DEBORA; Shujaa wa kupinga ndoa za utotoni na somo kwa mabinti

09Mar 2023
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
DEBORA; Shujaa wa kupinga ndoa za utotoni na somo kwa mabinti

…NAFANYA hii kazi kwa sababu na mimi niliwahi kupitia changamoto kama hii, ukatili wa kijinsia na katika kuelimisha jamii nimepitia makubwa na nilikuwa mdogo.

Pichani Debora na mwandishi wa makalaa hii, christina mwakangale.

“Hao walikuwa ni ndugu, sio wazazi wangu walitaka niolewe wakati nina miaka 14 nikakata…” Debora, anasiulia kwa hisia huku machozi yakimlenga. 

Akiwa na Nipashe, mwishoni hivi karibuni, anaeleza wazi na kutaka kuacha somo kwenye jamii kwamba, mtoto wa kike alindwe na jamii, familia, akisema wengi wanapitia hayo na kutokuwa na fursa ya kuamua chochote. 

Debora anasimulia hayo kwenye mahojiano na Nipashe, katika kongamano la kuadhimisha miaka 15 ya kuanzishwa Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T). 

Kwa namna Debora anavyojieleza utabaini alivyojasiri na anayeweza kutoa hadithi ya maisha yake hatua kwa hatua. 

Debora, ambaye sasa ni ‘young reporter’ (mtoa taarifa) na mwanaharakati kutoka Mwanza, anafanya kazi na shirika la Kiota Women's Health and Development (KIWOHEDE).

 

SIMULIZI MAISHANI

 

Debora Timoth, alizaliwa mwaka 2000 mkoani Mwanza, miaka saba baadae mama yake mzazi alifariki dunia. Malezi yake yakahamishiwa kwa bibi mzaa baba, ingawa hadi anafikia umri huo, hakuwahi kumtia machoni baba yake mzazi. 

“Mimi nimelelewa na bibi, upande wa  baba, sikuwahi kumuona baba hadi niliposikia siku moja ndugu zake wakipiga simu, wakimwambia wewe mke wako kafariki, unakuja lini? 

“Sikujua alichowajibu, ila nilikuwa tu nawaona ndugu wa baba, yaani baba mdogo na wengine wakija kwa bibi,” anasema Debora. 

Anasema akiwa huko kwa bibi yake alianza shule, ingawa baada ya miaka michache, bibi yake aliyekuwa anamlea alifariki dunia. 

Kwa simulizi yake anasema bibi yake, alipenda kusali na kila alipokwenda kanisani kwa siku za ibada na nyinginezo aliongozana naye. 

“Bibi nafikiri kadri siku zilivyokuwa zinakwenda aliibaini siku zake za kuishi zinapungua, alikuwa anamwambia mchungaji akifa anichukue, anilee,” anasema Debora. 

“Nililelewa na bibi yangu kwa sababu nilikuwa siwajui wazazi wangu wa kunizaa mpaka bibi alipofariki na alikuwa anasali katika kanisa hilo. 

“Bibi alisema kuwa mchungaji aniangalie. mwezi haukupita tangu bibi afariki. Hata hili jina la Timoth, si la baba yangu ni la mchungaji, yaani ndio kachukua majukumu tuseme yote yaani kama baba, kanisomesha hadi hapa nilipo nina miaka 23.” 

Debora anasema baada ya bibi yake kufariki, kikao cha ndugu kikakaa: “Kikawekwa kikao cha kusema kila mtu achukue familia yake nikachukuliwa na baba mdogo, nikawa nakaa miezi michache kwa kila ndugu. 

“Baba mkubwa akanipokea nikajua huyu atakauwa mtu sahihi lakini naye baada ya mwezi akanitafutia kazi za ndani na wakati ni mdogo bado na pesa akawa anachukua. 

“Akaja bosi, akasema jiandae unarudi kwenu na akanipa hela na nauli nafika tu kwa dada akaniambia nina habari njema za mimi kutaka kuolewa na nina miaka 14, na huyo mtu alikuwa ni mtu mzima na nikamwambia siwezi kabisa kufanya hivi, wakanishauri lakini nikakataa kuolewa. 

