jicho la ziada, kuwafikisha kwenye ujana wenye tija.
Eneo mojawapo linalohitaji kutupiwa macho ni nguvu kazi hii kuiepusha na kujiingiza kwenye kubeti na michezo mingine mingi inayochezwa kupitia mitandao na vyombo mbalimbali vinavyohimiza Watanzania kucheza ili kujipatia fedha kirahisi.
Haya yote yanafanyika kwa mwelekeo wa kamari na vijana wengi wamevutwa. Kimsingi masuala yanayohusiana na kucheza kamari siyo mazuri maana yanapelekea wahusika kupotoka na kujikuta kwenye uhalifu.
Kwanza, kuna kutekwa kifkra au kiakili na kupoteza maarifa ya kufanya maamuzi sahihi, kila wakati mhusika anabaki akijiweka kwenye nafasi ya kushinda tu, huku akitumia fedha ambazo harudishiwi iwapo hatashinda.
Pili, michezo ya aina hiyo, inajenga ‘lango’ la kutenda uhalifu ikiwamo wizi na udanganyifu, iwapo kijana hana fedha za kucheza, atafanya kila linalowezekana apate pesa kihalali au vinginevyo ili mradi afanikishe lengo.
Kihalali anaweza kuuza vitu vyake mfano, nguo, viatu, simu au akahangaika akapata kibarua na kupata fedha akacheze kwa mtazamo kuwa atashinda na kupata fedha atajirike haraka.
Vinginevyo, kuna uwezekano mkubwa kujenga tabia ya kudokoa mali za wengine au kuiba fedha na vitu vingine nyumbani, mitaani na hata kupora ili mradi afanikishe lengo lake.
Kwa bahati mtazamo huo usiofaa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi kubwa ya taifa letu, unachochewa na baadhi ya matangazo yanayofanyika kupitia vyombo mbalimbali mathalani, runinga, radio, magazeti na hata simu janja au viswaswadu.
Kuna wakati unapofungua ujumbe kwenye simu; mara kwa mara kuna ujumbe fulani zinazotangaza kuwa ‘wewe umekaribia kushinda kiasi fulani cha fedha mathalani, milioni 10, tuma ‘neno hili’ ushinde.
Ukiangalia tarakimu hizo na kwa lugha ya mitaani kwa ‘buku’ tu anahamasika kucheza, lakini ili aweze kushinda na kupata hizo fedha atacheza mara ngapi? Yote haya ni katika kugeuza akili za wengi na hasa vijana ambao ndiyo kundi kubwa linaloathirika zaidi.
Wakati mwingine yanaletwa maswali kadha wa kadha na mengi ni ya kimichezo hasa soka au kuigiza pia nyimbo hasa ‘bongo fleva’ na waimbaji wake. Nia ni watu wengi wajibu ili kuongeza mapato
Michezo inawafanya wengi wapoteze fedha zao kwa matumaini ya kupata au kushinda bila kujua wanaoshinda ni wachache sana kulingana na idadi ya wanaocheza.
Kabla mhusika hajacheza mchezo wowote wa kubahatisha, ni lazima kujua asilimia ya ushindi au uwezekano wa kushinda (probability rating) na hilo ni jambo la msingi. Kwa mfano, kuna wachezaji 1,000,000 kwa mchezo mmoja na pengine anatakiwa apatikane mshindi mmoja, washindi 10 au 100. Kinachotakiwa kukifahamu ni kujua kwa kiasi gani unaweza kushinda?
Kwa kundi la kwanza zitatolewa 1,000,000 pili milioni 10 na la tatu milioni 100, kiwango cha ushindi ni asilimia 0.0001, 001 na 0.01 kwa makundi hayo matatu sawia, hali hiyo inaonyesha kuwa ni asilimia ndogo sana ya mhusika kuweza kuibuka mshindi ndiyo maana ikaitwa ‘Bahati nasibu’.
Kadhalika, baadhi ya vijana hutembeza barabarani bidhaa mbalimbali mikononi wakitafuta wateja. Wengine wanatumia muda mrefu kutoka eneo moja kwenda jingine wakitafuta wanunuzi.
Jioni wanapoona hawana kitu mfukoni na njaa ‘imekaza uzi’ wanalazimika wauze kwa bei mnunuzi anayotaka ili mradi apate kiasi cha kumsaidia kujikimu.
Baadhi wanafamilia hivyo kujikuta katika changamoto hatarishi kiasi cha kulazimika kutenda uhalifu kwa kigezo cha ‘hakuna jinsi’ bora nusu shari kuliko shari kamili anaitelekeza familia yake.
