Msako wa Bodi ya Nyama ‘bucha na bucha’ hadi kufika machinjioni

09Jun 2023
Neema Hussein
MPANDA
Nipashe
Msako wa Bodi ya Nyama ‘bucha na bucha’ hadi kufika machinjioni
  • • Madudu kibao, zipo bubu, nyama ya kutu…

NI hivi karibuni, Bodi ya Nyama Kanda ya Magharibi, imefanya ukaguzi kuhusu usajili na utambuzi wa wadau katika tasnia ya nyama mkoani Katavi.

 

Hiyo inatajwa ni kuendelea kusisitiza uzingatiaji Sheria ya Mwaka 2006, inayowataka wafanyabiashara wa wanyama kulinda afya za walaji.

Ni ukaguzi unaofanyika, huku bodi hiyo ikihitimisha kazi hiyo katika mkoa wa Katavi, kwa kuwapitia wadau mbalimbali wa tasnia ya nyama kuwakagua.

Hapo wanajumuishwa wanenepeshaji, wamiliki wa machinjio, wamiliki wa minada, pia mabucha, pamoja na wafanyabiashara wa mifugo na wengineo katika mnyororo wa thamani wa nyama na mazao yake.

OFISA WA BODI

Joseph Kulwa, ni Ofisa Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Magharibi, anasema kitu walichokibaini ni wadau kutofuata sheria ya tasnia ya nyama.

"Sheria hiyo bado hawaitii, hawafuati maelekezo yaliyopo. Cha kwanza, sheria inawataka wadau wasajiliwe na watambulike, lakini tumezunguka jana na leo tumebaini kuna takribani mabucha sita ambayo yamefunguliwa kinyume na taratibu, yaani mabucha bubu.

"Hayo mabucha ni ya watu ambao kwanza ni wadau wetu, lakini wameongeza ‘udau’ kwa kuongeza biashara ya mabucha, hivyo wanafanya biashara kinyume kwa kutosajiliwa.

"Cha pili, tulichokibaini wadau wetu bado wanaendelea kutotii maelekezo ya sheria yalivyo, kwa kwenda kinyume na utaratibu. Bado mabucha ni machafu, bado upimaji wa afya ni tatizo, bado matumizi ya magogo yapo, matumizi ya nondo chafu na uuzaji nyama ambazo hazijakaguliwa machinjioni.

"Kama tunavyofahamu, sheria hii inataka mnyama akaguliwe machinjioni na auzwe buchani, kwa hiyo hii bado ni changamoto kwa wadau wetu. Kwa hiyo, tunatoa elimu pale inapolazimu tunawapiga faini, ili pengine kuwakumbusha kwamba ni takwa la kisheria, wanatakiwa wafuate utaratibu kadri ya sheria ilivyo.

"Machinjio yetu ya Mpanda hoteli naweza sema wanafanya maboresho, japo bado mapungufu yapo, kama vile matumizi ya nondo chafu machinjioni, kutokuwa na vyoo ambavyo havina sifa, lakini uzio unajengwa, japo haujakamilika, hakuna ofisi za wafanyakazi, pia hakuna utaratibu wa watu kuingia machinjioni.

"Yule ambaye anatakiwa kuingia machinjioni, ni ambaye anafanya shughuli za kuchakata mnyama na mazao yake kama vile utumbo na bidhaa nyingine za nyama, lakini unaona kabisa machinjio inaruhusu wadau mbalimbali. Ni kwa sababu ya kutokuwa na uzio.

"Uzio pia una umuhimu kuzuia wanyama wanaoingia machinjioni kama vile mbwa, fisi, ndege wasiofaa kuingia machinjioni. Tunashukuru kwamba, Manispaa (Mpanda)_ wamiliki wa machinjio wanajitahidi kujenga uzio, hivyo tunawaomba wakamilishe haraka.

"Hatua ambazo kama Bodi ya Nyama tumezichukua, tutaandika wito wa onyo kwa mmiliki, lakini tutatoa kusudio la kufunga machinjio, endapo yale tulioyabaini hayatatekelezwa.

"Wito wangu kwa wadau walio kwenye tasnia ya nyama, watii sheria bila shuruti, watii sheria ya tasnia ya nyama, hakuna sababu ya kukaa tunafungiana, hakuna sababu ya kutozana faini, wayafuate yale ambayo sisi wakaguzi mara nyingi tunawaelekeza.

"Mara nyingi tunavyofanya ukaguzi huu tunakuwa waungwana, tunawaambia hili hapana! Tunawapa muda, sasa kama hawatekelezi, tunalazimika kufunga na kuwapiga faini,” amatamka Kulwa na anaendelea:

“Wakifuata maelekezo, biashara itakuwa vizuri, mazingira ya biashara zao pia yatakuwa vizuri na kujikuta tunainyanyua tasnia ya nyama kutoka shambani mpaka kwa mlaji wa mwisho."

 

MSIMAMIZI MACHINJIO

Juma Gilibert, Msimamizi wa Machinjio ya Mpanda Hoteli, anasema kwa upande wa Manispaa, kwa machinjio changamoto kubwa kwao imekuwa kukosekana uzio.

"Kulingana na upatikanaji bajeti, tumekuwa tukipanga kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya machinjio, ikiwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa uzio kama unavyoona (yanajengwa) bado sehemu kidogo tu kumalizia, ambao muda si mrefu tutamalizia.

"Tatizo jingine lilikuwa ufinyu wa sehemu ya kuchinjia, hivyo serikali ilitoa fedha tukatanua sehemu ya kuchinjia, serikali imeendelea kutenga bajeti, ili kuendelea kuboresha miundombinu mingine kama vile ofisi na banda la ngozi," anasema Juma.

 

MUUZA NYAMA

 

Frank Mwita ni mfanyabiashara wa nyama soko Kuu la Mpanda anasema biashara kwa sasa si mbaya kutokana na uboreshwaji wa mabucha ikilinganishwa na awali mabucha mengi yalikuwa machafu.

 

"Tuliambiwa kuweka vyuma vya aluminiami tuwe na jokofu ndani, kwa hiyo hiyo hata nyama ikilala haiharibiki haraka na vyuma havitengenezi kutu, tofauti na vile vya zamani," anasema Frank.

 

Muuzaji mwingine, Hussein Aniseti, anasema hana vyuma, hivyo kutokana na changamoto ya havipatikani Mpanda, inamfanya aviagize kutoka Dar es Salaam na sasa anaahidi kutekeleza maagizo aliyopewa na mamlaka, kuwa na vyuma visivyoweka kutu, hata kuharibu nyama.

 

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form