Tanzania ni miongoni mwa zenye hali ya hewa na mazingira bora, kwa uzalishaji wa mkonge ambao ni zao la biashara.
Kwa wastani, mkonge unaweza kuishi wastani wa kati ya miaka 13 hadi 14, majani yake yanaweza kufikia urefu wa futi 200 hadi 300 hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile kamba nene, magunia, heleni na mazuria.
Kadri miaka inavyosonga mbele, ndivyo zao hilo linakuwa linavyozidi kuongezeka thamani, kutokana na mahitaji yake kuongezeka kadri siku zinavyoongezeka, kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Linazidi kuwa na thamani katika soko la kimataifa.
Historia ya nchi inaonyesha kuwa mkonge umekuwa ukimwa kwa sehemu kubwa ta mikoa ya Morogoro na Tanga.
Wakati bado haijatoweka kabisa katika mikoa hiyo miwili, imeanza kuibuka tena kwa kasi katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, ambako kuna kilimo kilichopamba moto.
Kasi yake imefika hatua ya kuchukua sura ya kuchuana na pamba inayolimwa kwa wingi huko kama zao la biashara.
KUTOKA KWA WAKULIMA
Suzan Jinyange (53), ni mkulima wa katani na msindikaji wa zao hilo kutoka wilayani Kishapu.
Anasema mkonge umewaongezea mafanikio wakulima wilayani humo na anatoa mfano binafsi kwamba akiwa mama aliyeolewa na mwenye watoto sita, amejikita katika kilimo hicho tangu mwaka 2013.
“Nilikuwa nalima mazao ya kawaida, lakini nilipoanza kulima zao la mkonge na kusindika, nimepata mafanikio makubwa,” anasema.
Jinyange anasema kuwa amepanda robo tatu ya ekari za zao hilo na ananunua mkonge kwa wakulima wengine kiasi cha ekari mbili kwa ajili ya kusindika.
Anasema kwa mwaka ana uwezo wa kusindika tani 10 anazoziuza kwa kampuni za mkonge na bei yake kwa kilo ni kati ya Sh. 800 hadi Sh. 1,000 na uliosindikwa unafikia bei zaidi ya Sh. 1,200 hadi Sh. 1,300.
“Nalishukuru shirika la Oxfam kupitia miradi yao, kwani limetupatia elimu juu ya zao hili, kwa sababu ardhi yetu ni kame mno. Tulikuwa tunapata hasara na kujikuta maendeleo ya kiuchumi yanarudi nyuma kila siku,” anasema.
Mkulima huyo anasema utaratibu wa sasa, wanapopanda mikonge kati eneo la kati, huchanganya na mazao mengine kama vile mahindi, choroko na karanga.
Jinyange anasema shirika hilo kupitia wataalamu wake, imembadilisha maisha kwa kumpatia mashine ya kusindika mkonge na elimu kuhusu kilimo hicho.
“Nimefanikiwa kununua mashamba, kusomesha watoto pamoja na kumuuguza mtoto wangu anayesumbuliwa na saratani ya mguu.
“Nilikuwa sina meno yaling’oka, ila nilipata fedha za kununua meno bandia. Pia nimewaajiri vijana ambao wananisaidia shughuli zangu za kusindika mkonge,” anasema Jinyange.
Mshauri wa Mradi wa Mnyororo wa Zao la Mkonge kutoka shirika la Oxfam, Azimio Mbegu, anasema wamefanya uchambuzi wa chanzo cha mabadiliko ya tabianchi na zao la biashara litakalohimili hali hiyo.
Wakulima kwa kushirikiana na shirika hilo, wamekubaliana zao pekee linalohimili ukame ni mkonge, kwani halishambuliwi na magonjwa.
Kaimu Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wilayani Kishapu,Godwin Evarist, anasema Oxfam lilianza kazi katika wilaya hiyo mwaka 2009.
Anasema ilianza shughuli zake katika vijiji 10 na baadaye ikavifikia vijiji 30, kwa lengo la kuelimisha jamii matumizi ya mkonge.
Evarist anasema mwanzoni walitumia mmea wa mkonge kuweka mpaka baina ya mashamba na sasa imepiga hatua na kuwa na hadhi ya zao la biashara.
Hivi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, imehamasika na imelichukua kuwa sehemu ya uchumi wa wilaya.
MIKAKATI YA MABORESHO
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imeingiza mkonge kwenye mpango mkakati wake, ikiwa ni hanzo cha ndani na imetenga bajeti ya Sh. milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza zao hilo.
Kiasi hicho cha fedha kimedhamiriwa kuviwezesha vikundi vya kinamama kupata pembejeo na mitaji ya kuendeleza biashara zao.
Changamoto inayotajwa kuwapo ni ubaba wa miche ya m ikonge na hivyo, imeanzishwa kitalu chenye miche 25 ya zao hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ng’umbi anasema wilaya itahakikisha zao hilo linapewa kipaumbele, baada ya wakulima kubaini umuhimu wake katika kuwaongezea kipato.
Hawa anasema kupitia mikutano ya hadhara, wamekuwa wakihamasisha kulima mazao mengine, bila ya kusahau mkonge kwa kuwa linastahimili ukame.
“Kampeni ya uhamasishaji imeanza katika shule, kaya na kata kupanda mikonge ekari mbili. Lakini nilishukuru shirika la Oxfam, kwa kutoa elimu kwa wakulima ambao hivi sasa wamepata mafanikio ,”anasema.










