Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa siku kadhaa Muhimbili, hospitali tatu za manispaa ya Dar es Salaam za Mwananyamala (Kinondoni), Amana (Ilala), Temeke na nyingine za mikoani, umebaini kuwa bado kuna changamoto nyingi zinazowakuta wajawazito.
Changamoto hizo ni ukubwa wa mahitaji kulinganisha na uwezo wa wodi (hospitali) na pia ukosefu wa vifaa tiba kama pamba, gloves, nyembe na hata dawa za vichocheo vya uchungu.
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu zilizoanza Agosti 21 hadi Oktoba 24, mwaka jana, Rais Magufuli aliahidi kushughulikia changamoto za huduma za afya huku akiahidi kuwafuta kazi mara moja watu atakaowapa dhamana ya kusimamia eneo hilo na kushindwa kuboresha huduma.
Kadhalika, aliyekuwa mgombea mwenza ambaye sasa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliahidi mara kadhaa kuwa serikali ya awamu ya tano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) italivalia njuga tatizo la huduma za afya kwa kina mama wajawazito, na kwamba yeye, akiwa mama mwenye kutambua adha zilizopo, atahakikisha kuwa serikali inashughulikia eneo hilo kwa ukamilifu.
MUHIMBILI MAMBO SAFI
Baada ya Rais Magufuli kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili na kutoridhishwa na hali aliyoikuta, hasa alipowaona kina mama wengi wakilala sakafuni kwa kukosa vitanda, alitoa maagizo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuamuru jengo la ghorofa tatu lililokuwa likitumiwa na wafanyakazi 70 wanaoshughulikia afya ya mama na mtoto, lijazwe vitanda ndani ya siku mbili na kubadilishwa matumizi ili litumiwe kama wodi ya wajawazito.
Siku mbili baadaye, wafanyakazi wote walihamishwa kutoka kwenye jengo hilo na kujazwa vitanda kabla ya kuanza kutumiwa na wajawazito.
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa hadi kufikia jana, kina mama wajawazito wanaofika Muhimbili wameimarishiwa huduma kwa kiasi kikubwa kwa sababu kuna vitanda vya kutosha na walau dawa na vifaa tiba hupatikana, tofauti na ilivyokuwa hapo kabla.
“Hii siyo mara yangu ya kwanza kuja kujifungua hapa (Muhimbili). Mara ya mwisho niliishia kulala chini baada ya kitanda kukosekana na wengi walikumbana na hali hiyo,” alisema mmoja wa kina mama waliozungumza na Nipashe hospitalini Muhimbili jana.
“Hivi sasa kuna mabadiliko makubwa. Vitanda vipo vya kutosha na dawa na vifaa vingi hupatikana hapa."
Akizungumza na Nipashe, Afisa habari wa Hospitali hiyo, Neema Mwangomo alisema hadi kufikia jana, walikuwa na vitanda 412 kwa ajili ya wajawazito na kwamba, hivi sasa wanaendelea na kazi ya kuboresha miundombinu ili waongeze vitanda vingine na kufikia uwezo wa kulaza vitandani wajawazito 635.
“Kuna mengi yanafanyika hivi sasa kwa nia ya kuboresha zaidi huduma kwa kina mama wajawazito,” alisema Neema jana.
MWANANYAMALA, TEMEKE
Tofauti na Muhimbili ambako hivi sasa kuna nafuu kubwa, hali katika hospitali za Sinza Palestina, Mwananyamala, Amana na Temeke jijini Dar es Salaam bado siyo ya kuridhisha.
Nipashe imebaini kuwa baadhi ya changamoto kubwa katika hospitali hizo ni pamoja na ukosefu wa vifaa tiba, dawa na pia miundombinu isiyokuwa rafiki na kusababisha baadhi ya kina mama kulala chini.
Imebainika kuwa chanzo cha changamoto zote hizo ni pamoja na kuwapo kwa ufinyu wa bajeti na pia ucheleweshwaji wa fedha kutoka serikali kuu.
