AJENDA YA SIKU MAZINGIRA 2023…

09Jun 2023
Vitus Audax
MWANZA
Nipashe
AJENDA YA SIKU MAZINGIRA 2023…
  • Taka plastiki shida, zachafua Ziwa Victoria zikidhuru viumbe waliomo

NI siku kadhaa tangu kumalizika Wiki ya Mazingira Duniani. Pia ni jana tu gazeti la Nipashe liliongozwa na habari, mabomba ya sindano kati ya uchafu unaokotwa kwa wingi ufukweni.

 

Ndani ya maadhimisho hayo ya Siku ya Mazingira Duniani, kunaripotiwa shughuli za kibinadamu zimeendelea kuwa kikwazo katika vita dhidi ya utupaji holela bidhaa za plastiki Ziwa Victoria, hata kuhatarisha uhai wa viumbe vilivyomo majini na nchi kavu.

Duniani kunatajwa kila dakika kuna chupa za plastiki za maji ya kunywa milioni moja zinanunuliwa, pia mifuko ya plastiki trilioni tano inayotumiwa kwa siku, inatumika kila mwaka na sehemu ndogo ndiyo zinarejeshwa kwa matumizi.

Utafiti uliofanywa na mwanazuoni na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bahati Mayoma, mwaka 2014, ukabaini asilimia 95 ya uchafu Ziwa Victoria, ni wa vipande vidogo vya plastiki.

Pia katika ngazi ya dunia, tani milioni nane za plastiki zinaishia bila kufanyiwa kazi.

Mwaka 2015, mwendelezo wa utafiti ukabaini vipande vya plastiki chini ya ziwa hilo ni zaidi ya tani 150, vilevile ukagundua wastani wa samaki mmoja kati ya watano wamemeza vipande hivyo, hali inayohatarisha uhai wa viumbe hivyo na binadamu wanaowatumia kitoweo.

ZIARA YA MIALO

Nipashe ilitembelea kwenye baadhi ya mialo mkoani Mwanza na kubaini uchafuzi wa Ziwa Victoria unaofanywa na wavuvi, pia wafanyabiashara katika mialo hiyo, sehemu kubwa ni uchafu uliojaa mifuko na chupa za plastiki.

Inatajwa kuwa hali inayosababishwa na ongezeko la watu eneo hilo lisilo na sehemu rasmi ya kumwaga taka. Pia kuna taka zinazosafiri mitaroni, maji yakitiririsha mkondo wake katika Ziwa Victoria, hivyo taka zote zinasombwa, zikiwamo plastiki na zinakusanywa ziwani, hata kusababisha miundombinu ya barabarani inaziba, zikichangia mafuriko barabarani.

Abdullahaziz Shabani, ni mvuvi katika Mwalo wa Mswahili, anasema wamekuwa wakikusanya taka jirani na ziwa, ila wingi wa wafanyabiashara na wavuvi eneo hilo imechangia taka zaidi kuingia ziwani, ikihatarisha afya zao na viumbe majini.

Rai yake, anawaomba wadau wa mazingira, pia mamlaka husika kupambana na kudhibiti hali hiyo, ili kurejesha mialo na maziwa kwa ujumla kubaki salama.

Wadau wa mazingira wanaiambia Nipashe kuhusu wajibu wa kudhibiti plastiki kuchafua Ziwa Victoria na vyanzo vingine vya maji.

Mratibu Mkuu wa Shirika la Synergistic Globe, Angelina Manyama, anaelimu kwa watumiaji na majirani zao, kuhusu haja ya kulinda vyanzo hivyo, ndiyo suala muhimu.

“Elimu hiyo inatakiwa kutolewa kwa watu wote, hususani waliopo karibu na mitaro inayotiririsha maji katika vyanzo vikuu vya maji, vilevile kwa wafanyabiashara na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Victoria, kuhakikisha wanatunza ziwa hilo kwani mifuko ya plastiki inayo sumu,” anasema Manyama.

Anasema mara kadhaa, wamekuwa wakitembelea mialo hiyo kwa lengo la kuelimisha, pamoja na kushiriki katika kufanya usafi na kutoa elimu ya utunzaji mazingira, lengo ni kudhibiti shughuli hizo za uchafuzi.

