Uwanja wa Ndege Moshi, miaka 59 ukisuasua, lakini ni nyeti kiuchumi

05May 2023
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Uwanja wa Ndege Moshi, miaka 59 ukisuasua, lakini ni nyeti kiuchumi

NI ngumu kutenganisha maendeleo ya mkoa wa Kilimanjaro na Uwanja Mdogo wa Ndege wa Moshi toka mwaka 1954,"anasema mbunge wa jimbo la Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro Priscus Tarimo.

Anasema uwanja huo, umekuwa msaada kwa watu wa mkoa wa Kilimanjaro, mikoa ya jirani na nchi jirani hasa katika sekta ya utalii, matibabu na biashara.

Uwanja huo mkongwe wenye takribani miaka 69 sasa, bado unakabiliwa na uchakavu wa miundombinu hasa barabara ya kutua na kuruka ndege zinazokidhi mahitaji ya uendeshaji kwa sasa,ukosefu wa jengo la abiria, uzio wa usalama kuzunguka eneo la kiwanja unaosababisha wananchi kukatiza kiholela kwenye maeneo ya kiwanja.

Pamoja na juhudi mbalimbali za ulinzi zinazofanyika ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi lakini bado hazijafanikiwa,hali hii imesababisha barabara ya kutua na kurukia ndege ya kiwango cha nyasi (grass runway 18/36) kufungwa na kukosekana kwa gari la zimamoto, ambalo ni muhimu katika shughuli za uendeshaji wa uwanja wakati wa dharura.

“Uwanja huu ni moja kati ya viwanja 59 ambavyo vinamilikiwa na mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania, ambacho ni kikongwe kilifunguliwa mwaka 1954 ambao upo Magharibi mwa mji wa Moshi takribani kilometa nne toka mjini kati,”anatoa historia na kuendelea:

“Kiwanja hiki kilianza kufanya kazi na Serikali ya Malkia Elizabeth. Kinaitwa   Moshi Aerodrome & King George V1 Playing Field. Kuanzia miaka ya 1999 kiliendeshwa chini ya idara ya serikali katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakati huo na kuanzia mwaka 1999 mwishoni, kiwanja kinaendeshwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),” anaeleza mbunge

Anafafanua kwamba, miundombinu iliyopo kwenye kiwanja hicho kina ukubwa upatao hekta 296 zimeshapata miliki  tangu mwaka 2006, kukiwapo barabara mbili za kutua na kuruka ndege, moja ya kiwango cha lami yenye urefu wa mita 1,268 na upana mita 30.

Tarimo anataja nyingine, ni ya nyasi yenye urefu wa mita 1480 na upana wa mita 30, kukiwapo barabara mbili za viungio (Taxi ways) pamoja na maegesho ya ndege (Apron) kwa kiwango cha lami.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Uwanja wa Ndege Moshi una fursa kubwa za kibiashara katika nyanja za kitalii kwa kanda ya Kaskazini, ikiwamo kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vya asili.

“Mnada wa kahawa unafanyika katika Bodi ya Kahawa (TCB), wafanyabiashara kote duniani hushiriki na wapo baadhi yao walikuwa wakitumia uwanja huo katika kurahisisha muda wa watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro, wengi walitumia uwanja huo ” anasema.

Anaendelea kufafanua kuwa, uwanja huo unatumika pia katika suala la uokoaji katika maeneo mbalimbali hasa miji ya Mlima Kilimanjaro pamoja na kusaidia uzimaji wa moto katika mlima huo, pia kuna usafirishaji wagonjwa mbalimbali wanaohitaji matibabu ya haraka kwenda kama Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) au nchi jirani, ikiwamo jijini Nairobi, Kenya.

Lingine analolitaja ni kutumika  ndege zisizozidi uzito wa kilo 31,600, ambazo zinatoa huduma za zimamoto, kulingana na viwango vya Shirika la Kimataifa la Usalama wa Usafiri wa Anga (ICAO).

Vilevile, kunatajwa kuwapo karakana kwa ajili ya matengenezo ya ndege, huku asasi ya madaktari wanaosafiri nao wakitumia kiwanja hicho, kwa ushirikiano na Hospitali ya Rufani ya KCMC, ikiwachukua madaktari na wagonjwa kuwapeleka na kuwarudisha sehemu mbalimbali, kwa ajili ya huduma za kitabibu na kuna kampuni pia watu binafsi wanao hifadhi ndege zao mahali hapo.

Katika majukumu, Tarimo anafafanua kwamba kiwanja hicho kwa sasa inasimamia viwanja viwili vidogo (airstrips), ambavyo ni Kiwanja cha Same Kiwanja cha Ndege cha West Kilimanjaro.

Tarimo anasema, serikali imetoa zaidi ya Sh. bilioni 12 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo, ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu, utakaosaidia ukuzaji utalii na uchumi kwa ujumla.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Kilimanjaro ambao ndio wasimamizi wa ukarabati huo wa uwanja, Mhandisi Motta Kyando, anasema  malengo ya mradi huo ni kuboresha usafiri wa anga, kwa ajili ya kuinua Pato la Taifa kupitia sekta ya Utalii.

Anasema, kwa kuzingatia umuhimu wa viwanja vya ndege, ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Moshi, utaleta matokeo chanya ya ongezeko na kukuza sekta ya utalii.

“Mkataba wa ukarabati wa kiwanja hicho ulisainiwa Septemba 30 mwaka jana na kuanza rasmi Novemba 18 mwaka jana, ambao unategemewa kukamilika Novemba 18 mwaka 2023. Kulingana na usanifu maboresho ya Kiwanja cha Ndege cha Moshi, yanahusisha kufanya ukarabati wa njia mbili za kutua na kuruka ndege pamoja na ujenzi wa maeneo ya usalama,” anasema.

Mhandisi anafafanua: “Maboresho ya maegesho ya ndege, ujenzi wa barabara ya kuingia na kutoka uwanjani, kuweka uzio wa usalama katika kiwanja pamoja na kutengeneza barabara ya mzunguko ndani ya kiwanja na kujenga mitaro na karavati za kutolea maji."

 

RC KILIMANJARO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alipotembelea kiwanja hicho kushuhudia hali halisi, akamtaka mkurugenzi kuhakikisha wote waliovamia uwanja huo wanaondoka, ili kabla ya mkandarasi kukabidhi uwanja huo Novemba mwaka huu, awe ameshaweka uzio kuzunguka uwanja huo.

"Tumesikia hapa uwanja huu unatakiwa kuwekewa fensi, lakini changamoto ni baadhi ya wananchi ambao wamevamia katika eneo la uwanja na kujenga makazi sasa na kuagiza Mkurugenzi wa Manispaa, hakikisha watu hao wanaondoka mara moja ili kupisha shughuli za ukarabati zinazoendelea katika kiwanja hiki" anasema

Mkuu wa Mkoa anasema, uwanja huo wa ndege una muda mrefu, lakini ni sehemu muhimu kwa mkoa, hivyo anamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu, kuona umuhimu wa kuufanyia ukarabati uwanja huo.

Anasema, kukamilika kwa ukarabati huo kutachangia kuongezeka watalii wanaoenda kwenye Mlima Kilimanjaro wanaopitia mahali hapo.