Flora Emmanuel aliyekutwa katika Hospitali ya Palestina, alisema anamuomba Mungu ajifungue salama licha ya changamoto zilizopo, na ikibidi asizidiwe na kuwahishwa Mwananyamala ambako changamoto ni nyingi zaidi kulinganisha na Palestina.
“Hapa (Sinza–Palestina) kuna changamoto nyingi tu, lakini siyo sawa na Mwananyamala ambako huko ndiyo balaa. Tatizo la hapa ni ukosefu wa vifaa," alisema Flora.
"Kuna mazingira mazuri lakini bado wajawazito tunaambiwa tubebe vifaa vya kujifungulia kama dripu, gloves, sindano, nyembe, kibanio cha kitovu na pamba.”
Mmoja wa kina mama waliokutwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuomba jina lake lihifadhiwe alisema hali imekuwa ngumu kwa wajawazito kwa sababu wanawekwa wawili katika kitanda kimoja huku wengine wakilala chini, hali aliyoielezea kuwa ni hatari kiafya kwao na watoto wanaotarajia kujifungua.
“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kujionea mwenyewe mateso wanayopata wajawazito Muhimbili… sasa namuomba afanye ziara kama ile katika hospitali nyingine kama hii ya Mwananyamala. Kwakweli hali ni mbaya sana,” alisema mama huyo.
Aidha, mama huyo alisema licha ya serikali kusisitiza mara kadhaa kuwa wajawazito wasiambiwe kujinunulia vifa vya kujifungulia kama pamba, nyembe na gloves, hali iko tofauti kwani vitu vyote hutakiwa wavinunue wenyewe, ikiwemo mipira ya kulalia wakati wa kujifungua.
Aidha, matatizo kama hayo yamekutwa pia na mwandishi katika hospitali za Amana na Temeke ambako wajawazito hukumbana na changamoto nyingi zikiwamo za ukosefu wa dawa na vifaa tiba.
Mkurugenzi wa Wauguzi na Ubora katika Hospitali ya Sinza-Palestina, Agness Mtawa, alisema miongoni mwa changamoto zilizopo ni ukosefu wa vifaa vinavyotosha kwa idadi kulingana na mahitaji na pia vinavyodumu kwa muda mrefu.
Alitolea mfano wa mashine za kupima shinikizo la moyo (BP), ambazo huletewa kutoka Bohari ya Dawa (MSD), kuwa hazina ubora unaotakiwa kwa kuwa huharibika mapema na hivyo kuwaongezea changamoto katika kuwahudumia wagonjwa.
Alisema tatizo la ukosefu wa vifaa na miundombinu inayokidhi mahitaji ndilo linalochangia baadhi ya kina mama kulala chini kwa sababu hata wanapokuwa na vitanda, bado wanakosa pa kuviweka kwa sababu eneo la wodi halitoshi.
“Kwa mfano, hivi sasa tuna vitanda 50 na magodoro 40 katika stoo yetu. Tatizo ni eneo la kuviweka. Tunapenda kila tunayemhudumia awe kitandani lakini inashindikana kutokana na changamoto hii,” alisema na kuongeza:
“Jiulize, ni muuguzi au daktari gani anayependa kuinama wakati anamhudumia mgonjwa aliyelala chini? Hayupo.
"Hata kitaaluma hairuhusiwi lakini tunafanya hivyo kwa sababu hatuwezi kuwaacha.”
Mtawa alisema wingi wa wagonjwa na uwezo wao katika kuwahudumia ni chanzo kingine cha huduma duni, akitolea mfano wodi 37 yenye vitanda 33 lakini wagonjwa waliokutwa Alhamisi iliyopita walikuwa 63.
“Pia wodi namba 33 vitanda vilivyopo ni 33 huku wagonjwa wakiwa ni 56… hizi changamoto ni nyingi.”
Mtawa alisema wanaendelea kupambana na kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kadri ya uwezo wao.
“Haiwezekani mjamzito afike mapokezi, yupo kwenye hatua ya mwisho ya kujifungua halafu arudishwe kwa sababu ya kukosaa kitanda… tutamuhudumia tu.”
