Afrika yote ikacharuka wakati huo vuguvugu la kudai uhuru lilikuwa juu, baadhi ya nchi kama Msumbiji zikiwa na mwaka mmoja wa uhuru.
Nchini Tanzania, ni tukio lililoukera umma ukiongozwa na Baba wa Taifa, Rais Julius Nyerere, kwa hisia hiyo akiungwa mkono kwa namna nyingi, ikiwamo bendi maarufu ya muziki wa dansi ya Urafiki, maarufu ‘Wana- Chakakua’ ikitunga kibao chenye hisia kali kukemea kilichotokea.
Daima suala la kumtetea mtoto halijawahi kusahaulika, akikumbukwa Mwalimu Nyerere, kuna wakati akahoji katika hotuba yake akitamka “Philosophically (kifalsafa) inanipa tabu, kwanini mtoto mdogo anafariki?”
Ni katika mwendelezo huo wa kumpenda mtoto, mwaka 2009 katika utawala awamu ya nne nchini, kukatungwa Sheria ya Mtoto Tanzania, inayolenga kumlinda na kumtetea mtoto na ndio inayotumika hadi sasa.
Kupitia awamu tofauti za uongozi wa nchi, kumekuwapo na uamuzi unaolea na kuboresha ustawi, haki na ulinzi wa mtoto na ndio maana, sasa kunashuhudiwa huduma za bure katika elimu hadi kidato cha nne, uzazi, pia watoto katika umri mdogo, mengine yakiwa yameamuliwa kisera, pia kitikadi nchini.
KINACHOENDELEA SASA
Wakati anakabidhiwa kiti kuwa Rais, mara moja Dk. Samia Suluhu Hassan akapatiwa jina ‘Mama’ kwa maana ya wajihi wake kijinsia, historia ya nchi, pia matarajio ya uzazi kiutawala.
Ndicho kinachotawala katika miaka miwili na ‘ushee’ wa utawala wa Rais Dk. Samia, akiwa katika mazingira ya ushirikiano wa ‘umama’na umma anauongoza ukisimama katika wasifu ‘mtoto.’
Dhana ‘mama ni mama’ ikajitokeza katika mkasa siku aliposimama na kumpisha kiti Georgina Magesa, mtoto mwenye umri miaka nane, akimruhusu akae, Rais Dk. Samia, akuifikia hatua hiyo, baada ya kuona makala fupi ya mtoto huyo iliyorushwa kwenye televisheni, akielezea ndoto zake za kutamani siku moja akawa Rais wa Tanzania.
Katika mkasa unaofanana na huo, mtoto mwingine aliyekuwa katika matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili akidhaminiwa na Rais Dk. Samia, hata alipipata nafuu akaomba akarejeshe shukurani, tukio ambalo alipowa fursa ya kurejesha shukurani kwa ‘mama’, akaishia kwenye bumbuwazi la furaha iliyoangukia katika kilio cha ‘ahsante.’
Vilevile, katika tukio, la ‘umama’ linalojitokeza upande wa pili, kwa simulizi ya wito kutoka kwa Filomena Chale, mkazi wa London, mjini Songea, akimwomba Rais Dk. Samia msaada wa shilingi milioni 1.5 za matibabu ya mjukuu Karen Mwingira.Hiyo ni anayesumbuliwa na tatizo la kichwa, matibabu yanayotakiwa kufanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, akiamini rais huyo ni nguzo ya msaada wake.
Katika mtazamo wake, mnamo Julai mwaka jana akifungua jengo jipya la Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam, Rais Dk. Samia, akawataka wauguzi nchini kuacha dharau kwa wajawazito, kuwaepushia na vifo vinavyozuilika.
Dk. Samia akasema lengo la ujenzi wa jengo hilo ni kumpatia mwanamke huduma bora ya uzazi tangu ujauzito, kujifungua na hatua ya uangalizi wa mtoto mchanga.
Hapo akataja mikakati ya kuboresha huduma kwa wajawazito na watoto wachanga, kwamba Wizara ya Afya, inashirikiana na vyama vya madaktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, wakianzisha mfumo wa kupitia takwimu za vifo vya mama na watoto, wakati wa kujifungua.
Pia akaelekeza mamlaka za kiserikali kuhakikisha madaktari bingwa wanakuwapo katika ngazi ya hospitali za wilaya, ili huduma hizo zipatikane kirahisi.
Maelekezo yake kwa Wizara ya Afya, ni kuhakikisha hospitali hiyo inafikia uwezo wa kuhudumia wanawake 300 kwa siku, iwe na jumla ya vitanda 140 na vyumba vinane ya kinamama kujifungua, hata kupata uwezo wa kuwachunguza mapema na kuwatibu watoto waliozaliwa na ulemavu.
Anasema, kuwapo hospitali hiyo ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2021/2022 – 2025/2026 wa kupunguza vifo vya uzazi kutoka vifo 321 kwa kila vizazi 100,000 hadi vifo 220.
ATOA MSHAHARA WAKE
Unasaba wa Rais na watoto nchi mwake unamea katika hatua pale anajitoa zaidi, mwaka jana alipoamua kuchangia fedha zake Sh. milioni 15 kwa Mtoto Ali Kimara (10), ambaye amekuwa akisumbuliwa na changamoto ya kupumua kwa takribani miaka nane, hadi wakati huo.
Mnamo Julai mwaka jana, miezi minne tangu achangie Sh. milioni 15, mara nyingine Dk. Samia akachangia fedha za mshahara wake Sh. milioni 70 kwa asasi ya Doris Mollel Foundation, akiwa mkoani Kigoma, kuhudumia watoto.
Ni fedha ambazo mgawanyiko wake, Sh. milioni 20 akazitoa kuwasaidia watoto waliozaliwa njiti kupitia shirika hilo lisilo la kiserikali, huku kiasi cha Sh. milioni 50 zikienda kununua vifaa tiba vya kuwasaidia watoto hao.
Akitoa shukrani zake, mama wa mtoto njiti, Halima Mathayo anamshukuru Rais Dk. Samia kwa kuboresha huduma za afya nchini, hasa kwa kinamama kwa kutoa zawadi zinazohudumia na kuwalea watoto wao.
“Rais Samia amewashika mkono kinamama waliojifungua watoto njiti kwa kutoa mashuka, blanketi, vitenge, sabuni, pampasi, mafuta ya nywele na mahaitaji mengine, ikiwa ni pamoja ba vyakula kama mchele na sukari,” anatamka Waziri Angella Kairuki, mwaka jana akiwa katika Hospitali ya Rufani Maweni, mjini Kigoma.
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, katika tuko hilo akatoa ahadi ya serikali kuwaletea vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti, akiorodhesha mashine za kufua hewa ya oksijeni, mashine za kuzalisha hewa joto na zile za kutunza watoto njiti.
Ni hoja inayopokewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Maweni, Dk. Stanley Binagi, anayesema vifaa tiba na mahitaji hayo, itasaidia utoaji wa huduma bora kwa watoto njiti waliopo na watakaozaliwa katika hospitali hapo.









