Hivyo basi anayecheza na uhai au maisha ya binadamu mwenzake, haijui thamani na kwa kufanya hivyo anaweza akawa anamkejeli au kumsahihisha Mwenyezi Mungu, aliyemuumba.
Hali hiyo haitofautiani na ujio wa vyuo vingi jijini Mbeya vinavyotoa taaluma ya uuguzi vichochoroni ilihali havijasajiliwa wala kutambuliwa na mamlaka za kiserikali zinazoshughulikia ubora na viwango vya elimu.
Ni kucheza na maisha kwwani wasio na mafunzo ndiyo watakaokuwa wakitibu na kuhangaikia masuala ya uhai wa wanadamu. Ni hatari.
Zimwi hili la uendeshwaji wa vyuo vyenye taaluma ya uuguzi bila kuzingatia sheria, kanuni pamoja na maelekezo ya taratibu ambavyo vimezagaa na kufunguliwa kila pande kwenye miji na majiji, wilaya na mikoa mbalimbali kwa kasi ya uyoga.
Kwa namna hii, iwe kwa kujua au kwa makusudi, wamiliki wake wanapoteza malengo na ndoto za baadaye walizojiwekea wanafunzi wanaojiunga na taasisi hizi.
Wakiwatoza ada za juu mno tofauti na uwezo wa wengi, lakini pia kuwapotezea muda huku wakijua wazi hata wakishahitimu masomo na kupatiwa vyeti si rahisi kupata ajira waitakayo kwa vile taaluma hazina viwango.
Miongoni mwa vyuo hivyo vinavyotoa mafunzo hayo pasipo kusajiliwa au kutambuliwa kisheria jijini Mbeya. Ni pamoja na, Faraja Health & Management (Faraja Hema) kilichopo eneo la Uwanja wa Ndege wa zamani, kinachotoa kozi ya mwaka mmoja na ada ya Shilingi milioni 1.1 kwa bweni na Shilingi 540,000 kwa kutwa.
Kingine ni St. Peter’s Health Management kilichopo eneo ndani ya uwanja wa Maonyesho ya Nanenane. Nacho kinatoa kozi ya mwaka mmoja wa masomo kwa ada ya Shilingi milioni 1.2 kwa bweni.Wakati kiasi ada ya Shilingi 600,000 ikikitozwa kwa wanafunzi wa kutwa.
Pia kipo Chuo cha St. Josephine Nursing College ambacho mwanafunzi hulipia ada ya Shilingi milioni kwa bweni na 500,000.
Vyuo hivi vikitofautiana kiasi fulani na chuo cha St. Joseph Health Training College (JHTC), kilichopo Iganzo, Ilemi kule Isanga.Kinachofundisha kwa ada Shilingi milioni 1.45 kwa wanafunzi wanaokaa kutwa! Mbali na gharama hizo kuwa juu. kuna madai mengine kama ada ya usajili Sh. 15,000, malipo ya mitihani 30,000 na ada ya ustawi wa mwanafunzi michango yote ikiwa ni ziada ya Shilingi 125, 000.
Vipo vigine kama, Kapombe Dispensary kilichopo Kalobe na St. Raymond Health College kilichopo Igurusi kilometa 46 kutoka jijini Mbeya.
HOFU
Kinachosikitisha zaidi ni uchafu wa mazingira kwenye vyuo vingi ikiwa tofauti na kozi wanazoziendesha , utashangaa kweli hapa zinatolewa taaluma za afya?.
Mmiliki wa Faraja Heath & Management, Ulimboka Mwakilili, alipotafutwa kutaka kujua kwa nini anaendesha kozi za uuguzi na kutangaza chuo kikiwa hakina utambulisho na mamlaka zinazohusika. Alisema chuo chake kimesajiliwa na kinatambuliwa na Mganga Mkuu hata Mkuu wa mkoa.
“Chuo hiki ni maarufu jijini Mbeya na kinatambulika na Mkuu wa Mkoa pamoja na Mganga Mkuu, na kozi zinazoendeshwa zimethibitishwa na mamlaka zote,”alisema Mwakilili.
Hata alipoulizwa kwa nini nje ya chuo kina jina la Maarifa Tuition Center, ilihali kwenye vyeti na fomu kinatambulika kama Faraja. Alidai ni kosa la kiufundi ambalo linafanyiwa marekebisho.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dokta Seif Mhina, ambaye pamoja na kujua uwepo wa vyuo hivi hajachua hatua na ofisi yake; zaidi sana aliahidi kuvifutilia.
“Ingawaje sina taarifa sahihi kutoka kwa Muuguzi Mkuu, ambaye ndiye huleta taarifa zihusianazo na kuwepo kwa vyuo hivyo. Lakini nitafuatilia,”alisema Dk.Mhina.
Pia Muuguzi Mkuu, Esticia George, naye anaendelea kushauri mamlaka zinazohusika kuwafungia huduma wote wanaoendesha mafunzo bila kibali.
“Maadamu wamegundulika na imethibitika kuwapo kwa vyuo hivyo, nashauri serikali kuwachukulia hatua kali ikiwamo kuwafungia,”alisema.