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Ezra Ngereza, alisema idadi ya wajawazito kulinganisha na uwezo uliopo wa kuwahudumia ni changamoto mojawapo kubwa zaidi, akitolea mfano katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mwananyamala ambayo uwezo wake ni kuhudumia wajawazito 64 kwa siku huku Sinza-Palestina ikiwa ni kuwahudumia kati ya wajawazito 90 hadi 100.
Hata hivyo, wajawazito huwa wengi wodini kwa sababu kwa wastani, kila siku hupokewa kina mama kati ya 30 hadi 40 katika Hospitali ya Mwananyamala na 70 hadi 90 katika Hospitali ya Sinza-Palestina.
Alikiri kwamba katika hospitali za Mwananyamala na Sinza-Palestina, kina mama hulazimika kulala wawili na wengine kulala chini kwa sababu wajawazito huwa wengi kuliko uwezo uliopo, jambo linalochangia pia kuwapo kwa tatizo la ukosefu wa dawa na vifaa tiba.
“Pia kuna changamoto ya ucheleweshwaji wa vifaa tiba na dawa kutoka MSD na ucheleweshwaji wa fedha za bajeti,” alisema Ngereza na kuongeza kuwa wakati mwingine, kiasi cha fedha kinachotolewa huwa hakiendani na mahitaji.
Akitoa mfano, alisema bajeti ya uendeshaji wa Hospitali ya Mwananyamala ya mwaka 2015/16 ilikuwa ni zaidi ya Sh. bilioni 11.5, lakini fedha zilizotengwa kulingana na ukomo wa bajeti ilikuwa ni Sh. bilioni 2.7, hivyo upungufu ukiwa ni zaidi ya Sh. bilioni 8.
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Watoto wa Manispaa ya Temeke, Catherine Mbeyela, alisema uwezo wa wodi ya wazazi hospitali ya Temeke ni kuhudumia wajawazito 20 kwa siku lakini wastani wa wajawazito wanaopokelewa kwao kwa siku ni kati ya 40 hadi 60.
“Muuguzi wa cheti anatakiwa ahudumie kina mama kati ya sita hadi nane, na mwenye advance na degree anatakiwa ahudumie kina mama nane hadi kumi… lakini katika hospitali zetu, mkunga mmoja hujikuta akihudumia kina mama 20 hadi 25 kwa siku,” alisema Mbeyela.
Kuhusu vitendea kazi, alisema huwa havikidhi mahitaji ya hospitali hiyo ya Temeke na hivyo kuwa changamoto kubwa kwao.
“Kwakweli bajeti haitoshelezi mahitaji.”
BOMBO - TANGA
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, kuna changamoto kadhaa zinazosababisha hali kuwa ngumu kwa wajawazito, kubwa ikiwa ni ya ukosefu wa watumishi kulingana na mahitaji.
Nipashe imebaini kuwa hivi sasa, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama katika hospitali ya Bombo ni mmoja tu huku pia kukiwa na upungufu wa wauguzi wakunga zaidi ya 40.
Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo, Batrice Rimoyi, alisema kuwa kutokana na uhaba wa watumishi na hasa wauguzi, hivi sasa kila muuguzi mkunga mmoja huhudumia wastani wa kina mama 24 kwa siku.
Rimoyi alisema kuna wajawazito zaidi ya 48 wanaofika kwa ajili ya kujifungua kila siku na kwa kila zamu huwapo wauguzi wawili tu, tofauti na inavyopaswa kuwa ambapo muuguzi mkunga mmoja hutakiwa kumhudumia mama mmoja.
Anasema kimsingi hali hiyo inawaweka katika wakati mgumu kiutendaji hasa kwa kuzingatia kuwa kuna baadhi ya kina mama hupaswa kujifungua kwa njia ya upasuaji.
“Hali hiyo ndiyo tunajikuta tunapata lawama kwa sababu muuguzi huyu huyu amwangalie mama anayetaka kujifungua, kumpima na kadhalika… wakati huo huo kuna aliyetoka kwenye upasuaji analia maumivu na bado kuna mwingine amejifungua kawaida lakini kuna matatizo na anahitaji kuhudumiwa. Hali ni ngumu lakini tunaendelea kujitahidi kadri ya uwezo wetu,” alisema Rimoyi.
