Wakijikita kwenye matumizi ya mbegu bora za alizeti na kilimo cha kisasa juhudi hizo zimewawezesha kupata mazao zaidi na kukua kibiashara na sasa wanamiliki viwanda.
Matumizi ya teknolojia ya kisasa, pembejeo na mbegu bora vimeongeza uzalishaji mavuno kwa wingi, kusindika alizeti kisasa na kupata mafuta yenye ubora na sasa wengine wanamiliki viwanda.
Mafanikio hayo ni ya mradi wa taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT), wenye lengo la kutoa elimu, kuhamasisha matumizi ya teknolojia, mbegu bora za alizeti na kilimo cha kitaalamu.
Baadhi ya shuhuda zinatoka kwa kinamama wanufaika ni kama hizi: Eva Tomson mkulima anayemiliki kiwanda cha kuchakata alizeti kilichopo Kibaigwa Dodoma, anasema alianza uwekezaji 2017, wakati huo biashara haikuwa na tija sababu uelewa mdogo na miundombinu duni ya kilimo.
Alikuwa na mashine moja lakini baada ya kuwezeshwa kitaalamu na taasisi ya Maendeleo ya Kilimo Denmark Asia (ADDA) Tanzania inayoshirikiana na AMDT anainuka baada ya kupata mashine iliyoongeza uchakataji na kupata madumu 200 ya mafuta kwa siku badala ya 50 hapo zamani.
Hadija Iddi, anaishi Kibaigwa pia, ana kiwanda cha kuchakata alizeti. Anajivunia mafunzo aliyoyapata ADDA chini ya mradi wa AMDT na sasa ameongeza soko na mapato.
Anasema awali walikuwa wanatumia madalali kununua alizeti leo wanakutana na wakulima moja kwa moja jambo linalowapunguzia gharama za manunuzi.
“Mafunzo ya AMDT yametukutanisha wafanyabiashara na wakulima, awali ugumu ulikuwepo hasa kwenye suala la soko wakati wa kununua mbegu unajikuta uko katikati ya madalali na wakulima, mnunuzi unapigwa hela kotekote ilimradi upate mbegu lakini kwa sasa hali hiyo haipo,” anasema Hadija.
Hawa Abdial, mwenye kiwanda cha kuchakata alizeti Dodoma, amenufaika pia na ADDA Tanzania na AMDT, akipata mashine ya kisasa na kuwezeshwa kutengenezewa miundombinu ya kisasa ya kusafisha mafuta na kuongeza ubora wa bidhaa anazozalisha.
“Mwanzoni nilikuwa nabahatisha, sasa naweza kuzalisha zaidi ya kilo 300,000 kwa kipindi chote cha msimu, tofauti na awali nikiishia kilo 180,000. Hiyo kwangu ni hatua kubwa kunijengea uaminifu kwa wateja wangu, walioongezeka kutokana na kuongezeka ufanisi na ubora.”
“Nawashukuru walionipa mafunzo kuanzia, SIDO na AMDT, nilikuwa sina cha kufanya, nilienda nikawaambia nina mashine lakini sina njia ya kutokea na walinishika mkono na kunisaidia kufanikisha uchakataji,” amesema Hawa.
Zuhura Mpinga, mkazi wa Kijiji cha Mayale mkoani Njombe, anasema alianza biashara ya mafuta miaka 10 iliyopita akiwa na mashine moja ya kukamua licha ya kwamba hakuwa na uelewa kuhusu kuchakata.
Anasema baada ya siku chache alikutana na taasisi iliyomshauri na kumkosoa kutokana na mfumo aliokuwa akiutumia na kumshauri kujiendeleza kitaalamu. “Nilifuata mafunzo waliyonipatia pia walinipeleka Dodoma kwa mafunzo, pia nilifundishwa namna ya kuweka kilimo mkataba na sasa wamenipokea watu wa AMDT,” anasema Zuhura.
