Hili la vyeti vya udereva kwa kweli, halijakaa sawa

05May 2023
Joseph Kulangwa
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hili la vyeti vya udereva kwa kweli, halijakaa sawa

JUZI nilikuwa mmoja wa wanahabari waliotembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa, iliyoko katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), katika ziara iliyoratibiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Tulitembelea hospitali hiyo, kwa lengo la kujionea ni kwa kiasi gani NHIF imewekeza katika suala zima la matibabu kwa Watanzania na hususan wanachama wake, ambao hata hivyo si wengi sana nchini.

Jambo kuu lililotuvutia watalii sisi, ni utaratibu wa wagonjwa walio wanachama kujisajili na kupata matibabu. Kuna ile dhana ya kutotumia karatasi asilani kama ilivyokuwa awali.

Tunakumbuka jinsi huko nyuma ilivyokuwa lazima kuandikisha cheti ili kumwona daktari na hata kufungua jalada lako la kumbukumbu za matibabu, ambayo mgonjwa alifika na kadi na kupewa jalada na kuzunguka nalo.

Kwa wagonjwa wa mara kwa mara, ni dhahiri jalada lilijaa na hata kuchakaa kutokana na wingi wa karatasi na ile zunguka zunguka nalo naweka toa kwenye makabati ya hospitali husika.

Kwa hospitali ya Benjamin Mkapa, mambo yamebadilika kabisa, ambayo sasa mgonjwa anatambuliwa kwa sura na alama za vidole na mawasiliano kuanzia hapo kidigitali. Hakuna karatasi kabisa.

Nimetoa bashraf hii, hasa kutokana na kinachotaka kufanyika nchini, kuhusu madereva wetu barabarani, eti kulazimika sasa kutembea na si tu leseni zao, bali pia vyeti vya udereva kutoka vyuo walivyosomea.

Tena kuna tangazo kuwa ukingoio mwa mwezi huu ndio mwisho wa kuhakikisha vyeti hivyo vipo na baada ya hapo utaanzishwa ukaguzi wa Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani, dhidi ya madereva watakaokuwa hawana vyeti.

Inashangaza kuwa wakati huu ambao watu wanatambulika kwa kado za uraia za NIDA, sasa tunataka kurejea kwenye analogi, kwa kutembea na vyeti. Kidogo kidogo baada ya hili, bila shaka tujiandae kutembea na vyeti vya kuzaliwa na vya ndoa.

Hivi kweli serikali haina uwezo wa kujua leseni gani ni bandia na ipi ni halali, mpaka kufikia kulazimisha madereva kutembea na vyeti? Inajulikana madereva leseni zinapomaliza muda hutakiwa kuzihuisha. Inakuwaje leo watiliwe shaka?

Nadhani polisi wanatakiwa kutafakari hatua hili, kwa kufanya ukaguzi wa kawaida tu wa leseni na watakapobaini dereva na leseni bandia basi waanzie hapo kwa kumchukulia hatua.

Dereva kajifunza au dereva miaka ya sabini, leo unamwambia atafute cheti chake atembee nacho barabarani, atakitoa wapi? Kwanza wakati huo nchi ilikuwa na vyuo vingapi vya udereva?

Wengi wa madereva walijifunzia majumbani kwa ndugu zao, baadhi walijifunzia kazini, mathalan jeshini ambako unaweza kujua udereva bila hata kutarajia, leo mstaafu anaendesha gari lake barabarani, asimamishwe na kuombwa cheti kweli!

Hatukatai kwamba ajali za barabara nini nyingi, lakini sidhani kama zinasababishwa na leseni, kwani kuna mambo mengi, hata wenye leseni za vyeti vya vyuo vikuu vya udereva, kama vipo wanaweza kusababisha ajali kwa sababu yoyote.

Lakini, bado gari linaloendeshwa na dereva mwenye shahada ya udereva, kama ipo,linaweza kusababisha ajali kutokana na ubovu wa muda mrefu au hata wa ghafla.

Miundombinu mibovu ya barabara nayo ina mchango mkubwa katika kusababisha ajali barabarani. Hivyo haitoshi kutazama tu leseni, kwamba ndicho kiini cha kusababisha ajali hizo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bila shaka ina kanzi data ya leseni za madereva wote nchini, hali kadhalika Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye mchango mkubwa sana katika kuthibitisha uhalali wa mtu kupewa leseni.

Tusijiegemeze kwenye vyeti, tukiamini kwamba ndiko kuliko na ujuzi au umahiri wa kufanya jambo, kwamba kama dereva hakupitia chuo cha udereva, basi hawezi kuelekezwa hata huko barabarani kwa kupewa elimu na kuwa bora.

Tutajikuta tunapanua wigo wa rushwa kwa baadhi ya askari wetu wasio waaminifu, ambao wengine tumekuwa tukiwashuhudia mchana kweupe wakiomba na kupokea chiochote.

Tumekuwa kila mwaka kwenye Wiki ya Nenda kwa Usalama, baadhi ya askari wasio waaminifu wakiigeuza kama wiki ya kivuno kwa kuuza stika, tukiambiwa kwa bei  kati ya Sh 5,000 na Sh 7,000 kutegemea ukubwa wa gari, bila hata kufanya ukaguzi. Hebu basi tulitazame hili kwa jicho la tatu. Alamsiki!