Makala haya hayakuishia hapo, yalifululiza hadi ofisi zinazohusika na Usajili wa Vyuo vya Ufundi (Nacte) na kukutana na Edward Mnade, Msimamizi wa Nacte Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Katika maelezo yake alisema jukumu la taasisi hiyo ni kushauri pale ambapo mmiliki wa chuo chochote hajafuata taratibu, lakini haina rungu la kuvifungie vyuo hivyo.
Alikwenda mbali zaidi akisema, zipo hatua zilizochukuliwa kabla ya yeye kufika mkoani hapo. Ambapo chuo cha Faraja Health & Management, kiliwahi kupewa onyo la kuendesha chuo bila usajili.
Lakini pia kuendesha ‘programme’ zisizoruhusiwa. Kwa makosa hayo mawili mmiliki wake , Mwakilili, alitozwa faini ya Shilingi 4,000,000.
Ikiwa na mgawanyiko wa kila kosa Shilingi 2,000,000, ambapo mwandishi alionyeshwa risiti za malipo yaliyofanywa kwa awamu na mmiliki kisha kumaliza faini yote.
“Hata hivyo pamoja na Mwakilili kulipishwa faini hiyo, ameendelea kuendesha kozi bila kujali. Hii ni kwa kuwa Nacte hatuna mamlaka ya kumfungia, lakini kama tungepewa kibali ningefanya hata leo,”alisema Mnade.
Naye Msimamizi wa Baraza la Famasia wa Kanda ya Mbeya, Hitson Nzunda, alipotakiwa kulisemea suala la chuo cha St. Joseph,kinachoendesha kozi ya Basic Technician Certificate in Pharmacy, kozi inayoendeshwa kwa muda wa mwaka mmoja. Alikuwa na haya:
“Hakuna chuo kinachoendesha kozi kama hiyo nisichokijua Mbeya, hao hawana usajili kiufupi ni ‘matapeli’ tu na mimi ndiye msemaji wa kozi hiyo, alisema Nzunda.
Mmiliki wa St. Peter’s Bwana Magabe, alipopigiwa simu ili kutaka kupata ufafanuzi zaidi mara zote alisema yupo safarini. Ingawaje alimtaka mwandishi kuchukua fomu kwa kiasi cha Shilingi 10,000 na kuiwasilisha chuoni hapo ikiwa ameridhia.
Cha kushangaza, pamoja na kuwa na masharti ya kujiunga kwenye fomu hiyo ikiwamo kumtaka mwanafunzi aliyepata kiwango cha ufaulu wa alama ‘D’ kwenye masomo ya Biology, Chemistry na Fizikia, hata ambaye amefeli asiye na cheti anapokelewa.
“Kama unasema mwanao alifeli hilo lisikupe shaka, sisi tunampika na kumpatia ‘skills’ zitakazomfanya aendane na masomo yalivyo,”alisema Magabe, kwa njia ya simu.
Mmiliki wa St. Josephine, muda wote alipopigiwa simu na kutakiwa kufanya miadi ya kuonana naye. Mara zote alisema yupo hospitali ya rufaa anamshughulikia mgonjwa.
Wamiliki wa vyuo vya St. Raymond , Kapombe Dispensary na St. Joseph. Wote hawakuwa na majibu ya kukidhi kuelezea kwa nini wanaendesha kozi za uuguzi wakati hawana usajili au vibali.
Ndipo Msajili wa Vyuo Baraza la Uuguzi (TNMC), Lena Mfalila, alilizungumzia suala hili la utitiri wa vyuo vinavyojinasibu kuwa ni vya uuguzi wakati vinaendeshwa kinyume na utaratibu akisema:
“Baraza lina utaratibu wa kuomba usajili na mmiliki kabla hajakubaliwa ni lazima baraza lijiridhishe ikiwamo kukagua mtaala, vitabu, ubora wa walimu na mikataba yao, mazingira ya kufundishia pamoja na vifaa muhimu vinavyotakiwa kama chuo.”
Aliongeza kusema kuwa baraza lina utaratibu mzuri wa namna ya anayetaka kufungua chuo kuzifuata.
Isipokuwa baadhi ya wahusika wamekuwa wagumu kufuata taratibu, hivyo kujikuta kila mara wakitofautiana na sheria, taratibu pamoja na kanuni za baraza linavyotaka.
Akiwazungumzia wote waliofungua vyuo hivyo kiholela, Mfalila alisema hana neno sahihi la kuwaelezea ila akawafananisha na wezi wengine wowote.
“Isipokuwa hawa wizi wao hauonekani kama walivyo wezi wa mifukoni wanaowachomolea watu simu na vitu vingine.”
Aidha, alitoa wito kwa wanaowapeleka wanafunzi kwenye vyuo hivi, kuwa makini kuepuka kupoteza muda na fedha zao.
Alisema wanaowapeleka watoto wao sehemu kama hizo huenda wamekosa sifa zinazotakiwa. Lakini kama wangekuwa na vigezo stahiki wasingehangaika na vyuo vya uchochoroni ambavyo vingi havina tofauti na nyumba za makazi ya watu.
Mungu Iponye Tanzania!
Mawasiliano :0713/0765 937 378,amwambapa7@gmail.com










