Japan inavyojikuta njia panda majasusi wakiibia teknolojia, ubunifu

30Aug 2023
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Japan inavyojikuta njia panda majasusi wakiibia teknolojia, ubunifu

KESI ya madai ya kuvuja kwa teknolojia inayomhusisha mtafiti wa China katika taasisi ya juu ya utafiti ya Japan inachukuliwa kama mwanzo wa kuanza kufanya mambo kwa tahadhari zaidi, kulinda usalama wa taifa,

 

Ni baada ya Quan Hengdao, mtafiti mkuu mwandamizi katika Taasisi ya Kitaifa ya Sayansi ya Juu ya Viwanda na Teknolojia (AIST), mjini Tsukuba, katika mkoa wa Ibaraki nchini Japani, hivi karibuni alikamatwa kwa tuhuma za kutoa siri za kiteknolojia.

Anadaiwa kuvujisha data iliyopatikana kama sehemu ya kazi yake katika AIST kwa kampuni ya China, kinyume na sheria inayokataza ushindani usio wa haki.

Quan (59) amefanya kazi Japan tangu Aprili 2002 lakini pia akawa profesa katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Beijing mwaka 2006, kulingana na uchunguzi wa gazeti la Sankei. Chuo Kikuu cha Beijing na kile cha Sayansi na Teknolojia cha Nanjing ambapo alikuwa mwanafunzi, ni taasisi muhimu katika "Wana Saba wa Ulinzi wa Kitaifa," ikimaanisha kuwa zina uhusiano na Jeshi la China.

Aidha, Quan alikuwa sehemu ya programu ya "Thousand Talents" ya serikali ya China, ambayo inalenga kuvutia watafiti katika nyadhifa muhimu kuendeleza uwezo wa Beijing wa kisayansi na kiteknolojia.

TUHUMA ZAKE

Quan anashutumiwa kutoa data za siri za teknolojia za kuunganisha misimbo ya florin (florine codes) kwa mradi wa biashara nchini China ambao alianzisha na mkewe.

Miezi michache baada ya data hizo kutumwa, kampuni ya wanandoa hao ilipata hati miliki ya teknolojia hiyo nchini China.

Taarifa ambazo Quan alitoa "hazionekani kuwa zinazohusiana na ulinzi au teknolojia zinazohusiana na usalama wa kiuchumi," anasema Jin Matsubara, Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Kitaifa ya Usalama wa Umma ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chama cha Kidemokrasia cha Kikatiba cha Japan, chama cha siasa za mrengo wa kushoto ambacho ni kikubwa zaidi cha upinzani bunge la Japan.

Lakini kesi hiyo inaangazia uharibifu unaoweza kusababishwa kwa Japan, anasema, na kuongeza kuwa “Inapaswa kuwa kama kelele inayoamsha tahadhari kwa serikali”.

"Ni muhimu kutathmini kesi hii kwa mtazamo mpana," anasema. "Kuna malengo mawili ya sheria za Japan kuhusu sayansi na teknolojia; la kwanza ni kuzuia kupotea kwa teknolojia za hali ya juu na la pili ni kukuza mabadilishano ya kimataifa na kuwaalika watafiti wa kigeni wenye ujuzi na vipaji vya kipekee ili kushirikiana na wataalam wa Japan," Matsubara anaongeza.

"Ndio maana kuna Wachina na Warusi wengi katika taasisi za utafiti na vyuo vikuu nchini Japan," anaiambia DW.

"Watafiti hao wa kigeni wamekuwa muhimu sana kiasi kwamba taasisi zingine haziwezi kufanya kazi bila wao."

China na Marekani ziko kwenye vita vya kibiashara, ambavyo ni vikwazo vya kushiriki teknolojia ya kisasa.

Japani na mataifa ya magharibi kama Marekani zimezidi kuwa na wasiwasi katika miaka ya hivi karibuni kuhusu uhamisho wa teknolojia ya kisasa kwenda China.

Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden, unasema unataka kuzuia teknolojia ya hali ya juu ya nchi za magharibi kununuliwa na vikosi vya Jeshi la China na mashirika ya kijasusi. Mwaka jana, Washington iliweka vizuizi kwa China kupata ‘chip’ za kisasa na vifaa vya kutengeneza chip, sababu ikielezwa kuwa ni usalama wa taifa.

Japan na Uholanzi pia hivi karibuni zilitangaza vikwazo vipya vya usafirishaji wa bidhaa kwenye teknolojia ya utengenezaji wa chip, bila kuitaja China.

UPO UTETEZI

Matsubara anadokeza kwamba masharti ya sheria ya kitaifa ya ujasusi ya China yanawataka Wachina wote kutoa maarifa yote waliyopata ng'ambo kwa serikali, licha ya makubaliano yoyote ya kutunza siri ambayo wanaweza kuwa wametia saini kwenye mataifa ya kigeni.

Na hiyo ina maana kwamba “Kila Mchina ana uwezo wa kuwa jasusi, anaiambia” DW.

“Hii ndiyo sababu nchi kama Japan na Marekani hazina chaguo bali kuwatenga watafiti wa China kutoka taasisi zinazoshughulikia teknolojia nyeti sana za kiuchumi au zinazohusiana na usalama kupitia utumiaji mzuri wa mfumo wa kibali cha usalama,” anasema.

MAJASUSI WENGI

Swali hili linaulizwa kuna majasusi wengi zaidi nchini Japan? Na jibu linakuwa wengine wanaamini kwamba awamu za serikali za Japan zilizofuatana zimeshindwa kuchukua tahadhari zinazohitajika na kwamba usalama wa taifa hilo unahatarishwa.

"Sielewi jinsi Quan alivyoruhusiwa kubaki katika wadhifa huo kwa miaka 20 bila kuchunguzwa," anasema Yoichi Shimada, Profesa wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Fukui.

"Kwangu hii inaonyesha tu jinsi tulivyolegea linapokuja suala la mustakabali wa kiuchumi wa Japan na usalama wetu wa siku zijazo. Kwa kweli ni jambo lisilosameheka."

Shimada anasisitiza kuwa ana hakika kuna majasusi wengi zaidi kutoka China na kwingineko nchini Japan. Anatoa wito kwa serikali kutosubiri tena ianze kushughulikia tatizo hilo.

"Hisia yangu ni kwamba serikali hii na vyuo vikuu wamekuwa dhaifu sana juu ya matatizo haya na hii imedhihirisha ukubwa wa kadhia," anaongeza.