Hao wavukao mipaka, hutumia muda mrefu kuhesabu siku nyingi, inaathiri biashara katika maeneo husika, ikiwamo kuuzwa kwa bei ya juu.
Sasa, tukio la kazi ya ujenzi wa reli ya kisasa kilomita 165, kutoka mkoa wa Tabora hadi Mji Mdogo wa Isaka, ni ujenzi wa kipande kinasaidia katika kukuza uchumi wa mikoa hiyo kupitia rasilimali zilizopo.
Ikiangaliwa katika mkoa wa Tabora, kuna fursa kubwa kutoka zao la tumbaku, hali ambayo reli inapokamilika, inaleta neema ya kujengwa viwanda vingi katika mkoa huo, kwani wawekezaji watakuja kwa wingi kwa kuvutiwa na mazingira ya miundombinu.
Vilevile inatajwa, kwa kutumia reli hiyo, pia inakuwa fursa kubwa katika kukuza baadhi ya mji iliyopo pembezoni mwa reli hiyo, pale vinapojengwa vituo vya kisasa kwa ajili ya abiria na mizigo hasa katika miji ya Isaka, Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga na mkoa wa Tabora.
Ni matarajio kwamba, reli itapunguza mwendo wa muda mrefu wa magari ya mizigo, hasa yale yanayoenda katika nchi za jirani, kwani yapo yanayotumia wastani wa siku saba hadi 30 katika safari za kwenda na kurudi, vyote vinatarajiwa baada ya reli kukamilika kuingia katika mabadiliko makubwa katika eneo hilo la usafirishaji.
MKURUGENZI TRC
Mhandisi Masanja Kadogosa, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), anasema vipande vyote vinne vya ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi jijini Mwanza, hadi zaidi ya mwezi mmoja uliopita, makandarasi na ujenzi wake wanaendelea na wananchi wamepata fursa ya kupata ajira za muda, huku taarifa ya hivi karibuni ya kiserikali muda mfupi uliopita ni vichwa vya treni vimeingizwa nchini kwa majaribio.
Anasema, ujenzi wa reli hiyo ulianza tangu mwaka 2017 na una urefu wa kilomita 1,596, ukitarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika mikoa hiyo na serikali ikiendelea na ununuzi wa mabehewa 89 kwa ajili ya kubeba abiria na mizigo.
Mhandisi Kadogosa anasema, mradi wa Tabora hadi Isaka unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi trilioni 2.6, ukichukua miezi 42 hadi kukamilika kwake mwaka 2026 na usanifu na utunzaji wa mazingira utazingatiwa.
“Ni mradi unaotarajiwa kuwa fursa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na serikali itakipanua Chuo cha Reli kilichopo mkoani Tabora, hata kikatoa shahada ya ngazi ya juu na tayari kimeshatoa ajira kwa watu 20, 000,”anasema Mhandisi Kadogosa.
WAKAZI WA ISAKA
Juma Bundala, ni mkazi wa Mji Mdogo wa Isaka, ambako reli hiyo ya kisasa itapita, hivi karibuni akiambia Nipashe kuwa wakati umefika wa mkandarasi anayejenga reli hiyo kuona jinsi atawapa kipaumbele katika kuwapa kazi wananchi na hasa vijana wa eneo, ambao watakuwa na sifa.
Anasema, kumekuwa na tabia ya wakandarasi kuajiri watumishi kutoka nje ya eneo la mradi hali ambayo imekuwa ikileta malalamiko makubwa kwa wenyeji walipo katika mradi husika na kushindwa kunufaika kwa kupata kazi za muda mfupi.
Naye Nyamizi Masanja, anasema mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya Yap Markez, haina budi kuangalia ajira kwa upande wa wanawake, ili nao waweze kujipatia ajira na kuweza kuendesha maisha yao kama walivyo wanaume ikiwemo za usambazaji wa chakula kwa vibarua.
WAKUU MIKOA KANDA
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yahaya Nawanda, anasema kukamilika ujenzi wa reli ya kisasa, kutasaidia kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga na kuwataka kuchangamkia fursa zilizopo katika mradi huo, ili kujiingizia kipato maradufu.
Anataja kazi zinazoweza kufanywa na wananchi wa maeneo mradi unapopita, wapewe ili waweze kukuza uchumi wao, hali ambayo itawasaidia kuwatoa kwenye wimbi la umasikini katika familia zao na kupunguza wimbi la vijana wa mitaani wasiokuwa na ajira na wizi wa mafuta katika mradi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Batilda Buriani, anasema reli hiyo itasaidia kuinuka kiuchumi wa mkoa wake, kwa wawekezaji kuiunga nao kiuchumi, kwani kwa sasa umekuwa hanuna viwanda na kusababisha malighafi yote kusafirishwa kwenda mikoa mingine yenye viwanda.
“Hakuna sababu kwa wawekezaji kutowekeza katika mkoa wa Tabora kwa kipindi hicho (reli ikikamilika), tunaweza kuwekeza katika mambo mbalimbali kama ujenzi wa Kiwanda cha Saruji kwa kuwa mali ghafi nyingi ya bidhaa hiyo inapatikana katika Mkoa huu,” anasema Dk. Buriani.
Aidha, anaeleza kukamilika kwa reli hiyo, pia utafungua milango katika maeneo hasa ya pembezoni yaliokuwa hayana viwanda kupata wawekezaji, kwakuwa usafiri wa uhakika utakuwapo na bidhaa zitafika kwa wakati sokoni na viwandani.
M/KITI KAMATI BUNGE
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu, Moshi Kakoso, anakasema kampuni ya ujenzi ya Yap Markez, mpaka Februari meaka huu, ilikuwa hijalipaa wakandarasi wadogo wa mradi huo kiasi cha Sh.Bilioni 12 na akawataka kufanya malipo, kuondoa migogoro, ili mradi utakapokamilika kusiwe na madai yoyote.
Waziri wa Ujenzi na Miundombinu Makame Mbarawa, anakasema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwaletea wananchi miundominu mizuri katika kipindi hicho na akiwataka kuchangamkia fursa pale miradi mikubwa ya kimkakati inapoanzisha na kujiingizia kupato.
MAKAMU WA RAIS
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, anasema, mradi wa Reli ya kisasa ni wa mfano barani Afrika na kutokana na hali hiyo serikali imeamua kuwekeza sekta ya usafirishaji ili kuhakikisha wananchi wake hawapati shida na bidhaa zinafika sokoni kwa wakati.
Anasema, ujenzi wake utasadia katika kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuliweka Taifa katika ushindani wa kibiashara huku akisisitiza ni lazima usimamiwe ili uweze kumalizika kwa wakati na kuanza kuwanufaisha wananchi pamoja na wafanyabiashara.
Aidha Dk. Mpango anasema, serkali imewekeza uwekezaji katika reli na Bandari, katika ujenzi wa reli hiyo jumla ya ajira 20,000 zimepatikana zenye thamani ya Sh.bilioni 237.6 ambazo zitatumika kulipa mishahara, shilingi trilioni 1.9 zimetumika katika zabuni huku serikali ikikusanya Sh.bilioni 949 kama kodi.
Hata hivyo Dk. Mpango anasema sehemu kubwa ya fedha za mradi huo ni mkopo na hakuna ubaya wowote wa kukopa nakwamba serikali haitaacha kukopa na uwezo wa urejeshaji upo na kuwataka viongozi na wasimamizi kusimamia fedha hizo vizuri ili mradi ukamilike kwa wakati na kutoa huduma zilizolengwa kwa wananchi na malengo ya kitaifa.