Mmoja wa kina mama waliokutwa hospitalini hapo kufuata huduma, aliiambia Nipashe kuwa serikali inapaswa kuiangalia hospitali hiyo ya rufaa kwa jicho la huruma kwa sababu inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za ukosefu wa vifaa, dawa na wauguzi wanaokidhi mahitaji.
“Huko tunakotoka kuna vituo vya afya pia, lakini tumepewa masharti kwamba mimba ya kwanza lazima uje huku Bombo au kama wewe mimba zako ni za upasuaji unalazimika kuja huku," alisema mama huyo.
"Sasa daktari ni mmoja tu na wauguzi ni wachache. Hili serikali ya Rais Magufuli iliangalie kwa sababu hali ni mbaya.”
Sarah John, aliyefika hospitali ya Bombo akitokea Mkinga, aliiambia Nipashe kuwa tatizo la vifaa vya kujifungulia ni kama halipo kwa sababu wamekuwa wakipatiwa karibu kila kitu bure kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ambao unaendesha mradi uitwao KFW chini ya ufadhili wa serikali ya Ujerumani.
“Tatizo huwa ni watumishi na uhaba wa vitanda… watu wanalala hadi watatu kwenye kitanda kimoja. Hili ni tatizo kubwa,” alisema Sarah na kuongeza:
“Hebu fikiria… mnalala watatu kitanda kimoja mkiwa na watoto wenu. Labda wale waliofanyiwa upasuaji ambao siku ya kwanza hulala peke yao, lakini kesho yake wanaletwa wengine. Ni hatari sana kiafya.”
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita, alikiri kuwapo kwa changamoto hizo na kusema kuwa katika kukabiliana nazo, wanaendelea kuboresha hospitali za wilaya na vituo vya afya ili kuhakikisha kuwa wanapunguza mrundikano wa wagonjwa Bombo.
Aidha, Mahita alisema wameanza kufanyia ukarabati jengo la wazazi na hivyo msongamano umeongezeka katika wodi inayotumika sasa.
“Kwa hapa Bombo kweli kuna msongamano wodini na sababu kubwa ni kazi ya ukarabati unaoendelea kwenye ile wodi nyingine (ya wazazi)," alisema Dk. Mahita.
"Lakini msongamano huu pia unatokana na wagonjwa wengi kukimbilia huku hata kwa baadhi ya matatizo ambayo yangeweza kumalizwa kwenye vituo vya afya wilayani.
"Sasa tunachofanya ni kuhakikisha tunaboresha hali ya upatikanaji wa huduma huko ili kupunguza hii hali ya mrundikano huku.”
Dk. Mahita alisema kuna changamoto ya kutopatikana kwa dawa na vifaa tiba vya kutosha na kwa wakati kutoka MSD licha ya kwamba kumefunguliwa kituo cha kanda (cha msd) mkoani Arusha.
“Tunakarabati jengo letu ili na sisi tufunguliwe duka letu la dawa la MSD kama lile lililofunguliwa pale Muhimbili, lengo likiwa ni kukabialiana na changamoto za upatikanaji wa dawa.“
Dk. Mahita alisema tatizo jingine kubwa ni ufinyu wa bajeti na uhaba wa watumishi.
HOSPITALI DODOMA
Hali si nzuri pia kwa wajawazito wanaofika kwenye hospitali ya mkoa wa Dodoma.
Hata hivyo, tatizo kubwa linalotajwa na wengi ni uhaba wa vitanda na pia namna baadhi ya wauguzi wanavyofanya kazi zao kwani hukosa huruma na utu.
Mmoja wa kina mama waliozungumza na Nipashe alisema mbali na changamoto nyingi, lipo pia tatizo la baadhi ya wauguzi kutowajali wagonjwa, akitolea mfano yeye kwa kusema kuwa alijifungua peke yake bila msaada wowote akiwa kwenye wodi ya wazazi licha ya kupiga sana kelele na kuomba msaada wa wauguzi wakati uchungu ulipomzidia.