“Kuna haja ya kusimamia kikamilifu sheria za mazingira juu ya wale wanaotumia plastiki, kisha kuzitupa holela hali inayosababisha kuendelea kuonekana kwa uchafu huo katika Ziwa Victoria, vilevile kupitia sheria ya uzalishaji wa plastiki serikali iendelee kuweka mkazo wa kuzuia: anasema.

BODI ZIWA VICTORIA

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Renatus Shinhu, anaeleza mikakati ya bodi hiyo kudhibiti uchafuzi ziwani, kupitia shughuli za kibinadamu, anasema jukumu la utunzaji vyanzo vya maji ni la kila mwananchi.

Anaeleza watumishi wa bodi hiyo kwa kushirikiana na watumiaji, pamoja na wanaofanya shughuli zao karibu na vyanzo vya maji, kuhakikisha wanafanya usafi Ziwa Victoria, kwa kuondoa taka ngumu zikiwamo plastiki na magugumaji, huku kuelimishana kukichukua nafasi yake kujihami na athari za uchafuzi wa vyanzo maji.

Kwa mujibu wa Renatus, kosa kisheria kuweka dampo la taka katika eneo lenye chanzo cha maji, hivyo kwa wanaogundulika, wanauchukuliwa hatua za kisheria.

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria inahimiza uzingatiaji Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya Mwaka 2009, inaeleza umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji na kueleza kuwa, palipo na wingi wa watu na uzalishaji taka unakuwa mkubwa.

Pia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria linataarifu hatua zinazochukuliwa ni kuhakikisha wanadhibiti uchafuzi wa plastiki kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Baraza la Taifa (NEMC) ambao wanawajibika katika kukamata na kufungua mashauri kwa watu wote wanaogundulika kuwa na viwanda vya uzalishaji wa mifuko hiyo, huku wanaotengeneza chupa za plastiki kuhakikisha zinaweza kufanyiwa kazi nyingine na kuweka ufuatiliaji.

KUTOKA NEMC

Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, Jarome Kayombo, anaiambia Nipashe, mamlaka yake iko katika hatua  kudhibiti uzalishaji bidhaa za plastiki aina zote, isipokuwa zinazotumika kuwa kifungashio kusimamia ubora, mfano hai ni dawa.

Anataja Sheria ya kuzuia Matumizi ya Mifuko ya Plastiki ya Mwaka 2019, inataja makosa matano, ambayo ni: Kuzalisha na kuagiza mifuko ya plastiki; kusafirisha nje; kuhifadhi na kusambaza; kuuza; pia kumiliki na kutumia.

Kuhusu uzalishaji na uagizaji bidhaa za plastiki, au kuziingiza nchini, Kayombo anataja adhabu ni faini kati ya Sh. milioni 20 mpaka Sh. bilioni moja, pia kifungo cha miaka miwili, au vyote kwa pamoja.

Vilevile anasema, kwa wanaotiwa hatiani kusafirisha mifuko hiyo kwenda nje, faini dhidi yao ni shilingi milioni tano hadi Sh. milioni 20, jela miaka miwili, au vyote kwa pamoja.

Aidha, kwa wanaotiwa hatiani kuuza na kusambazaji wa mifuko hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, adhabu yao ni kati ya Sh.100, 000 hadi Sh.500, 000, kifungo cha miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

Vilevile, sheria hiyo inagusa mtumiaji wa mfuko wa plastiki, adhabu yake ni faini ya Sh.30, 000 hadi Sh.200, 000, kifungo cha siku saba au vyote kwa pamoja.

Hivyo, anaitoa wito kwa wahusika kuacha kujishughulisha na bidhaa hizo, wabaki wazalendo wa kulinda na kutunza mazingira dhidi ya taka za plastiki, inayochangia kulinda viumbe hai.

Mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, mwaka huu yamefanyika kitaifa mkoani Dodoma, yakiwa na kaulimbiu ya ‘Pinga Uchafuzi wa Mazingira unaotokana na Taka za Plastiki’

 

Top of Form

Bottom of FormuktokaKUT

 

cTop of Form

Bottom of Form