Fahamu sababu mwanao kumaliza shule pasipo kujua chochote, hata ‘a’

07Mar 2023
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Fahamu sababu mwanao kumaliza shule pasipo kujua chochote, hata ‘a’

ELIMU na lishe bora ni mapacha havitenganishwi, kwa vile mwanafunzi asipopata chakula asubuhi na mchana hawezi kuelewa masomo darasani. Kwa maelezo kuwa ubongo hautapokea anachofundishwa.

Wakili Ibrahim Mohamed, akiwaelezea wanafunzi wa Shule ya Msingi Olpopongi iliyoko Kiteto mkoani Manyara umuhimu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na ulazima wa chakula shuleni. PICHA: JALIWASON JASSON

Ni ukweli huo unaowahamasisha wazazi, walezi na walimu kutetea upatikanaji wa chakula shuleni,

Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Simon Mumbee, anasema.

Anaongeza kuwa chakula kina manufaa mengi, mosi kukua kimwili na kiakili kwa mwanafunzi, kuongezeka kimo na ubongo kufanyakazi.

Mumbee anasema wanafunzi wakikosa chakula bora hudumaa na hivyo wazazi wakichezea lishe kwenye umri wa miaka minne mpaka minane ambao wengi wao wanakuwa darasa la awali hadi la pili au la tatu wanaweza kusababisha ukuaji duni.

"Mtoto akikaa siku nzima bila kula anaathirika kiafya na uwezo wa kujifunza unaondoka,"anasema Mumbee.

Aidha, njaa huchangia utoro, ni chanzo cha kupiga miayo na usikivu hafifu darasani, anafafanua zaidi.

Kadhalika, kukiwapo na chakula mahudhurio huongezeka na wengi huipenda shule wakiwa na uhakika wa kula, anasema Ofisa Elimu na kwamba wanasimamia maelekezo ya waraka wa mwaka 2016 unaowataka wazazi au walezi kutoa chakula shuleni.

Mumbee anasema kwa mujibu wa waraka, wazazi na walezi wanatakiwa kubeba jukumu hilo na walimu kufundisha na ili kupata ufanisi, watendaji wa kata na walimu wamepewa maelekezo na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati na kwamba kila baada ya miezi mitatu kuna utaratibu wa kutathmini wanafunzi wangapi wanapata chakula shuleni na shule zote zinatoa chakula.

“Kila mzazi au mlezi anatakiwa kumchangia kilo 30 za mahindi kwa mhula, wanatakiwa kuzingatia hilo,” anasema Ofisa Elimu Maalum  Halmashauri ya Babati, Eveta Kavishe.

Anaongeza kuwa kati ya shule za msingi 148 za halmashauri hiyo, zinazotoa chakula cha mchana ni 142 na wamefanikiwa kwa sababu ya kulifanya suala hilo kuwa ajenda maalumu kwenye vikao vya Baraza la Madiwani.

Mwalimu wa awali kutoka Shule ya Msingi Maisaka wilayani humo, Raeikiel Mkanza, anasema madarasa ya awali yanapopata chakula kinaongeza furaha na ari ya kusoma na ufaulu, tena hakuna kusinzia darasani.

“Wanaweza kutamka  herufi kwa ufasaha hivyo nafasi ya chakula ni muhimu, akiongeza kuwa watoto wengi wa awali hawapati chakula usiku na asubuhi wanaamshwa kwenda shule wakiwa na njaa, akiwaasa wana familia kuwapa chakula asubuhi ili kufanikisha ufundishaji na ujifunzaji.

Mwalimu Rehema Mwendo wa Kituo cha kulelea watoto cha kutwa cha Enhakore kilichoko Halmashauri ya Mji wa Babati anasema chakula shuleni ni muhimu tena chenye virutubisho vyote kwa kuwa watoto wanatakiwa wapate lishe bora.

Rehema anasema katika kituo chake anawapa uji saa nne asubuhi na chakula cha mchana saa 6:30 mchana na watoto anawapa matunda na mboga hivyo kila siku yanatolewa aina tofauti za matunda.

Anaeleza kuwa kula shuleni ni muhimu zaidi kwa kuwa chakula kinakuwa na usalama na tofauti na akirudi nyumbani anaweza asikute chakula maana wazazi wanakwenda kwenye shughuli zao.

ATHARI KUKIKOSA 

Ofisa Elimu Mkoa wa Manyara, Halfani Masukira, anasema mwanafunzi anahudhuria shule siku 194 kwa mwaka, hivyo kila mlo mmoja kwa usiku, inamaanisha miaka saba ya msingi itakapomalizika anakuwa amekosa chakula miaka 3.6 mpaka anamalize shule.

“Ndiyo maana siku hizi wanafunzi wanamaliza masomo hawaeleweki ni kwa sababu wengi wao walikuwa wanashinda njaa hivyo akili zimedumaa.