“Siku baba mkubwa aliniadhibu, usiku ule nikaondoka na kutembea usiku kucha. Namshukuru Mungu nikampata mchungaji akanitetea na ndugu wakawa hawanitaki tena kunisikia,” anasimulia Debora. 

“Mchungaji akanichukua na kunilea mpaka sasa na nikawa nawaza nitapata wapi muda na mimi nije nitoe au nipaze sauti kwa mabinti wenzangu, ili wasaidiwe, nikawa napata semina nafundisha kitu kutoka ndani ya moyo kwa sababu nimepitia hiyo changamoto.” 

Anasema tangu darasa la tatu anaishi kwa mchungaji, na alipomaliza darasa la saba, alianza masomo ya QT hadi kidato cha nne na kushiriki mafunzo ya kompyuta na sasa anafanya kazi kwenye kituo cha kulea watoto ‘day care’ iliyoanzishwa na mchungaji.

 

ALIPO SASA

 

Debora anasema mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia ulianza mwaka 2009 ukiwa na mabinti 30 wakifanya kazi kwenye kata nne. 

“Tunatoa elimu kwenye shule, zahanati majumbani na sehemu za watu mbalimbali. Mradi wa uwezo unawezeshwa kata nne, ikiwamo Buzuruga, Kisesa, Buhongwa na Mhandu. 

“Mradi huu unapambana kutokomeza rushwa ya ngono na kimtamdao Mwanza pia tunajitahidi kutoa elimu na kufanya kazi kwa vitengo mfano kwa kata ya Buzuruga watafanya siku yao na kata zingine pia hivyo hivyo,” anasema Debora. 

“Kikubwa kazi ifanyike kwa wakati, tuna vitu vingi ambavyo tunavipeleka katika jamii na kupambana navyo usiku na mchana hususani kwa wale waandishi wadogo mmoja wapo ni mimi na hapo wapo machampioni na sisi wadogo.” 

Anasema changamoto wanazokutana nazo ni zinazohusu ukatili wa watoto kubakwa. 

“Dereva wa bodaboda katika kata fulani mtoto alikuwa akienda shule na bodaboda akiwa njiani anapita akiendelea na kazi zake akasimamisha bodaboda na kumwambia nikupeleke shule na mtoto akawa amekataa. 

“Lakini kwa kuwa bodaboda ana mbinu nyingi, akamwambia kitu mtoto akakubali na alikuwa darasa la nne na akampakia kwenye pikipiki na badala ampleke shule, akampeleka kwenye boma ambalo halijamaliziwa akamfanyia ukatili wa ubakaji na mtoto alikuwa mdogo kama miaka 10. 

“Na baadae kuna mpitanjia alipita, ambao tunawaita raia wema, alisikia kelele na kwenda moja kwa moja kuangalia ndani ya boma hilo, akakutana na bodaboda anamfanyia hicho kitendo na bahati mbaya tayari alikuwa ametekeleza jambo lake. 

“Wakamkimbiza na kumkamata hiyo kijana na kesi ikatufikia kwetu sisi na kwa bahati nzuri hiyo kata kuna baadhi ya machampioni wakawa wanatoa elimu ya kuhusu mambo ya ukatili. 

“Huwa tunaanzia ngazi za  chini kama serikali za mtaa na pia kufika katika ngazi ya ustawi wa jamii na kufika juu kabisa na mtoto akapewa Pf3 yake, ili apelekwe hospitali na kupima kuthibishwa amebakwa na kuendelea na matibabu na ikatubidi kurudi katika aliyemfanyia kitendo. 

“Baadae kesi ikaenda mahakamani na tukapigwa tarehe na changamoto ikaja kwa baba alikuwa hataki kesi ifike mbali na wakati huo, mama yeye anasema kesi lazima ifike mbali na baba anaonekana alipokea kitu naona kutoka upande wa pili kutaka kesi iishe haraka. 

“Mama akahakikisha na sisi tukasimama upande wa mama na kesi ikaenda na kupangiwa tarehe na mtu wa kundi letu akafika mahakamani na baba akikazana kesi iishe na tukafika mbali, huku chini kabisa ushirkiriano ukawa unapotea”