Tujiulize kwa mstkabali wa taifa letu je, vijana kutaka kupata fedha haraka haraka kupitia michezo mbalimbali ya kifedha kama kubeti kitaifa ni jambo jema? Je, vijana na watu wengine tunatumia muda vizuri kwa manufaa yetu, familia na taifa pia?
Kimsingi, matumizi halisi ya muda kwa nyakati hizi ni suala la kuwekewa mkazo. Kila siku tunapoamka tunafanya nini? Maana unakuta makundi ya watu, rika mbalimbali, wakiongelea masuala ya michezo, mfano, kusajili wachezaji, hususani timu za Tanzania na Ulaya.
Kadhalika, unaona vijana wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ‘wakichati’ kupitia simu janja. Je, ni matumizi halisi ya muda? Siku ina saa 24, na wiki siku saba ina saa 168. Kawaida binadamu anatakiwa kulala usingizi (angalau saa nane kwa siku, kwa wiki atatumia saa56 usingizini).
Wiki ukiondoa siku moja ya kuabudu au kusali kuna siku sita za kufanyakazi. Hii ina maanisha kuwa tukiondoa saa za kusinzia; kwa siku tuna saa 16 za kufanyakazi na ndani ya siku sita ni takribani saa 96 za kufanyakazi.
Muda huu ukitumiwa kwa kiwango cha kufikia asilimia 75 takribani saa 12 kwa siku sawa na saa 72 kwa wiki, ukatumika kuzalisha mali na huduma ili kujipatia kipato, hakika nchi itajikwamua kimaendeleo na muda uliobaki takribani saa 4 kwa siku au saa 24 kwa siku sita za kazi; ukatumika kwenda na kutoka mahali pa kazi, pengine kupata mapumziko mafupi wakati mhusika akiwa kazini.
Uzoefu unaonyesha kuwa wengi wetu, wakiwamo vijana, hatuzingatii matumizi mazuri ya muda iwe ofisini, viwandani, nyumbani au kwingineko; bado kuna kusuasua bila maelezo ya kutosheleza. Vijana wajiepushe na kufuata mkumbo kwa masuala yasiyotuletea maendeleo ya kweli kimaisha.
Serikali iweke sera thabiti kuinua maisha ya Watanzania hususani vijana. Tuliporuhusu matumizi ya bodaboda na bajaji kutoa huduma za usafiri na usafirishaji; jambo hilo limekuwa faraja kwa vijana wengi kujiajiri au kuajiriwa. Wanaoitumia fursa hiyo kwa umakini, baada ya miaka michache wanasonga mbele.
Mkakati wa serikali wa kuinua zaidi shughuli za kilimo kwa lengo la kuwapatia vijana ajira na kuimarisha au kuendeleza uchumi wa taifa; upewe msukumo zaidi ili kuhusisha sekta mbalimbali za umma na binafsi
Kupanuliwe wigo ili vijana wengi waweze kujipanga kikamilifu kulingana na uwezo wao, wenye ari ya kufuga wafanye hivyo, kitaaluma au kibiashara, wenye kumudu masuala ya uvuvi, misitu, nyuki na utalii pamoja na biashara wafanye hivyo pia.
Kadhalika, shughuli za ugani ziimarishwe kuhakikisha mafanikio yanayotarajiwa yanapatikana. Tukiongeza tija na bidhaa nyingi kuzalishwa hapa nchini; tutajenga uwezo wetu kujitegemea. Wakati huo huo, tutasaidia idadi kubwa ya vijana kuachana na michezo isiyowasaidia, hivyo kuimarisha nguvu kazi ya taifa letu kwa faida ya wengi.
Halmashauri nchini na mamlaka za mikoa na wilaya; zihakikishe kuna mazingira bora ya kuwezesha vijana kutumia ardhi kwa faida na weledi mathalani, zianzishe mifumo thabiti ya kuunganisha vijana kwenye maeneo yao.
Kuweka fursa za mitaji kuwakopesha vijana; tukizingatia masharti nafuu na kuweka ‘kanzidata’ kuhusu vijana kuhusiana na taaluma na uwezo wao.
Katika kuyatekeleza hayo, uwazi na uadilifu vizingatiwe ipasavyo. Vijana wajengewe mazingira ya kuwa waaminifu katika kutumia muda vizuri na kutimiza wajibu ipasavyo. Viongozi kwa ngazi zote, tuwe waadilifu, siyo kwa maneno tu, bali kimatendo.Tuchukie udanganyifu, wizi, kutoa na kupokea rushwa au kukwapua mali za umma.
Hayo yawe mwiko katika sifa za kiongozi bora anayetumainiwa na wengi na kuachana na tamaa za kujitajirisha chapuchapu kwa kutumia njia haramu na zisizofaa, vyote vikomeshwe na watakobainika wachukuliwe hatua kali za kiutawala na kisheria.









