Ni ajabu Wazanzibari kusherekea maradhi, misiba

13Mar 2016
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Ni ajabu Wazanzibari kusherekea maradhi, misiba

KWA wanadamu kuna mambo ambayo yanaweza kuchukuliwa kama uhayawani mojawapo ni kusherekea ama kushangilia misiba, maradhi au watu wanapokumbwa na misukosuko ya kimaisha.

Inashangaza kuona kuwa wapo wanaochekelea wakisikia fulani kafa. Kuna wengine wanaandaa hata karamu na kujifurahisha wanapotaarifiwa kuwa jamaa wanayemfahamu anaumwa ama amefikwa na tatizo. Inafika wakati wanasusia hata maziko!

Huo si uongo ni mambo yanayotokea hapa Zanzibar. Ni kwa bahati mbaya kwamba tangu kurejea mfumo wa vyama vingi yanashuhudiwa mambo mengi kama kuporoko kwa misingi ya ustaarabu na ungwana uliostawi kwa sababu ya kutoa nafasi ya kuchipuka chuki za kisiasa.

Binadamu unatakiwa kuweka kanda misimamo ya kisiasa, itikadi na dini pale mwezake anapokuwa na matatizo kama maradhi na misiba ili kumfariji na kushiriki katika matatizo hayo makubwa yanayoshuhudiwa kwenye maisha ya kila binadamu.

Cha ajabu Zanzibar kumeanza kuibuka vitendo ambavyo vinasikitisha na vinavuruga amani na uhusiano wa kijamii. Mathalani, kushangilia kifo au maradhi kwa sababu mtu huyo ni mwanasiasa ambaye si muumini wa chama chako? Ni mfuasi wa upinzania badala ya chama tawala.

Vitendo hivyo vinahitaji kulaaniwa na kukomeshwa na viongozi na kila mwana jamii awe Pemba au Zanzibar.
Katika maisha hakuna binadamu ambaye ataishi milele au bila kuugua kwa sababu na hayupo mwenye mkataba wa kuishi milele duniani.

Nirejee ukumbini kueleza kuwa baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) Salmin Awadhi Salmin, baadhi ya watu kwa bashasha na hamasa walishagilia kifo chake kwa sababu ya chuki za kisiasa na kutounga mkono harakati zake za kisiasa!

Mbali na mkasa huo pia wapo waliosherehekea kifo cha mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa UWT, hayati Asha Bakari Makame, baada ya kuripotiwa kuwa amefariki huko Dubai akitokea India kupata matibabu. Kisa ni tofauti za vyama .

Matukio hayo yalitanguliwa na msiba wa kitaifa baada ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kufariki mwaka 1999, baadhi ya watu pia bila soni walishagilia na wengine kufanya karamu kwa sababu hisia hizo za kisiasa.

Kuna wanasiasa ambao machoni ni watu wenye heshima na staha lakini wanapokuwa majukwaani humnanga kwa kauli chafu Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd bila sababu, mbali na imani za uchama na hisia za itikadi.

Wakati matukio hayo yakiendelea kuchafua ustarabu mila na utamaduni wa Zanzibar, wiki hii Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Shariff Hamad, afya yake ilizorota na kulazwa katika hospitali ya Hindu Mandal Dar es Salaam.

Lakini wapo walioanza kushangilia kuugua kwa mwanasiasa huyo mkongwe Tanzania Bara na Zanzibar wakiandika maneno ya chuki ndani ya mitandao ya kijamii na katika mabago ya kisiasa kwa sababu ya tofauti za kisiasa na misimamo ya kiitikadi.

Kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa John Magufuli na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein , mgombea urais wa ADC Hamad Rashid Mohamed, kumtembelea Hamad,alipotoka hospitalini ni somo na fundisho kwa wananchi kujiepusha kuchaganya mambo ya kijamii, utu na siasa.