Natasha ndio jina alilopewa na wazazi wake, lakini katika ulimwengu wa ndondi alibatizwa Jonas jina la babaye mzazi au Tasha12 kutokana na umahiri wake wa mchezo huo.
Jonas au Tasha12 kama anavyojiita mwenyewe ni mmoja kati ya mabondia wakubwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa akiwa anashikilia mikanda ya ubingwa wa IBF, WBO na WBC katika uzani tofauti.
Tasha12 ambaye ni raia wa Uingereza, kwa sasa yupo nchini kwa ajili ya mapumziko yake binafsi, lakini ameamua kuchukua muda wake kwa kutembelea baadhi ya gym za mabondia wa Tanzania na ameshangzwa na mazingira aliyoyaona ya mazoezi huku wakiwa bado wanafurahia wanachokifanya.
Bondia huyo ambaye amepewa ubalozi wa Utalii, Zanzibar, amefanya mahojiano maalum Nipashe juu ya ujio wake nchini pamoja na mipango yake ya kuhakikisha mchezo wa ngumi za kulipwa Bongo unachukua nafasi kubwa.
Bondia huyo amefichua ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania safari yake ikianzia visiwani Zanzibar alifanikiwa kupewa zawadi ya ubalozi wa utalii wa kuhakikisha anavitangaza visiwa hivyo kupitia majukwaa mbalimbali atakayokuwa akiyatumia kupigana.
"Ni mara yangu ya kwanza kuwa hapa Tanzania, lakini nilianzia Zanzibar, wamenipa ubalozi wa utalii chini ya waziri wa utalii, kwangu imekuwa faraja kubwa kwa heshima ambayo nimepewa,” anasema Bondia huyo.
Mipango yake ya kutangaza utalii wa Zanzibar
Natasha anasema kufanya mambo mengi ya kuhakikisha Zanzibar inapokea watalii wengi ambao watakuja kutalii kwa sababu ni sehemu nzuri yenye mambo mengi ya kuvutia.
"Binafsi nimeweza kujifunza mambo mengi, uzoefu ambao nimeweza kuupata kupitia safari kubwa kuanzia visiwani hadi hapa Bara kwa sababu nilipata nafasi ya kuangalia hadi mechi ya watani wa jadi ambayo Simba walifanikiwa kushinda, ulikuwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii,” anasema Bondia huyo.
Sapoti yake kurejea masumbwi Zanzibar baada ya miaka 60
“Nadhani kunakuwa na programu maalum za kuendeleza na kukuza vipaji kwa lengo la kuwaendeleza na kuifanya Zanzibar ijulikane kupitia mchezo huu wa ngumi,” anasema Bondia huyo wa Uingereza.
Anasema anaimani kubwa ya Zanzibar kufanikiwa malengo hayo ya kuurudisha mchezo huo kwa sababu ametembelea baadhi ya gym na kuona vipaji vingi ikiwamo mchezo huo.
Gym za mabondia Dar es Salaam
"Nimeona mambo mengi yamenishangaza hasa upande wa mazingira ambayo mabondia wanafanya mazoezi, lakini bado wanakuwa na furaha.
Hili jambo limenihamasisha kwa kiasi kikubwa na kuona watu wanavyojituma katika mambo wanayopenda kufanya, nitawasapoti kadiri ambavyo inawezakana ili kuifanya Tanzania kuwa mmoja kati ya taifa kubwa la ngumi,” anasema Natasha.
Anasema baada ya kutembelea gym mbalimbali ameona changamoto za mabondia na anatarajia atakaporejea Uingereza atakutana na wasimamizi wake kwa ajili ya kuona jinsi gani wanaweza kunyanyua mchezo wa ngumi.
Tasha12 anasema anatamani zaidi kuona mchezo wa ngumi Tanzania unakuwa juu baada ya kuona baadhi ya mabondia kuwa na vipaji vikubwa akiwamo Hassan Mwakinyo ambaye aliweza kumshawishi kuja kufanya mapumziko yake nchini hapa.
“Mwakinyo alipokuwa Uingereza aliniambia nije kufanya mapumziko yangu hapa Tanzania, pia kupitia baadhi ya gym za mabondia na kuona vipaji, kweli vipo na ninatakapokuwa nyumbani nitakuwa balozi mkubwa wa Tanzania katika kuufanya mchezo wa ngumu unakuwa zaidi,” anasema Natasha.