Udumavu mwingine tunausababisha wenyewe wazazi na walezi, ukichangia chakula shuleni ni sawa amehamisha kutoka nyumbani kwenda shule ili mtoto ale mchana,"anasema Masukira

Januari Dalushi ni Ofisa Lishe wa Manyara anayenukuu utafiti wa mwaka 2015/2016, akisema  ulibaini watoto wanapokelewa shuleni wakiwa na athari za kilishe.

Ananukuu utafiti kuwa asilimia 58 ya watoto chini ya miaka mitano walikuwa na upungufu wa damu na kwamba wa darasa la awali na la kwanza madhara wanayoweza kuyapata ni kinga kuwa chini hivyo ni rahisi kupata magonjwa kila mara na matokeo yake ni utoro.

Madhara mengine ni kukosa nguvu na uchovu wa mara kwa mara, kukosa usikivu darasani na vifo vinakuwa vingi katika umri huo.

"Tunaweza kuwadahili wanafunzi wengi wa darasa la awali na la kwanza ila tukawapoteza tusipowapa chakula," anasema Dalushi.

Mtaalamu huyo wa lishe anaeleza kuwa watoto hao umri huo ni wa msingi katika ukuaji ambapo anasema katika ukuaji wanaangalia awamu mbili ya kwanza ni miaka sifuri hadi miaka miwili na awamu ya pili ni kuanzia miaka mitano hadi miaka 18.

"Mtoto akishinda bila kula tumbo lake linakuwa wazi hivyo tunamwathiri ukuaji na usikivu darasani,"anaeleza.

Kiongozi huyo wa lishe anasema bado kuna desturi ya ulaji wa mazoea ila bado wanaratibu masuala ya chakula kwenye kamati za usimamizi za vijiji na Miata.

Anafafanua kuwa chakula kinachangwa ila wasimamizi ni lazima wahakikishe kina makundi matano ili kiwe bora, kiwe safi na virutubisho.

 

Mshauri wa awali wa malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kutoka Shirika la Children Incrossfire (CIC) Davis Gisuka, anasema ubongo ili uweze kukua kikamilifu ni lazima upate chakula bora ubongo, bila hivyo unadumaa.

Gisuka anasema kipindi kizuri cha kumwandaa mtoto ni kuanzia miaka 0  hadi nane na kwamba utafiti unaonyesha ukuaji wa ubongo na utendaji wa akili unakua kwa kasi mtoto akiwa na miaka mitatu mpaka minne ambapo ubongo unakua kwa asilimia 70 hadi asilimia 80 ya mtu mzima.

"Asipopata chakula mtoto atadumaa na hatasoma vizuri tutaishia kusema mtoto hana uwezo darasani kumbe alidumaa kwasababu ya kukosa chakula,"anasema Gisuka.

 

Analeza kushangazwa na wanafunzi wa darasa la awali kupewa chakula saa 5:00 asubuhi wakati wanataka kurudi nyumbani badala ya kupewa asubuhi saa 3:00 ili wawe makini darasani kumsikiliza mwalimu.

Gisuka anasema wanasisitiza siku 1,000 mama ale vizuri ili mtoto akizaliwa akue kikamilifu na katika  kipindi hicho cha siku 1, 000 ndicho cha kumtengeneza binadamu bora.

Mtaalamu huyo anasema kuchangia chakula shuleni hakuna hasara ni sawa na kuhamisha chakula nyumbani na kupeleka shuleni, akiongeza kuwa kama tumbo halina chochote hata akili haina chochote pia.

Anafafanua kuwa chakula ndicho kinamjenga mtoto na kuna sababu za wazazi kuwekeza katika chakula maana wakipewa chakula kitafanikisha wanafunzi wa awali na darasa la kwanza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).

Mratibu wa lishe shuleni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Grace Shileringo, akizungumza kwenye kikao cha mapitio ya utekelezaji wa programu jumuishi ya taifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) anasema lishe shuleni ifuate muongozo wa lishe shuleni wa mwaka 2016 ili kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia.

Anashauri mashamba ya shule yatumike kuzalisha chakula cha wanafunzi walime mboga, matunda na  nafaka.

Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) ya 2021/22- 2025/26 lishe shuleni ni matokeo ya juhudi za wadau zinazotokana na ubunifu.

PJT-MMMAM inaeleza kuwa walimu au uongozi wa shule kuchangisha chakula kutoka kwa wazazi au walezi au ni kutokana na michango ya wasamaria wema.

Hata hivyo lishe hiyo haifikii kiwango bora cha vyakula mchanganyiko ambapo wadau kadhaa wanaohojiwa wanaonyesha kuwa uji wa nafaka pekee ndiyo unaotolewa.

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Dk. Charles Msonde, akizungumza na wadau wa elimu mkoani Manyara mapema mwaka huu, anasema chakula shuleni siyo hiari ni lazima na kuhimiza utekelezaji.