UWEKEZAJI MKUBWA
AMDT imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani na tija katika kilimo nchini, kwa wanawake wanaosindika alizeti, ikiwasaidia mafunzo, vifaa vya kisasa na teknolojia kuwawezesha kuendesha shughuli za kukamua na kuzalisha mafuta bora ya alizeti inayolimwa kwa ubora.
Meneja wa mradi unaohamasisha kilimo chenye tija kwa upande wa ADDA Tanzania, Mercy Kingo, anasema wanashirikiana na wakulima na wasindikaji wadogo wa alizeti wanaofadhiliwa na AMDT ili kuongeza mnyororo wa thamani na kufikia uwekezaji wenye tija.
Anajivunia mafanikio kwa kina mama wanaosindika alizeti ambao ni miongoni mwa washirika wao, na kwamba wamewawezesha pia kuwa na vigezo vya kukopa kwenye taasisi kubwa za kifedha pamoja na kuingia mikataba ya manunuzi na wakulima wadogo.
Mercy anakiri kinamama wengi walikuwa na upungufu mfano kukosa mitaji na uwezo wa kusimamia na kuendesha viwanda vidogo na kwamba AMDT na ADDA Tanzania wakiwa miongoni mwa washirika katika utekelezaji wa mradi wamefanya jitihada mbalimbali kuwainua wajasiriamali hao na kukuza biashara zao.
“Pia tumewawezesha kutunza taarifa zao, waone faida ya kinachoingia na kutoka katika biashara wanayoifanya, pamoja na kuhakikisha viwanda na mitambo wanayoitumia kusindika inakuwa ya kisasa ili watoe mafuta yenye ubora,” anasema Mercy.
“Katika kufanikisha hilo mradi unatoa asilimia 60 katika kununua mashine za kisasa na wenyewe wanatoa asilimia 40 ya fedha, lakini pia tunawasaidia bidhaa wanazozizalisha zinapata masoko na waweze kufahamika.”
Anaeleza kuwa wanawasaidia pia kupata vibali vya Shirika la Viwango (TBS) pamoja na kuhakikisha miundombinu ya mahali wanapofanyia kazi inakidhi viwango.
Anasema wamewaelimisha pia namna ya kutunza faida zao, kurekebisha mazingira ya viwanda, kufanya kazi kwa utaratibu maalumu, na kuboresha miundombinu jambo ambalo limesaidia kuongezeka kwa ubora wa mafuta na kuwavutia wanunuzi wengi.
Anabainisha kuwa wanafanya kazi pia na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ili kuhakikisha viwango vya viwanda wanavyoviendesha kina mama hao vinakua sawa, na kwamba wanashirikiana pia na shirika la Brazil linalotoa huduma za kijamii viwandani (SESI) kuwapa mafunzo.
“Tunafanya kazi pia na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) na katika utekelezaji tunataka wasindikaji wadogo wafanye kazi na wakulima wadogo ili kuongeza mnyororo wa thamani wa alizeti,” anasema Mercy.
MALENGO AMDT
Mtendaji Mkuu wa AMDT, Charles Ogutu, anasema uwekezaji unalenga kuiwezesha miradi inayoendeleza alizeti na mikunde, kusaidia vipaumbele vya serikali katika kilimo na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDPII)
Pia inaelezwa kuwa mfuko wa maendeleo ya masoko ya kilimo AMDT unafanya kazi ili mapato na fursa za ajira za wanawake maskini, wanaume na vijana ziongezwe katika minyororo ya thamani ya kilimo.
Aidha, anasema taasisi inalenga kufikia azma hiyo kupitia matokeo mawili, la kwanza ni wakulima na wajasiriamali wadogo wanaweza kushindana na kufanikiwa zaidi katika masoko ya kilimo yaliyochaguliwa na kwamba kazi zinazowasaidia zinaboreshwa.
Ya pili ni kuweka mazingira wezeshi, kuboreshwa katika minyororo ya thamani ya kilimo ikiwemo sheria, kanuni, sera, taarifa, maarifa, uratibu na uaminifu, anaongeza Ogutu.