“Ilikuwa usiku, majira ya saa sita… niliwaomba sana wauguzi waje kunisaidia lakini wakanikatalia na kuendelea na mambo yao kwa maelezo kuwa hawana gloves," alisema.
Kuhusu suala la dawa na vifaa tiba, mama huyo alisema karibu vyote hupatikana bure hospitalini hapo, ijapokuwa yeye alikataliwa kusaidiwa kujifungua kwa madai kwamba hakuna gloves.
“Wako pia wanaotumia lugha za matusi… serikali imejitahidi sana hapa katika suala la dawa na vifaa, ila baadhi ya wauguzi ndiyo tatizo.”
Asia Iddi alisema ni mara yake ya kwanza kujifungua na tatizo kubwa aliloliona ni ukosefu wa vitanda ambao huwalazimu kina mama kulala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja.
“Pamoja na kulala watu wengi katika kitanda kimoja lakini pia kuna tatizo kubwa la ukosefu wa vyandarua. Matokeo yake wazazi na watoto hung’atwa na mbu nah ii ni hatari kwa malaria,” alisema Asia.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Nasoro Mzee, alisema kuwa uwezo wa wodi ya wajawazito ni mdogo ukilinganisha na idadi ya kina mama wanaopokewa kwa siku na hiyo ndiyo changamoto kubwa kwao.
Alisema kuwa katika wodi hiyo ya wazazi, kuna vitanda 15 lakini huhudumia wastani wa kina mama 40 kila siku.
“Kwa idadi hiyo ya vitanda katika wodi, unaona kabisa ni namna gani haikidhi mahitaji. Wakati mwingine tunahudumia hadi wajawazito 50 ndani ya saa 24. Hii ni changamoto kubwa inayosababisha kuibuka kwa malalamiko mengine.”
Aliongeza kuwa hivi sasa wanachofanya ni kufanya jitihada za kuona namna gani watapunguza msongamano huo, ikiwamo kuvijengea uwezo vituo vya afya.
Alisema pia waliwahi kusumbuliwa na tatizo la dawa katika hospitali hiyo ambalo hutokana na kuwapo kwa deni kubwa la MSD.
“Lakini hivi sasa tumelimaliza na kwa wastani dawa na vifaa tiba siyo tatizo,”alisema Dk. Mzee, akiongeza kuwa huwa na utaratibu pia wa kutumia sanduku la maoni kupokea malalamiko na kuchukua hatua dhidi ya wauguzi wasiozingatia miiko ya kazi yao.
HOSPITALI NJOMBE
Changamoto kwa wajawazito mkoani Njombe ambao hupata huduma katika Hospitali ya Kibena mjini humo haitofautiani na maeneo mengine mengi, mojawapo ikiwa ni ile ya ukosefu wa vifaa na vitanda vinavyokidhi mahitaji na hivyo baadhi ya kina mama kujikuta wakilala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja na wengine kulala chini.
“Binafsi nimepokewa vizuri na huduma siyo mbaya. Tatizo ni ukosefu wa vifaa na pia vitanda… hili ni tatizo kubwa,” alisema mmoja wa kina mama waliokutwa katika hospitali ya Njombe ambayo bado haijawa na hadhi ya rufaa ya mkoa.
SEKOU TOURE-MWANZA
Katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, hali ya utoaji wa huduma ya afya ya uzazi kwa kina mama wajawazito imekuwa pia ya kusuasua.
Nipashe imebaini kuwapo kwa msongamano mkubwa wa wajawazito, huku baadhi yao wakilala wawili hadi watatu kwenye kitanda kimoja.
Mmoja wa kina mama waliokutwa hospitalini hapo kwa ajili ya maandalizi ya kujifungua (jina linahifadhiwa), alisema hali bado siyo nzuri ijapokuwa wauguzi wamepunguza maneno ya kebehi kwa wagonjwa.
“Hivi sasa kuna nafuu kubwa katika upatikanaji wa vifaa vya kujifungulia… kwakweli huwa tunavipata bure. Tatizo lipo kwenye vitanda na baadhi ya dawa,” alisema mama huyo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Onesmo Rwakyendela, akitolea ufafanuzi kuhusu na huduma hospitalini hapo, alisema changamoto iliyopo ni wingi wa wajawazito kulinganisha na uwezo.
