze matibabu. Niliendelea kuchelewa, Aprili 2011, nilienda katika Hospitali ya Apollo India. Madaktari walifanya uchunguzi zaidi kabla sijaanza tiba. Huu ulikuwa wakati mwingine mgumu,” anasema Dk. Grace.

"Nilikuwa na wasiwasi wa matokeo ya uchunguzi wa daktari na nini kingetokea hasa kiwango cha ugonjwa huo  na athari za tiba ya saratani ya ‘chemotherapy’"

Lakini mwezi huo huo Dk. Mzengi alianza matibabu ambayo alimaliza Agosti 2011, akisema haikuwa rahisi kuvumilia. Kuna wakati alipata maambukizo na seli nyeupe za damu zilipopungua , lakini alifanya mazoezi na aliendelea kuhimili.

Dokta Grace alipitia matibabu ya upasuaji mwaka 2010, ikifuatiwa na tiba ya saratani ‘chemotheray’ mwaka 2011, kisha tiba ya homoni na radiotherapy.

Kufuatia matibabu hayo, anasema, niliishi kwa miaka 10 bila matatizo ya kiafya. Kwa muda huo nilikuwa najipima matiti kila mwezi, sikuwahi kuhisi mabadiliko yoyote.”

 

SARATANI KUJIRUDIA

Mnamo Mei 2021, Grace alifanyiwa uchunguzi wa kila mwaka wa matibabu ya  uchunguzi wa ‘mammogram’ au altrasound ya matiti na X-ray ya kifua ulifanyika. Matokeo yalikuwa ya kawaida.

Lakini Desemba 2021, wakati wa uchunguzi wa kawaida wa matiti wa kila mwezi, alihisi kuna uvimbe laini usio na maumivu chini ya kovu la awali la titi lile lililokuwa na tatizo.

Mnamo Februari 2022, uvimbe uliondolewa na kuchunguzwa katika idara ya saratani ya Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, ripoti ya ugonjwa ikafichua kwamba saratani hiyo imejirudia.”

“Nilipoteza matumaini kabisa. Usiku huo sikulala usingizi. Niliumia moyoni. Huu ulikuwa wakati mgumu zaidi maishani mwangu. Nilikuwa nikipima kuanza au kutoanza matibabu. Mwishowe, nilianza mzunguko wa kwanza wa chemotherapy. Bado sikufurahishwa na matibabu."

Dokta Grace anaongeza: "Baada ya mzunguko wa kwanza wa chemotherapy, nilikwenda Hospitali ya Agha Khan Dar es Salaam kutafuta maoni zaidi ya kitaalamu. Nilitaka kuondoa shaka kuhusu utambuzi na kuepuka chemotherapy. Shukrani kwa mtaalamu wa saratani ‘oncologist’ na upasuaji ambaye alinishauri. Nilipata tena nguvu za kufanyiwa matibabu hayo.”

Anazidi kueleza: "Nilikuwa na mizunguko sita ya chemotherapy na ‘mastectomy’ kuondoa titi. Baada ya kukamilika kwa matibabu ya kemikali, miezi miwili baadaye nilipata ugonjwa wa moyo. Hili lilikuwa pigo lingine maishani mwangu kwani lazima nihudhurie kliniki za moyo na kutumia dawa kila siku.”

Mtaalamu huyo wa afya anasema, amejifunza kuwa mtu yeyote anaweza kupata saratani ya matiti bila kujali hali yake. Saratani yoyote ni kama vita, ukipata matokeo ya uchunguzi, wakati wa matibabu, baada ya matibabu na hali yote maishani. Mtu anatakiwa kupambana nayo kwa ukali na kulenga kuishinda.

"Uchunguzi wa matiti unapaswa kuhamasishwa ili kugunduliwa mapema. Mfano mzuri ni pale nilipoona uvimbe huo miezi saba baada ya uchunguzi wa kimatibabu hospitalini.”

Anataja somo jingine kuwa huwezi kupigana peke yako, unahitaji watu, wahudumu wa afya, wanafamilia, marafiki, viongozi wa kiroho na jamii inayokuzunguka. Wote wana jukumu la kufanya kufanikisha mchakato wako wa matibabu.

"Kuwaeleza wengine habari hasa ndugu, marafiki, wafanyakazi wenzako na viongozi wa kidini ni muhimu kupunguza unyanyapaa na huzuni.Watu wanapaswa kutafuta habari kutoka kwa vyanzo vya kuaminika. Kuna hadithi na habari potofu katika jamii zetu kuhusu ugonjwa na matibabu.” Anasema Dk. Grace.

 

KUHIMILI MABADILIKO

Anasema: "Kabla ya matibabu nilikuwa na afya njema na mwenye bidii. Baada ya matibabu, nilikuwa na mabadiliko mengi kama upara, rangi ya ngozi na kucha, kujisikia joto kali bila kujali hali ya hewa ya baridi huko Mafinga. Kwa watu walionifahamu, wangeweza kuuliza kilichotokea. Mbali na jamii, nilikuwa nikifundisha wanafunzi wa udaktari. Lazima nihudhurie vipindi vyangu licha ya sura na hisia zangu kubadilika.”

"Haikuwa ngumu kufichua nilichokuwa nikipitia kwa sababu nilitaka wanafunzi wangu wajifunze kuhusu saratani ya matiti kutoka upande wa wataalamu, kinga, uchunguzi, utambuzi na usimamizi. Pia ninahimizi kujichunguza matiti ili kutambua tatizo mapema. Pia nilitumia kurasa zangu za mitandao ya kijamii kufichua na kuongeza ufahamu kila Oktoba,” anasema Dk. Grace.

 

YA KUBORESHWA

Anapendekeza hospitali za umma na binafsi ziwafunze madaktari kuchunguzana kugundua wagonjwa ili watibiwe mapema na wapewe bora.

Aidha, gharama za dawa za saratani ni kubwa, wagonjwa wengi hawazimudu, hivyo kukimbilia tiba za asili, serikali inapaswa kuangalia upya na kuzingatia msamaha wa dawa za saratani.

"Vituo vyote vya saratani lazima vitumie waliougua kansa ya matiti kama washauri kwa wagonjwa wapya waliogunduliwa na na wale wanaotibiwa," anasema.