Shule ya Msingi Kiloleli iliyoko Kishapu mkoani Shinyanga, haina vyoo na kama ilivyo ada wanaoathirika zaidi ni wasichana ambao wanakosa chumba cha kujistiri lakini pia wanaona aibu kujisaidia vichakani ili kulinda utu na heshima.
Wanahofia kwenda haja vichakani kutokana na uwezekano wa kunyanyaswa na kukejeliwa na hata kuumizwa ikiwamo kurushiwa mawe na watu wasiowafahamu.
Shuleni hapo vyoo ni vibovu na havifai tena kwa matumizi, anasema Mwalimu Mkuu Msaidizi Juliana Petro, akiongeza kuwa idadi ya wanafunzi ni 997, ambao wote wanajisaidia vichakani.
Aidha, anasema vyoo vya shule hiyo ni vibovu na havifai kutumiwa kwa sababu vinahatarisha usalama wa wanafunzi na afya zao, hivyo wakalazimika kuwazuia wasiendelee kuvitumia, bali watumie njia nyingine ikiwamo kwenda vichakani.
“Ni hatari kiafya shule kutokuwa na vyoo, na hapa hatuna hata maji ila tunashukuru wananchi wa Kiloleli wamehamasika na kuanza kujenga matundu 24 ya vyoo,” anaongeza Mwalimu Juliana.
Mwanafunzi Mary Joseph, anazungumzia hali hiyo akisema ukosefu wa vyoo unawapa shida nyingi wasichana. Mosi wanakosa eneo la kujisaidia lakini ugumu unajitokeza zaidi wakati wa siku zao, yote hayo yakiwasababishia wakati mwingine kuchukia kwenda shule hali inayoongeza utoro na hata kuwa na idadi kubwa ya wasichana wasiohitimu elimu ya msingi.
“Wanafunzi wa kike siyo kama wa kiume, sisi tunahitaji usiri mkubwa, sasa kwenda kujisaidia vichakani siyo jambo jepesi tena si maadili na ukimaliza kujisaidia hakuna hata maji kwa ajili ya usafi, wakati mwingine tunarudi nyumbani kujisaidia hasa wanaoishi jirani. Lakini wapo wenzetu wengine huondoka moja kwa moja bila kujali kinachoendelea darasani,”anasema Mary.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiloleli Kuhwema Mshala, anasema changamoto hiyo ya ukosefu wa vyoo Kiloleli wanaifahamu, na wameanza kuchukua hatua. Hivi karibuni walikutana na wajumbe wa kituo cha taarifa na maarifa kinachojengewa uwezo na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)kuibua matatizo ndani ya jamii, na sasa wanatafuta namna bora ya kushirikiana kuitatua.
Anasema waliitisha mkutano wa hadhara wa kijiji na wakakubaliana kila kaya kuchanga Shilingi 2,000 pamoja na kujitolea nguvu kazi ili kusomba mchanga, mawe, kokoto na kuchimba shimo la choo.
Anasema serikali ya kijiji kupitia mfuko wake nayo ilitoa Shilingi 600,000 na Jeshi la Jadi Sungusungu Shilingi 500,000 na kuanza ujenzi wa matundu 24 shuleni hapo.
Mtendaji wa Kijiji cha Kiloleli, Nicholaus Mzirai, anasema katika mchango wa fedha wananchi wamechangia Shilingi 700,000 na kwamba katika pesa walizopata za ushuru wa pamba Shilingi milioni 1.3 walikubaliana kutenga Shilingi 500,000 na kuzielekeza kwenye ujenzi wa vyoo shuleni hapo.
“Serikali ya kijiji tunashukuru wananchi kuhamasika na kuchangia shughuli za maendeleo, kwa sababu watoto wanaosoma katika shule hii ni wetu hivyo ni vyema kuwawekea mazingira mazuri ya kusoma kwa kuwajengea vyoo na kulinda usalama na afya zao,”anasema Mzirai.
Mkazi wa kijiji cha Kiloleli, Martha Ngwelu, anasema baada ya kuhamasishwa kujenga vyoo katika shule hiyo, waliitikia kutokana na hali ambayo walijionea wazazi na walezi jinsi kulivyokuwa na kuhatarisha afya za watoto wao.
Mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa kutoka Kiloleli, Helena Makelele, anasema baada ya kufika katika shule hiyo na kujionea vyoo vilivyokuwa katika hali mbaya na kufungwa, tena na kupokea taarifa za wanafunzi kuwa wanajisaidia vichakani, wakaanza kupanga mikakati na kuchukua hatua.
Anasema hatua mojawapo ni kushirikiana na uongozi wa kijiji na kukubaliana kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa vyoo na siku ya mkutano wakafanya harambee na kupatikana Shilingi 50,000 na mifuko mitano ya sementi.
Anasema katika ujenzi wa matundu hayo 24 ya vyoo shuleni hapo, kutakuwapo pia na chumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujistiri na kueleza kwamba ujenzi umefikia hatua ya kufunga lenta na kuwashukuru wananchi kujitoa ili kulinda afya za wanafunzi na wananchi majirani na eneo hilo.
Diwani wa Kiloleli, Edward Manyama, anasema tatizo la ubovu wa vyoo katika shule hiyo analifahamu, na wamekuwa wakizungumza kwenye vikao vya kata kuona namna ya kulitatua, na kushukuru wananchi wameanza kulifanyika kazi.
Ofisa Elimu wa Shule za Msingi na Awali Halmashauri ya Kishapu, Angasirini Kweka, anasema ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Kiloleli umetengewa Shilingi milioni 13 na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu imechangia Shilingi 600,000 ili kuunga mkono nguvu kazi za wananchi katika ujenzi wa vyoo.
Anasema halmashauri hiyo ina upungufu wa matundu ya vyoo 2,626 kwa shule za msingi na kwamba yaliyopo ni 1,281 huku mahitaji ni 3,907 na katika mwaka wa fedha 2023/2024, ulioanzwa kutekelezwa mwezi uliopita Julai mosi, Shilingi milioni 126.4 zimetengwa kwa ajili ya kujenga matundu 114.
Aidha, anasema kuwa katika mpango shirikishi wananchi wanatarajia kujenga matundu 1,004.