Alisema kwa wastani hupokea wajawazito kati ya 30 hadi 40 kila siku na hivyo kusababisha mrundikano.
Aidha, Dk. Rwakyendela alisema bado hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha kwa ajili ya kununulia vifaa tiba pamoja na dawa ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa mama wajawazito.
Hivi karibuni, serikali ilifungua duka la dawa la MSD hali ambayo inaonekana kuwasaidia wagonjwa wengi kununua dawa katika duka hilo.
SHINYANGA
Mkoani Shinyanga kuna nafuu kubwa kwa kina mama wajawazito.
Baadhi ya kina mama wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo wameipongeza serikali na kutaka iendelee na kasi iliyoanza nayo ya kuboresha huduma kwenye hospitali hiyo.
“Wauguzi wamekuwa na kauli nzuri sana hivi sasa. Uhaba wa vifaa na dawa umepungua kwa sababu baadhi hupatikana hapa hospitali,” alisema mmoja wa kina mama waliokutwa hospitalini hapo na kujitambulisha kwa jina la Semeni Daudi.
“Kabla ya Magufuli kulikuwa na unyanyasaji mkubwa. Walikuwa wakitulazimisha kutuuzia hata baadhi ya vifaa ambavyo wenyewe tayari tunavyo kama mabeseni ya kuogesehea mtoto… lakini hivi sasa kuna mabadiliko makubwa na wapo wanaotoa huduma huku wakitupa maneno mazuri ya faraja. Inatia moyo kwakweli,” alisema Semeni.
Mama mwingine aliongeza kuwa hali sasa inaelekea kuwa nzuri hospitalini hapo na kwamba, tatizo pekee ni uhaba wa vitanda ambao huwalazimu wengi wao kulala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Ntuli Kapologwe, alisema suala hilo la uhaba wa vitanda linafanyiwa kazi na kwamba hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa jengo la wazazi ili kumaliza msongamano wa uliopo sasa katika wodi yao ambayo hupokea wajawazito 15 hadi 20 kwa siku.
Kuhusu dawa, Kapologwe alisema hivi sasa upatikanaji wake ni wa asilimia 95 na wao wanatekeleza sera ya afya ya mwaka 2007 inayowataka kutoa huduma kwa wajawazito bure huku muuguzi au mkunga anayebainika kumuomba pesa mgonjwa huchukuliwa hatua kali za kisheria bila kuoneana haya.
KILIMANJARO
Katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, hali siyo nzuri pia kwa sababu wajawazito hulala zaidi ya mmoja, tatizo likitajwa kuwa ni ukosefu wa majengo malum kwa wazazi.
Mmoja wa watumishi katika hospitali hiyo aliiambia Nipashe hopitali hiyo ya Hai huwa na wajawazito zaidi ya 70 kila siku, hali isiyolingana na uwezo wa wodi iliyopo na hivyo baadhi yao kujikuta wakilala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Paulo Chaote, alikiri kuwapo kwa changamoto kadhaa ikiwamo ya uhaba wa vitanda, lakini akasema tayari suala hilo liko katika mipango ya kufanyiwa kazi na halmashauri ya wilaya yao.
KATIBU MKUU AFYA ANENA
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wajawazito katika hospitali mbalimbali nchini, Katibu Mkuu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, alisema ongezeko la wagonjwa ndio tatizo linalosababisha bajeti zinazotengwa kutotosheleza.
“Kila hospitali hutenga fedha na serikali inaongezea lakini bado hazikidhi kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa, tunaamini bajeti inayoandaliwa sasa na wataalamu itazingatia wingi wa watu,” alisema.
*Imeandaliwa na Romana Malya na Moshi Lusonzo (Dar), Furaha Eliab (Njombe), Paul Mabeja (Dodoma), Masyenene Damian, Rose Joseph, Winfrida Joseph, Neema Emmanuel (Mwanza), Marco Maduhu (Shinyanga), Mary Mosha (Kilimanjaro).










