Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akawa mgeni rasmi katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, kulikosheheni hadhira iliyooongozwa na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), nyuma yao kuna umma wa wafanyakazi na wananchi kwa jumla, wakiguswa na kauli mbiu 'uadilifu na weledi kazini, ni chumbuko la maisha bora kwa wafanyakazi'.
Kikuu kwanza kuvutia hadhira hiyo, ni ahadi ya mwaka jana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye akawaahidi wafanyakazi mwaka jana katika kile anatumia msamiati ‘jambo letu’ kwa maana ya maslahi, kwamba pande mbili zingekutana kuyajadili hayo.
Katika hotuba yake Rais Dk. Samia siku nne zilizopita, zilijaa mambo ya kuwatia moyo wafanyakazi, hata 'kuwakuna' katika namna ilivyojikita katika mambo makuu kadhaa, yanayogukia katika sura kuu mbili, yaani utekelezaji wa serikali kwa maslahi ya wafanyakazi, pili ahadi kwao.
Rais Dk. Samia akaweka bayana kuhusu utekelezaji wa madai ya malimbikizo ya wafanyakazi, akisema jumla yake yalikuwa 14,516 na kwamba tayari serikali imeshafanyia kazi madai 13, 523, huku akifafanua kwamba yamebaki machache.
Hapo akafafanua nafasi ya waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii, rais akisema ameshamwagiza waziri mwenye dhamana ya ajira pamoja na waziri mkuu, kufanya mkutano na waajiri ili wafanyakazi walipwe stahiki zao katika namna inayohitajika.
Mnamo Mei mwaka jana, Rais Samia aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara, ikiwamo kima cha chini kwa watumishi wa umma asilimia 23.3 na fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.59 ikatumika kuongeza hitaji hilo kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jambo ambalo wiki hii akalianika kwamba limeshatekelezwa kwa wafanyakazi hao wenye mishahara ya chini kwa asilimia 23 iliyopangwa katika bajeti ya sasa.
Eneo lingine la maslahi kwa wafanyakazi, Rais akasema Baraza la Kazi na Uchumi nchini limeshaelekezwa kusikiliza changamoto za mfumo wa fidia kwa wafanyakazi, ili iweze kutoa huduma, pia kuunda Kamati za Usalama Sehemu za Kazi, inayowajumuisha waajiri na wafanyakazi wenyewe.
Rais anafafanua kwamba, unahusu kuwaongezea watumishi vitendea kazi katika kitengo cha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ikiwa na maana ya kuendelea kuongeza wafanyakazi mahali hapo, pia magari ili kazi zake zifanyike kwa ufanisi
NYONGEZA KILA MWAKAPenye msamiati wa maslahi ‘jambo letu’ ambao Rais Dk. Samia aliutamka mwaka jana, sasa anataja mbinu mpya iliyowahi kuwapo zama zilizopita katika suala la nyongeza ya mshahara, wakati wa sikukuu ya mwaka huu mjini Morogoro.
Rais akafafanua staili ya nyongeza kufanyika kwa ukimya, hadi sasa namna ya utekelezaji wake unaendelea kufanyiwa kazi, rais akisema itaendana na kulipa malimbikizo ya madai katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao.
Anafafanua kuwa, hatua hizo sasa itafanyika kwa ukimya, ikilenga kuwabana wafanyabiashara wanaovizia matangazo ya mishahara mipya, kwa kupandisha bei za bidhaa zao sokoni, Rais Dk. Samia akiitafsiri inawaumiza watu wenye kipato cha chini.
‘Wafanyakazi mambo ni moto…mambo ni fire,’ akasikika Rais Dk. Samia wakati akitangaza kurejesha nyongeza ya mishahara ya kila mwaka kwa wafanyakazi wa umma, ikiwa ni miaka saba tangu kuondolewa mwaka 2016.
AHADI NYINGINE
Rais Dk. Samia anafafanua ahadi kuwa serikali itajitahidi kuwekeza na kuvutia uwekezaji nchini, kujenga uchumi, ili kutengeneza nafasi zaidi za ajira kitaifa kwa maslahi ya wafanyakazi wakiwa ni kipaumbele.
Hapo anatoa rai kwa vyama vya wafanyakazi viendelee kushikamana, huku serikali kwa upande wake ikifanya jitihada za kuhakikisha inaboresha maslahi yao, ikiwa ni sehemu ya umma kuendelea kuwa na maisha bora.
"Serikali itajitahidi kuwekeza na kuvutia uwekezaji, kujenga uchumi ili kutengeneza nafasi zaidi za kazi, kujenga uchumi ili maslahi yanayodaiwa na wafanyakazi yaweze kupatikana," anasema.
Lingine ni pale Rais Dk. Samia anapokumbusha kwa msisitizo kuwa, suala la uadilifu na weledi kazini ni muhimu kwa kila mfanyakazi, kwa kuwa ndio chimbuko la maisha bora kwao mahali walipo.
Kuhusu nafasi ya pekee kwa taaluma ya ualimu, ambayo kimsingi ina kundi kubwa la watumishi nchini wanaangukia ofisini kwake, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), huku kitaaluma wakiwa wanaunda nguzo ya uelewa na utaaluma kitaifa na kimataifa, Dk. Samia anagusia dai la haki zao lililoibuka bungeni hivi karibuni, kuhusu kuwapo posho za kufundishia.
Hapo rais akaahidi kulifanyia kazi kama walivyoomba, jibu hilo akiunganisha na dai linalohusu matumizi ya vishikwambi (tablets), ambazo wamepewa walimu kutekeleza majukumu yao, baada ya kutumika kwenye Sensa ya Watu na Makazi mwaka jana.
Siku chache zilizopita, Mbunge wa Kilwa Kusini mkoani Lindi, Ally Kasinge, akaibua hoja bungeni, jijini Dodoma kwamba elimu inaendelea kudorora kutokana na kuondolewa kwa posho ya kufundishia kwa walimu, akidai kwa sasa walimu wengi wamekata tamaa na kukosa ari ya kufundisha kwa madai kwamba kuondolewa kwa posho hiyo kunachangia hayo yote.
.